1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uwanja wa ndege wa Mogadishu wafungwa kwa hofu ya mashambulizi

Liongo, Aboubakary Jumaa17 Septemba 2008

Serikali ya mpito ya Somalia imeufunga kwa sehemu kubwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa mjini Mogadishu kufuatia tishio la wanamgambo wa kiislam kuzishambulia ndege zote zitakazoutumia uwanja huo

https://p.dw.com/p/FK44
Wananchi wa mjini Mogadishu wakibeba mwili wa mmoja wa watu waliyouawa katika moja ya mapigano yaliyotokea mjini humoPicha: AP

Kwa mujibu wa wafanyakazi wa uwanja huo wa ndege wa Mogadishu, amri imetolewa ya kutotumika kwa sehemu inayoangalia eneo la bahari katika kujaribu kuepuka vitisho hivyo.


Kundi la Al Shabaab ambalo liko katika orodha ya Marekani ya makundi ya kigaidi, limekuwa likizidisha mashambulizi yake dhidi ya serikali ya mpito nchini humo inayoungwa mkono na Ethiopia.


Kundi hilo lilitangaza kuwa litazilipua ndege zote zitakazoutumia uwanja huo pamoja na kuwaua wafanyakazi wa ndege hizo, likisema kuwa uwanja huo umekuwa ukitumiwa na majeshi ya Ethiopea pamoja na yale ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika kuisaidia serikali ya Somalia wanayotaka kuiondosha madarakani.


Kwa kawaida kati ya ndege nne hadi tano kwa siku hutua na kuruka kutoka katika uwanja huo wa ndege wa kimataifa wa Mogadishu.


Vikosi vya majeshi ya Umoja wa Afrika vimeweka kambi yao katika uwanja huo na vimelaani tishio hilo la kundi la Al Shabaab, likisema kuwa litawaathiri zaidi wananchi kwani litazuia ndege zenye shehena ya madawa kutua.Umoja huo una kiasi cha askari 2,200 idadi kubwa ikiwa ni kutoka Uganda.



Msemaji wa kikosi hicho Barigye Ba-Hoku amesema kuwa kikosi hicho kitaendelea kuutumia uwanja huo ingawaje kwa sasa hakina ratiba yoyote ya ndege zake kutua au kuruka, na kuongeza kuwa,kwao wao uwanja huo bado haujafungwa.


Amesema kuwa tishio hilo la Al Shabaab siyo jipya kwani toka kikosi hicho kilipowasili, uwanja huo umekuwa ni sehemu ya malengo ya wanamgambo hao wa kiislam toka walipoanzisha mashambulizi yao kwa mtindo wanamgambo wa Iraq yaani kujitoa mhanga, mwaka jana.


Mwishoni mwa wiki iliyopita wanajeshi wawili wa kikosi hicho cha Uganda nchini Somalia waliuawa kutokana na shambulizi la bomu la kutegwa ardhini.


Tishio hilo linaashiria kuimarika kwa kundi hilo la Al Shabaab ambalo mwezi uliyopita liliongoza mapambano ya kuutwaa mji wa bandari ya Kismayu uliyoko kusini mwa Somalia, likiwa eneo muhimu kivita lililoko karibu na mpaka wa Kenya.


Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Somalia Ahmedou Ould-Abdallah ambaye yuko nchini Djibouti kujaribu kusaidia kufikia mkataba wa amani kati ya serikali ya mpito na makundi mengine ya upinzani yenye msimamo wa wastan amelaani tishio hilo la Al Shabaab.


Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa ndege yoyote itakayoangushwa, katika uwanja huo wa ndege, kundi la Al Shabaab litawajibika.

Kwa mujibu wa makundi ya haki za binaadam mapigano nchini Somalia yamesababisha kiasi cha watu 838 kuawa toka mwezi June na kufanya idadi ya waliyouawa toka mwaka huu uanze kufikia 9,474.


Yasin Ali Gedi ambaye ni makamu mwenyekiti wa shirika la amani na haki za binaadam nchini Somalia liitwalo Elman anasema kuwa mbali ya vifo hivyo kiasi cha watu 53 walitekwa nyara kati ya hao 51 ni wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada pamoja na waandishi wa habari wawili wa kigeni.


Wiki iliyopita mbunge mmoja wa bunge la Somalia aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa nje ya msikiti mjini Baidoa ambako ndiko makao makuu ya bunge la Somalia.


Mbunge huyo Mohamed Osman Maye inaaminika kuwa alikuwa mfuasi wa Rais Abdullahi Yusuf na ni wa kwanza kuawa toka serikali hiyo ya mpito ilipoingia madarakani kwa msaada wa majeshi ya Ethiopia.


Mwezi uliyopita Umoja wa Mataifa ulisema ya kwamba idadi ya watu wanaohitaji misaada ya kibinaadam kutokana na vita hivyo nchini Somalia ni zaidi ya millioni 3.2