Iran inayatafakari mapendekezo mapya ya Marekani
7 Mei 2026
Tathmini hiyo inafanyika wakati Rais wa Marekani Donald Trump akitishia kuanzisha wimbi jipya la mashambulizi, kama hatua ya kushinikiza makubaliano ya kusitisha vita pamoja na kuufungua Mlango Bahari wa Hormuz. Juhudi za kutafuta ufumbuzi katika mzozo wa Mashariki ya Kati bado zinaendelea wakati Rais wa Marekani Donald Trump akionya kuwa mashambulizi dhidi ya Iran yanaweza kuanza tena iwapo mazungumzo yatavunjika.
Trump kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Socials amesema vita hivyo huenda vikaisha hivi karibuni na kuwa usafirishaji wa mafuta na gesi uliovurugika katika Mlango Bahari wa Hormuz huenda ukaanza tena. Hata hivyo amesema hilo linategemea kama Iran itayakubali mapendekezo ambayo hayakutolewa maelezo.
Akizungumza na waandishi wa habari Trump ameonesha matumaini akisema pande hizo mbili za mzozo zimekuwa na mazungumzo yenye tija. Aidha, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran Esmaeil Baghaei, ameiambia televisheni ya taifa hilo kuwa Tehran inayapinga vikali mapendekezo ya Washington lakini bado inayachunguza.
Kwa upande wake Pakistan ambayo imekuwa ikiratibu mazungumzo ya usuluhishi ya Iran na Marekani imesema inatarajia kuwa makubaliano yatapatikana hivi karibuni. Awali Spika wa bunge la Iran, , ambaye amekuwa akiongoza mazungumzo ya kutafuta mwisho wa mzozo huo aliishutumu Marekani kwa kuweka vizuizi vya majini, shinikizo la kiuchumi na udanganyifu kwa kutumia vyombo vya habari ili kuharibu mshikamano wa Iran kwa lengo la kuilazimisha kusalimu amri.
Mashambulizi yaripotiwa Hormuz licha ya juhudi za kidiplomasia
Wakati Washington na Tehran zikihangaika na hatma ya mzozo wao, Marekani imeishambulia meli ya mafuta ya Iran katika Ghuba ya Oman. Kamandi Kuu ya Marekani kupitia chapisho kwenye mtandao wa kijamii imethibitisha mashambulizi hayo ikidai kuwa meli hiyo ilijaribu kuvunja mzingiro wa Marekani katika bandari za Iran Shambulio hilo limeripotiwa wakati na Marekani zikiwa kwenye makubaliano ya kusitisha vita tangu Aprili 8.
Katika hatua nyingine Ubalozi wa Iran nchini Korea Kusini imekanusha kuwa wanajeshi wake walihusika na mlipuko ulioilenga meli yataifa hilo kwenye Mlango Bahari wa Hormuz wiki hii. Meli hiyo HMM Namu iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Panama iliharibiwa na mlipuko huo kwenye njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta ikiwa na wafanyakazi 24.
Muda mfupi baadaye Rais wa Marekani Donald Trump alinukuliwa akidai kuwa Iran ilifyatua makombora kadhaa dhidi ya meli hiyo. Aidha, aliitolea wito Korea Kusini kushiriki katika juhudi zinazoongozwa na Marekani za kurejesha usalama wa usafirishaji katika Mlango wa Hormuz, ingawa juhudi hizo kwa sasa zimesitishwa.