1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dereva mmoja wa WFP auawa Somalia

Kalyango Siraj9 Julai 2008

Maharamia waachilia huru meli waliokuwa wameiteka Somalia

https://p.dw.com/p/EZKQ
Picha ya meli ya mizigo ya Uholanzi iliotekwa nyara 27 May 2008 na maharamia wa kisomali.Meli kama hiyo ya Ujerumani imeachiliwa huru pamoja na wafanyakazi wake wote.Picha: picture-alliance/dpa

Watu wenye silaha wamemuua kwa kumpiga risasi dereva wa lori la kutoa misaada la mpango wa chakula duniani la WFP nje ya mji wa Mogadishu nchini Somalia.

Tukio hili limekuja wakati kukitolewa taarifa kuwa ile meli ya mizigo ya kijerumani iliotekwa nyara katika mwambao wa Somalia mwezi Mei imeachiliwa huru pamoja na watumishi wake wote.

Shirika la mpango wa chakula duniani la WFP linasema kuwa watu wenye silaha wamemuua, kwa kumpiga risasi, dereva wa lori la shirika hilo.

Shirika la WFP linasema gari la dereva huyo lilikuwa sehemu ya mlolongo wa magari mengine ya shirika hilo yaliyokuwa yamebeba tani 602 za chakula cha msaada yakielekea katika maeneo ya Bakool na Bay yakitokea Mogadishu mji mkuu wa Somalia.

Dereva huyo ni wa nne kupigwa risasi nchini humo mwaka huu.Jumapili mkuu wa shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP nchini Somalia aliuawa kwa kupigwa risasi huku mkuu wa ofisi ya Mogadishu ya shirika la umoja wa mataifa linalowahudumia wakimbizi la UNHCR baado anashikiliwa mateka na watu wasiojulikana.

Shirika la WFP limeziomba pande zote husika katika mgogoro wa Somalia, kukubali misaada ya kiutu kupita salama salimini katika maeneo yao.

Mkurugenzi wa ofisi ya Somalia ya WFP,Peter Goossens,amesema kuwa watu wengi nchini humo hutegemea chakula cha msaada kinachotolewa na shirika hilo,lakini ,ameongeza kuwa ,madereva wao huhatarisha maisha yao kukisafirisha .

WFP linasema linapaswa kuzidisha mara dufu juhudi zake nchini humo ili kuweza kukidhi mahitaji ya wasomali takriban millioni Unusu katika kipindi kijacho cha mwaka.

Hata hivyo juhudi zao zinatatizwa na visa vya kuwashambulia watumishi wa shughuli za kimisaada na vilevile uharamia ambao umezidi katika mwambao wa Somalia.

Kwa mda huohuo meli ya mizigo ya kijerumani iliotekwa nyara mwezi Mei karibu na mwambao wa Somalia imeachiliwa huru pamoja na watumishi wake.Hata hivyo mmiliki wa meli hiyo hakutoa taarifa zaidi kuhusu mazingira yaliyopelekea kuachiliwa huru kwa meli yake.

Meli hiyo ambayo ilisajiliwa nchini Gibralter ilitekwa nyara Mei 28 na mahariamia wakisomali katika ghuba la Ajemi ikiwa na wafanyakazi wake 15 ambao ni raia wa Urusi,Estonia, Ukraine na Mynmar.

Kampuni ya meli ya Hans Lehmann KG,katika taarifa ilioitoa, imesema kuwa meli hiyo ilikuwa inaelekea mahali salama ambapo watumishi wake baadae watapimwa afya zao.

Meli hiyo iliotekwa nyara wakati ilipokuwa inaelekea katika mfereji wa Suez nchini Misri.Imekuwa ikizuiliwa na maharamia kwa siku 41.

Hata hivyo wenye meli wamekataa kufichua mazingira ya kuachiliwa huru kwa meli hiyo wakisema hawataki kuhatarisha hatua za hapo baade za uokozi.

Maeneo ya karibu na mwambao wa Somalia ni miongoni mwa maeneo hatari duniani,kutokan na kuwa taifa hilo limekuwa halina serikali kwa kipindi cha takriban miaka 17.

Shirika la safari za meli la kimataifa linasema kuwa zaidi ya meli 25 zilitekwa nyara mwaka jana katika mwambao wa Somalia unaokisiwa kuwa na urefu wa kilomita elf tatu na mia saba.

Na hayo yakiarifiwa Umoja wa Afrika unataka Umoja wa Mataifa kuziwekea vikwazo pande zote ambazo zinakwamisha utekelezwaji wa usitishwaji mapigano nchini Somalia uliofikiwa mwezi jana .