1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala wapanuka kuhusu uwezo wa silaha za kivita Iran

Michael Kwena
26 Machi 2026

Vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vimeingia wiki ya nne, huku mjadala ukizidi kuhusu uwezo wa makombora na droni za Iran licha ya mashambulizi yake kuendelea Israel na Ghuba.

https://p.dw.com/p/5BCTH
 Makombora ya Iran I RGC
Makombora ya Iran yakifyatuliwa wakati wa mazoezi ya kijeshi kabla ya vita.Picha: Irgc Official Webiste/ZUMA/IMAGO

Licha Marekani na Israel kutangaza kwamba uwezo wa kijeshi wa Iran umesambaratishwa, mashambulizi ya Iran bado yanaendelea ndani ya Israel na katika eneo la Ghuba. 

Mnamo Machi 14, Ikulu ya Marekani ya White House ilidai kuwa uwezo wa makombora ya balistiki ya Iran ulikuwa umeharibiwa kwa kiasi kikubwa, lakini Iran imeendelea kurusha makombora hayo hata baada ya kauli hiyo.

Kwa mujibu wa Burcu Ozcelik, mchambuzi wa usalama wa Mashariki ya Kati kutoka taasisi ya RUSI, uwezo wa Iran umedorora, lakini haujaisha kabisa.

Hakuna takwimu kamili kuhusu idadi ya makombora ya Iran yaliyosalia. Jeshi la Israel lilidai Iran ilikuwa na takriban makombora 2,500 kabla ya vita, wakati wataalamu wengine wanakadiria hadi 6,000.

Iran ilijulikana kuwa na hazina kubwa zaidi ya makombora katika Mashariki ya Kati, ikiwa na mifumo kama Sejjil, Ghadr, Khorramshahr, Shahab-3 na Emad.

Kwa mujibu ripoti ya kijasusi kutoka Marekani, Iran ilikuwa na mifumo ya makombora yanayoweza kufika umbali kati ya kilomita 1,300 hadi 2,000, na hata zaidi ya kilomita 3,500.

Hata kama mashambulizi ya Marekani na Israel kwenye viwanda vya kutengeneza makombora na maghala ya silaha ya Iran yamepunguza uzalishaji wa Iran, bado haijabainika ni kwa kiwango kipi.

Droni za Shaheed katikati ya vita vya wiki nne

Kwa upande wa droni, Iran ilikadiriwa kuwa na karibu droni elfu 80 za Shahed kabla ya vita kuzuka. Droni hizo zimekuwa nguzo muhimu za kimkakati kwa Iran kwa sababu ni za bei nafuu, na ni rahisi kuzizalisha, na ni vigumu kuzizuia. Mara nyingi gharama ya kuangusha droni moja ni kubwa kuliko droni yenyewe, jambo linaloipa Iran faida ya gharama kwenye uwanja wa vita.

Athari za Makombora ya Iran kwa Uchumi wa Afrika Mashariki

Kwa mujibu wa mtaalamu wa usalama na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Portsmouth nchini Uingereza, Matthew Powell, Iran ina uwezo wa kutengeneza hadi droni 10,000 za Shahed kila mwezi, ingawa kasi hiyo huenda imeshuka kutokana na mashambulizi ya kijeshi kutoka kwa Marekani na Israel. Makombora, kwa upande mwingine, ni ya gharama kubwa na changamoto zaidi kutengeneza.

Maafisa wa Iran wanasisitiza kuwa uzalishaji wa makombora unaendelea licha ya vita, ingawa madai hayo hayawezi kuthibitishwa nje ya Tehran. Kauli hiyo ilirejelewa hivi karibuni na msemaji wa IRGC, Ali Mohammad Naini, ambaye baadaye aliripotiwa kuuawa katika mashambulizi yanayoendelea nchini humo.

Mbali ya kuyazuwia mashambulizi ya sasa, malengo ya Marekani na Israel ni pamoja na kuudhoofisha uwezo wa Iran wa kujijenga upya baada ya vita. 

Hata hivyo, ukosefu wa uwazi wa Iran, miundombinu yake ya chini ya ardhi, na uwezo wake wa kutengeneza droni kwa wingi unaiacha dunia ikiwa na taswira isiyo kamili kuhusu uwezo wake halisi wa kijeshi uliosalia.