Iran yathibitisha kifo cha mkuu wa usalama Larijani
18 Machi 2026
Larijani alikuwa akichukuliwa kama mmoja ya watu wenye ushawishi mkubwa sana nchini Iran tangu Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei alipouawa katika siku ya kwanza ya vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Sehemu ya taarifa ya kifo cha Larijani ilisomwa na mtangazaji wa habari ambaye hakujitambulisha ilisema "Roho za watakatifu za mashahidi zilikumbatia roho safi ya mtumishi mwadilifu wa Mungu, shahidi Dkt. Ali Larijani. Na baada ya maisha ya mapambano kwa ajili ya maendeleo ya Iran na Mapinduzi ya Kiislamu, hatimaye alitimiza ndoto yake ya muda mrefu. Na amejiunga na kiongozi wa mashahidi na jihadi dhidi ya Marekani na Israel Ayatollah Seyyed Ali Khamenei, mwalimu wake aliyeuawa kishahidi, Ayatollah Motahari na wenzake waliouawa kishahidi Seyyed Hassan Nasrallah na Haj Qasim Soleimani."
Tehran imesema Larijani, mwanawe na walinzi wake kadhaa walifariki katika shambulizi hilo la Jumanne. Baraza la Usalama la Iran lilimpongeza Larijani kwa utumishi uliotukuka wa miaka mingi.
Larijani, spika wa zamani wa bunge na mshauri mkuu wa sera, alikuwa akimshauri Khamenei kuhusu mazungumzo ya nyuklia na utawala wa Rais Donald Trump. Aliwekewa vikwazo na wizara ya fedha ya Marekani mwezi Januari kwa jukumu lake la "kuratibu" ukandamizaji dhidi ya waandamanaji mwezi huohuo.
Tehran yathibitisha kifo cha Jenerali Gholamreza Soleimani
Shirika la habari la Fars nalo lilichapisha taarifa ya kifo cha Jenerali Gholamreza Soleimani. Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi walimtolea heshima na kumpongeza kwa "kuuawa kama shahidi," na kuongeza kuwa wapiganaji wa Basij kamwe hawataacha kulipiza kisasi kutokana na kifo cha kiongozi wao. Vikosi Basij vikiongozwa na Soleimani ndivyo vilihusika na hatua kali dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakiipinga serikali ya Iran mnamo Januari.
Hili ni pigo kubwa lililolenga kudhoofisha hata zaidi uongozi wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu, inayokabiliwa na mtihani mkubwa zaidi katika miongo kadhaa.
Mataifa ya Ghuba yaendelea kukabiliwa na mashambulizi kutoka Iran
Mbali na taarifa hizo za vifo, Mataifa ya Ghuba yameendelea kukabiliwa na mashambulizi ya makombora na droni kutokea Iran jana Jumanne, ambayo ilikuwa ikilenga miundombinu ya mafuta. Israel pia ilifanya mashambulizi mapya nchini Iran na Lebanon. Nchini Iraq, maafisa wanasema droni kwa mara nyingine zilishambulia ubalozi wa Marekani ulioko mjini Baghdad. Iraq imeyashutumu makundi yaliyopigwa marufuku kwa mashambulizi ambayo imeyataja kuwa ni ugaidi dhidi ya uhuru wa nchi.
Mjini Tel Aviv, kikosi cha dharura kimearifu kuwa watu wawili wameuawa katika mashambulizi ya makombora ya Iran, kufuatia ripoti kutokea kwenye maeneo kulikofanyika mashambulizi ndani na yanayouzunguka mji huo. Taarifa ya awali ilisema majeruhi wawili walikuwa na hali mbaya, huku polisi ikithibitisha kuanguka kwa vipande vya risasi kwenye mitaa ya Tel Aviv.
Na huko Dubai, kumesikika vishindo kwenye maeneo kadhaa hii ikiwa ni kulingana na mamlaka ambazo zimesema mifumo ya ulinzi wa angani imekuwa ikidhibiti vitisho vya makombora na droni kutokea Iran. Umoja wa Falme za Kiarabu umesema umelengwa na zaidi ya droni 2,000 pamoja na makombora ya Iran tangu vita vilipoanza.