Ushawishi wa viongozi wa kidini katika serikali ya Irak waongezaka | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 11.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Ushawishi wa viongozi wa kidini katika serikali ya Irak waongezaka

Viongozi wa kidini wameanza kuwa na ushawishi mkubwa nchini Irak. Wairaki wengi sasa wanahofia viongozi hao ni tishio kwa haki za binadamu na uhuru wa kidini katika nchi iliyokuwa zamani kwa kiwango kikubwa nchi ya kilimwengu.

Waziri mkuu wa Irak Nouri al-Maliki

Waziri mkuu wa Irak Nouri al-Maliki

Viongozi wa kidini walianza kuwa na jukumu kubwa tangu uvamizi wa Irak ulioongozwa na Marekani mnamo mwezi Aprili mwaka mwaka wa 2003. Licha ya ahadi za rais George W Bush kuibadili Irak kuwa taifa huru na lisiloegemea dini, mashehe wa kiislamu ndio wamekuwa viongozi halisi na wameanza kusimamia maswala mengi ya kisiasa.

Shakir Hamdan, mtaalamu wa maswala ya kiislamu mjini Baghdad amesema ni bahati mbaya kwa Wairaki wote kwamba jumuiya ya kimataifa imewaleta viongozi wa kidini madarakani. Hamdan amesema viongozi hao wataielekeza nchi katika vita vya kikabila na kuirejesha nyuma katika karne za zamani ambapo mtu mmoja anatawala na uhuru unapotea.

Hamdan ameutaja mkutano wa hivi majuzi kati ya waziri mkuu wa Irak, Nuri al Maliki na shehe mkuu wa madhehebu ya Shia, Ayatollah Ali al Sistani katika mji mtakatifu wa Najaf, ambapo maswala ya serikali yalijadiliwa. Hii inadhihirisha ushawishi mkubwa wa viongozi wa dini katika maswala ya serikali. Serikali pamoja na bunge haiwezi kupitisha uamuzi wowote bila kushauriana na mashehe.

Irak ilikuwa kwa kiwango kikubwa nchi ya kilimwengu wakati wa utawala wa rais wa zamani Saddam Hussein, ikizingatiwa hofu ya Saddam kwamba viongozi wa dini wangehujumu utawala wake. Uvamizi na kukaliwa kuliiharibu Irak na taasisi zake hivyo kuacha pengo la madaraka lililojazwa na viongozi wa kidini waliotoa huduma msingi ambazo serikali haingeweza kuzitoa.

Munthir Sulayman, mtetezi wa mageuzi ya kijamii katika mji mkuu Baghdad, anasema nchi yao imegeuka kutoka taifa la kilimwengu na kuwa nchi ya kidini. Aidha mtetezi huyo amesema walitumai Irak ingepata maendeleo makubwa katika maswala ya jamii na kuwa nchi ya kisasa iliyo huru, ambapo raia wangeweza kushiriki katika siasa, uchumi na maswala yote yanayohusiana na maisha. Lakini kilichotokea ni kinyume cha matumaini hayo na Irak sasa inadhibitiwa na mashehe.

Wasomi kadhaa na viongozi wa kijamii wanasema wamepoteza jukumu lao la kujaribu kuboresha mfumo wa kisiasa na kijamii nchini Irak.

Kundi kubwa la mashehe wa madhehebu ya Sunni linakanusha kwamba viongozi wa kidini wanajaribu kuchukua nafasi ya serikali. Naibu katibu mkuu wa kundi hilo, Dakta Abdul Salam al Kubayssi anasema Irak inahitaji kuongozwa na watu wenye uzoefu na elimu ya njia za mageuzi na ujenzi.

Aidha kiongozi huyo amesema lengo lao ni kuisadia serikali inayoingoza nchi hiyo kufikia usalama na maendeleo pasipo kuisimamia wala kuiingilia katika utendaji wake. Kuitawala Irak ni kibarua kigumu ambacho hakiwezi kufanywa na kundi la maimamu.

Lakini vikosi ya Marekani na viongozi wao wamekuwa wakiwategemea mashehe tangu siku za mwanzo za kuikalia Irak. Baraza kuu la Irak liliwajumulisha mashehe kama vile Ayatollah Bahrul-Uloom na Abdul Aziz al-Hakim, pamoja na viongozi wengine wa vyama vya kiislamu kama vile al-Dawa na chama cha kiislamu cha Irak. Uchaguzi wa mwaka juzi 2005 karibu wote ulisamamiwa na makundi ya kidini na vyama vyao vya kisiasa.

Vyama vya kishia, hususan baraza kuu la kiislmu la Irak, likiongozwa na Hakim, lilimnukulu al Sistani akiwatolea mwito waumini waipigie kura orodha ya muungano wa vyama vya kishia. Orodha hiyo inaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ya sasa ya Irak. Marekani na wasimamizi wa uchaguzi wa mwaka juzi hawakufanya mengi kuzuia mgawanyiko huo wa kimadhehebu.

Fadhil Yassen, wakili wa mjini Baghdad anasema ilikuwa njama ya Marekani tangu mwanzo kushirikiana na mashehe ili kuidhibiti hali nchini Irak. Sasa Wairaki na Wamarekani wanalipa gharama kubwa kupitia damu yao na mali zao. Maimamu wa kishia wenyewe wamegawanyika na makundi hasimu ya kishia yanapigania madaraka katika maeneo ya Washia mjini Baghdad na kusini mwa Irak.

 • Tarehe 11.09.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB1P
 • Tarehe 11.09.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB1P

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com