Urusi yahimiza uvumilivu mzozo wa Iran na Marekani
29 Januari 2026
Urusi imesema hivi leo kwamba bado kuna nafasi ya mazungumzo kutatuwa mvutano kati ya mshirika wake Iran na Marekani baada ya rais Donald Trump kutishia kuishambulia Jamhuri hiyo ya kiislamu.
Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov amewaambia waandishi habari kwamba kuna uwezekano wa wazi wa kufanyika mashauriano kati ya pande hizo mbili na kutowa mwito wa kuvumiliana.
Wasiwasi wa kitisho cha Marekani kuishambulia Iran
Urusi pia imesema iko tayari kuondowa wafanyakazi wake katika kituo cha Nyuklia cha Buscher nchini Iran ikihitajika. Kwa upande mwingine Uturuki ambayo imetangaza kujiandaa kuimarisha usalama kwenye mpaka wake ikiwa mzozo huo utaongezeka, imejitolea kuwa msuluhishi kati ya Washington na Tehran.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Aragchi ambaye anaitembelea Ankara kesho Ijumaa amesema vikosi vya nchi yake viko tayari kujibu mashambulio ikiwa Marekani itashambulia.