1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yakana kuwasajili wapiganaji kutoka Afrika

20 Februari 2026

Serikali ya Urusi imejitenga na madai ya kuwasajili Wakenya wanaojiunga na jeshi lake katika vita vyake dhidi ya Ukraine.

https://p.dw.com/p/599S2
Kenia Nyeri 2026 | Mutter trauert um ihren in Russlands Krieg gegen die Ukraine gefallenen Sohn
Urusi imeeleza kusikitishwa kwake na ripoti zinazoihusisha moja kwa moja na njama ya kuwalaghai Wakenya kujiunga na vikosi vyake vya ulinzi. Picha: Andrew Kasuku/AP Photo/picture alliance

Katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye ukarasa wa kijamii wa X,Ubalozi wa Urusi nchini Kenya umejitenga na madai ya kuwapa wakenya visa vya kusafiri ili kujiunga na vikosi vyake vya ulinzi. Taarifa hiyo aidha imetaja ripoti hizo kama propaganda ambazo zimekuwa zikisambazwa nchini humo.

Kauli yao inakuja wakati ambapo idara za Ujasusi na Jinai za Kenya zikiwa tayari zimewasilisha ripoti zao bungeni siku ya Jumatano na kubainisha kwamba angalau Wakenya 1000 walisajiliwa kujiunga na jeshi la Urusi.

Kulingana na ripoti yao, usajili huo haukufuata utaratibu wa kisheria huku wengi wa vijana wakidaiwa kuhadaiwa na mashirika ya uajiri kwa ushirikiano na baadhi ya maafisa wa Urusi kwenye sakata hiyo ambayo sasa imezua hamaki kubwa miongoni mwa wakenya.

Kenia Besuch des deutschen Bundeswirtschaftsminister Habeck
Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Musalia Mudavadi anatarajiwa kusafiri Moscow kufuatia sakata la Wakenya kulaghaiwa na kujiunga na jeshi la UrusiPicha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Familia nyingi za Wakenya walioripotiwa kujiunga na jeshi la Urusi, zimekuwa zikiishinikiza serikali kuwarejesha wapendwa wao ama hai au maiti nchini mwao. Jana Alhamisi, familia za Wakenya 35 waliohadaiwa kujiunga na jeshi la Urusi walishiriki maandamano ya amani jijini Nairobi wakiitaka serikali kupitia wizara ya masuala ya kigeni kuwarejesha vijana hao nyumbani.

Mashirika yanayowalenga maafisa wastaafu wa Polisi

Kiongozi wa walio wengi katika bunge la taifa hilo Kimani Ichungwa aliwaambia wabunge kwamba, kuna mashirika laghai ambayo yamekuwa yakiwalenga maafisa wastaafu wa polisi, wanajeshi na hata raia na kuwaaahidi kazi ughaibuni kwenye sakata yao.

Mbunge hiyo kadhalika, alisema, mashirika hayo laghai yamekuwa yakishirikiana na wafanyikazi kwenye viwanja vya ndege pamoja na maafisa wa idara ya uhamiaji kufanikisha sakata hiyo ambayo imekuwa ikiwalenga vijana kutoka bara la Afrika.

Vita vya Urusi vya Ukraine
Urusi imetuhumiwa kuwasajili Wakenya kupigana upande wake katikavita vyake na UkrainePicha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/picture alliance

"Mashirika hayo yamekuwa yakiwavutia Wakenya kwa kuwaahidi ajira na mishahara ya takribani shilingi 350,000 kwa mwezi na marupurupu Makubwa kati ya shilingi laki 9 hadi shilingi milioni 1.2, pamoja na hatimaye kupewa uraia wa Urusi. Hadi sasa, zaidi ya Wakenya 1,000 wameajiriwa na kusafiri kwenda kupigana kwenye vita vya Urusi na Ukraine."

Wakenya zaidi ya 20 hawajulikani waliko

Kulingana naye, Wakenya 39 wamelazwa hospitalini nchini Urusi baada ya kujeruhiwa kwenye vita, 28 hawajulikani waliko na wenginne 89 wakiripotiwa kuwa katika uwanja wa vita nchini Ukraine. Kwa mujibu wa mratibu wa familia hizo, Peter Kimani, ambaye kaka yake ni miongoni mwa waliopotea, familia kadhaa za Wakenya waliosafiri kuelekea Urusi zimetangaza kuwasilisha maombi kwenye ofisi za serikali na ubalozi wa Urusi wiki ijayo kushinikiza kurejeshwa kwao.

Serikali ya Kenya imelaani kutumiwa vibaya kwa raia wake na Waziri wa masuala ya kigeni Musalia Mudavadi tayari anatarajiwa kuelekea Moscow mwezi ujao kujadili mustakabali wa Wakenya hao.