Wakenya 19 wauawa wakipigana vita vya Ukraine
8 Mei 2026
Serikali ya Kenya imesema raia wake 19 wamefariki dunia wakipigana katika mstari wa mbele wa vita vya Ukraine huku wengine 32 wakiripotiwa kutoweka, hali inayozidisha wasiwasi kuhusu ongezeko la Wakenya wanaojiunga na jeshi la Urusi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi amesema idadi ya Wakenya waliojiunga na jeshi la Urusi imeongezeka hadi 291 kutoka takwimu ya awali ya 250.
Akizungumza mbele ya kamati ya Seneti Alhamisi, Mudavadi alisema serikali inaendelea kufuatilia taarifa za Wakenya waliotumwa kupigana katika vita hivyo, huku akithibitisha kuwa watu 53 tayari wamerejeshwa nyumbani kutoka Urusi.
"Mambo zaidi yameendelea kufichuka kuhusu waliotumikia vikosi maalumu vya Urusi,” alisema Mudavadi mbele ya wajumbe wa Seneti.
Aliongeza kuwa watu 19 wanaaminika kufariki nchini Urusi huku wengine 32 wakihesabika kuwa hawajulikani walipo baada ya kutumwa vitani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya amethibitisha kuwa vifo hivyo vilitokea katika uwanja wa vita nchini Ukraine. Aidha, Mudavadi amesema Wakenya wawili wanashikiliwa nchini Ukraine kama wafungwa wa vita.
Ahadi za kazi zageuka vita
Kwa mujibu wa vyombo vya usalama vya Kenya, idadi halisi ya Wakenya waliojiunga na jeshi la Urusi inaweza kuwa kubwa zaidi. Ripoti za kiintelijensia zinaonyesha kuwa zaidi ya Wakenya 1,000 huenda wamehusishwa katika mpango huo baada ya kurubuniwa kwa ahadi za kazi zenye mishahara mikubwa nchini Urusi.
Chunguzi mbalimbali za kimataifa zimeonyesha kuwa mawakala wanaohusishwa na Urusi wamekuwa wakivutia vijana kutoka mataifa ya Afrika kwa ahadi za ajira nzuri, lakini baada ya kufika huko hulazimishwa kujiunga na jeshi na kupelekwa mstari wa mbele wa vita dhidi ya Ukraine.
Taarifa hizo zimezua mjadala mkubwa nchini Kenya huku familia nyingi zikihofia usalama wa ndugu zao waliokwenda Urusi kutafuta kazi.
Kenya yaishinikiza Urusi
Mudavadi alitembelea Moscow mwezi Machi ambako alifanya mazungumzo na maafisa waandamizi wa Urusi kuhusu kile Nairobi imekiita kuwalazimisha Wakenya kujiunga na jeshi la Urusi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Abraham Korir Sing'Oei amekosoa vikali hatua hiyo akisema matumizi ya Wakenya kama "chakula cha mizinga” vitani hayakubaliki.
Kauli hiyo imeongeza shinikizo kwa serikali ya Kenya kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya mitandao ya usafirishaji wa vijana wanaopelekwa Urusi kwa madai ya ajira.
Vita vya Ukraine vyawavuta Waafrika
Tangu kuanza kwa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, mataifa kadhaa ya Afrika yameripoti visa vya raia wao kuhusishwa katika mapigano hayo baada ya kupewa ahadi za kazi za ujenzi, ulinzi au huduma nyingine.
Mashirika ya haki za binadamu yanaonya kuwa vijana wengi kutoka Afrika wanaingia katika mazingira hatari kutokana na ukosefu wa ajira na hali ngumu ya maisha katika nchi zao.
Wachambuzi wa usalama wanaonya kuwa ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa, mtandao huo unaweza kuendelea kuwalenga vijana wa Afrika Mashariki wanaotafuta ajira nje ya nchi.