Uvamizi wa Uturuki na Maoni ya Vijana Magazetini | Magazetini | DW | 16.10.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Uvamizi wa Uturuki na Maoni ya Vijana Magazetini

Uvamizi wa Uturuki nchini Syria, uwezekano wa Umoja wa Ulaya kuzidisha wanachama, au kujipanua kama inavyotajwa, na utafiti wa maoni ya vijana kuhusu siasa, maisha ya jamii na mazingira ni miongoni mwa mada magazetini

Tunaanzia kaskazini mwa Syria ambako Uturuki inaendelea na opereshini zake za kutenga eneo la usalama ili kuitenganisha nchi yake na wanamgambo wa kikurd wanaoishi katika eneo hilo. Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linazungumzia balaa linaloweza kutokea na kuandika: "Kaskazini mwa Syria vikosi vya nchi moja mwanachama wa jumuia ya kujihami ya NATO vitajikuta hivi karibuni vikikabailiana na vile vya nchi mshirika wa Urusi. Uamuzi wa kuacha kuipatia serikali ya mjini Ankara silaha ingawa ni wa maana lakini hautoshi.  Hakuna aliyewahi kufikiria kwamba itawadia siku ambapo wanachama wa jumuia ya kujihami watalazimika kuwekeana vikwazo vya silaha. Jumuia hiyo inabidi ijitafakari na kuchukua hatua zinazostahiki. Mbali na hayo mzozo huu unaonyesha kuzidi makali na sio tu katika eneo hilo la mapigano. Watu takriban milioni tatu-wenye asili tangu ya kituruki mpaka ya kikurd wanaishi nchini Ujerumani. Uhusiano kati yao haujawahi kuwa mfano wa kuigizwa; kutokana na  kile kinachotokea kaskazini mwa Syria, watu hawawezi kuondowa uwezekano wa kuripuka wakati wowote ule ghadhabu au hata matumizi ya nguvu kati yao. Kilichotokea katika mji wa Herne katika mkoa wa mto Ruhr jumatatu iliyopita, ni mfano mdogo tu wa kile kinachoweza kujiri."

Albania na Macedonia zaomba kuwa wanachama wa Umoja wa Ulaya

Mjadala umepamba moto miongoni mwa wanachama wa Umoja wa Ulaya kama jumuia hiyo ijipanue na kuzikubalia uwanachama nchi mbili zaidi au la. Kuna wanaounga mkono na bila ya shaka kuna wanaopinga pia. Nje ya Umoja wa ulaya kuna wanaosubiri waidake fursa itakayojitokeza. Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linaandika: "Suala linalojitokeza ni jee ufumbuzi wa maana unakutikana wapi, ndani au nje ya Umoja wa ulaya? Wawe wanachama kamili au si kamili kwasababu ya masuala ya kisiasa ya nchi zinazoomba uanachama?

Ikiwa mataifa ya magharibi mwa Balkan, Slovenia na Kroatia zimeshakubaliwa na Serbia inasubiri kukubaliwa, vipi majirani zao watakataliwa? Na ikiwa masharti yameshakamilika ? Hata kama juhudi za kujumuika zina mashaka-kama kadhia ya Uturuki ilivyobainisha, au hata kushindwa-hata hivyo kinachobidi kuzingatiwa zaidi ni hoja za sera ya kikanda. IKiwa Umoja wa ulaya utasita sita, wengine wataidaka fursa hiyo: Urusi, China na Uturuki wanavizia tu."

Tofauti za maoni miongoni mwa vijana zinabainisha chanzo kiko wapi

Utafiti wa maoni uliosimamiwa na taasisi ya Shell kuhusu jinsi vijana wanavyovutiwa na siasa, maisha ya jamii na mazingira, umebainisha pengo kubwa lililoko kati ya vijana wanaotokea katika familia za wasomi na wale ambao wazee wao hawakubahatika kufika mbali shuleni. Gazeti la "Weser-Kurier" linaandika: "Wanasiasa na jamii wanabidi wawahusishe zaidi vijana na kuwajumuisha maamuzi yanapopitishwa. Hiyo ndio njia mojawapo inayoweza kuwafanya vijana wavutiwe zaidi na mfumo wa kidemokrasi na vyama vya kisiasa. Zaidi ya hayo wanasiasa wanabidi wayashughulikie zaidi pia masuala yanayowahusu vijana."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri: Sekione Kitojo