Urusi yataka kuimarisha jeshi lake na inasema haina tamaa za kibeberu | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 11.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

IDHAA YA KISWAHILI

Urusi yataka kuimarisha jeshi lake na inasema haina tamaa za kibeberu

Wakati Rais Dmitry Medvedev wa Urusi akisema Urusi kulipatia jeshi lake zana za kisasa ni kipau mbele cha kwanza Waziri Mkuu wake Vladimir Putin amesema haina tamaa za kibeberu.

default

Vikosi vya Urusi vikiwa Ossetia Kusini.

Mzozo uliosababisha vita vya Georgia bado unaendelea kufukuta huku majimbo ya zamani ya Urusi yakiwa na wasi wasi nayo yasije yakawakuta yale yaliotokea Georgia.

Rais Medvedev wa Urusi amesema katika mkutano wa Ikulu ya Urusi na kukaririwa na shirika la habari la Interfax kwamba wanapaswa kuweka nadhari katika masuala ya zana za kijeshi na kwamba bila ya shaka uamuzi huo umechochewa na mzozo katika eneo la Caucasis ,uvamizi wa Georgia na kuendelea kwake kujiimarisha kijeshi.

Amesema wanahitaji jeshi la kisasa lenye ufanisi na kwamba hilo ni mojawapo ya malengo makuu ya taifa.

Naye Waziri Mkuu wa Urusi Vladimir Putin amesema Urusi haina tamaa za kibeberu huku kukiwa na wasi wasi katika nchi kama vile Ukraine kufuatia mzozo wa mwezi uliopita nchini Georgia.

Putin ameuambia mkutano wa maafisa wa serikali na wataalamu katika kikao kwenye mji wa kitalii wa Sochi huko Bahari Nyeusi kwamba hawana na hawatokuwa na tamaa zozote zile za kibeberu ambazo watu wanajaribu kuwashutumu nazo.

Amesema kushindwa kuchukuwa hatua kwa Urusi kungelishajiisha machafuko katika maeneo ya kaskazini ya Urusi,katika majimbo kadhaa na makundi mbali mbali ya kikabila wakiwemo Wachechnya.

Urusi hapo mwezi wa Augusti ilituma vikosi vyake katika jimbo la waasi la Ossetia Kusini na ndani mwa ardhi ya Georgia kwa kile ilichosema ni hatua ya kuwalinda raia wake.

Serikali ya Urusi ilitupilia mbali shutuma kutoka mataifa ya magharibi kwamba lengo lake lilikuwa ni kutwaa sehemu za Georgia na imeishutumu Marekani kwa kuchochea vita hivyo kwa kule kuipatia Georgia silaha kabla na baada ya kuzuka kwa mzozo huo.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa na mwenzake wa Urusi Dmitry Medvedev waikubaliana juu ya kuondolewa kwa vikosi vya Urusi kutoka magharibi mwa Georgia wiki hii lakini Urusi na Umoja wa Ulaya zimekuwa zikitafautiana juu ya uwekaji wa waangalizi wa umoja huo katika eneo hilo.

Mvutano wa kimataifa juu ya Georgia umezidi kupamba moto wakati Urusi ikishutumu serikali ya Ukraine inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi kwa kuchukuwa msimamomwa uhasama na kukiuka haki za waakazi wanaozungumza Kirusi nchini humo.

Maafisa wa mataifa ya magharibi kabila kubwa la Warusi walioko Ukraine wanaweza kuwa rahisi kuingiliwa na serikali ya Urusi kwa ajili ya sababu ya kuwahami huku kamishna anayehusika na kutanuka kwa Umoja wa Ulaya akionya kwamba Ukraine inaweza kuwa nchi ya pili kushambuliwa na Urusi.

Marekani imesema Urusi imekiuka dhahiri makubaliano ya kusitisha mapigano kutokana na uamuzi wake wa kuweka wanajeshi 7,600 katika majimbo yaliojitenga ya Georgia ya Abkhazia na Ossetia Kusini kwa mipango ya muda mrefu.

Urusi ambayo inatambuwa majimbo hayo kuwa huru kufuatia kuzuka kwa mzozo huo imekubali kuondowa vikosi vyake kutoka maeneo yaliotengwa yasio ya mapigano yaliozunguka majimbo hayo yanayotaka kujitenga kufikia tarehe Mosi Oktoba iwapo waangalizi wa amani wa Umoja wa Ulaya watakuwa wamewekwa.

 • Tarehe 11.09.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FGHM
 • Tarehe 11.09.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FGHM
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com