1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIran

Iran yaendelea kuishambulia UAE, anga lafungwa kwa muda

17 Machi 2026

Kumeshuhudiwa mashambulizi ya makombora na droni huko Umoja wa Falme za Kiarabu siku ya Jumatatu, yaliyomuua mtu mmoja na kuharibu jengo moja kwenye mji wa Umm Al Quwain, kaskazini mwa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/5AW45
Umoja wa Falme za Kiarabu Fujairah 2026 | Moto katika kiwanda cha mafuta baada ya shambulio la ndege zisizo na rubani za Iran
Iran imeendeleza mashambulizi kwenye Umoja wa falme za Kiarabu katikati ya vita vyake na Marekani na IsraelPicha: AFP

Mashambulizi hayo yanafanywa siku moja baada ya mwanadiplomasia mkuu wa Iran Abbas Araghchi kusema kambi za Marekani zilizopo Mashariki ya Kati zimekuwa zikitumika kwa mashambulizi dhidi yao. Lakini Umoja wa Falme za Kiarabu unakana madai hayo.

Usambazaji wa gesi katika kinu cha Shah umesitishwa kutokana na mashambulizi ya droni, na sasa mamlaka zinatathmini athari, hii ikiwa ni kulingana na vyombo vya habari vya Abu Dhabi. Kinu hicho ni moja ya vinu vikubwa kabisa na cha kipekee kilichopo kama kilomita 180 kusinimagharibi mwa Abu Dhabi.

Mapema leo, mamlaka ya UAE zilitangaza kufunga kwa muda anga lake kufuatia wasiwasi wa usalama kwenye kanda hiyo baada ya wizara ya ulinzi kusema ilikuwa ikikabiliana na vitisho vya makombora na droni kutokea Iran. Hata hivyo, baadae safari za ndege zilirejea kama kawaida baada ya tahadhari kuondolewa, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la WAM lililonukuu Mamlaka ya Anga ya nchi hiyo.

Iraq yalaani mashambulizi nchini mwake

Iraq Baghdad 2025 | Mohammed Shia al-Sudani akipiga kura yake katika uchaguzi wa bunge
Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia al-Sudani ametaka wahusika wa mashambulizi nchini mwake kufikishwa mikononi mwa sheria mara mojaPicha: Ahmed Saad/REUTERS

Kwa upande mwingine, Iraq imelaani vikali msururu wa mashambulizi ya kigaidi yaliyolenga hoteli ya kitalii  mjini Baghdad na Ubalozi wa Marekani ambao upo kwenye eneo lenye ulinzi mkali pamoja na kisima kikubwa cha mafuta kilichoko kusini mwa taifa hilo Jumatatu jioni, na kuyataja mashambulizi hayo kama vitisho kwa usalama na utulivu wa Iraq. Ni mashambulizi yaliyofanywa siku moja baada ya kundi la Kataeb-Hezbollah linaloungwa mkono na Iran kutangaza kwamba kiongozi wake mwandamizi Abu Al al-Askari ameuawa.

Waziri Mkuu Mohammed Shia al-Sudani ameviagiza vikosi vya usalama kuwasaka wahusika wa mashambulizi hayo na kuwafikisha kwenye mkono wa sheria mara moja ili waadhibiwe, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wake Sabah al-Numan.

Iran kwa upande wake imeonya kulipiza kisasi ikiwa Marekani itafanya mashambulizi zaidi kwenye visima vya mafuta vilivyoko katika kisiwa cha Kharg, amesema msemaji wa vikosi vya jeshi nchini humo Abolfazi Shekarchi. Shirika la habari la Tasmin limeripoti jana kwamba msemaji huyo alisema Iran itashambulia visima vyote vya mafuta na gesi vya taifa lolote litakalojihusisha na mashambulizi kama hayo.

Uswisi Geneva 2026 | Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi akizungumza katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Kupunguza Silaha
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema vita vya sasa vinalenga kumfunza mvamizi aina ya taifa inalokabiliana nalo na hivyo havitamalizika mapemaPicha: Pierre Albouy/REUTERS

Araghchi: 'Tunataka kumfunza mvamizi'

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amenukuliwa akiwashutumu wapinzani wao kwa kujaribu kuilazimisha nchi hiyo "kusalimu amri bila masharti" na kusisitiza kwamba wanataka kuhakikisha vita hivi vinamalizika na hakutatokea vita vingine kama vya sasa.

"Acha niseme tena kwamba Iran haijaashiria ama kuomba kusitisha mapigano. Mgogoro huu lazima uishe kwa sharti kwamba hautarudiwa kamwe. Tunaposema hatutaki kusitisha mapigano si kwa sababu tunataka kuendelea na vita. Ni kwa sababu vita hivi ni lazima viishe kwa njia ambayo maadui hawatafikiria kurudia mashambulizi. Ninaamini wamejifunza somo kubwa na kutambua aina ya nchi wanayokabiliana nayo -- nchi ambayo haitasita kulinda usalama wake na iko tayari kuendelea na vita kwa gharama yoyote," alisema Araghchi.

Katika hatua nyingine, Araghchi amesema hajafanya mawasiliano yoyote ya moja kwa moja na mjumbe maalumu wa Marekani Steve Witkoff, kauli Kauli inayotofautiana na taarifa za awali za vyombo vya habari kwamba kumekuwepo na mawasiliano baina yao katika siku za karibuni.

Araghchi, amesema kupitia mtandao wa X kwamba, mara ya mwisho aliwasiliana na Witkoff kabla Rais Donald Trump hajaamua kukatisha mchakato wa kidiplomasia na kuanzisha operesheni nyingine haramu ya kijeshi.

Jeshi la Marekani limesema jana kwamba wanajeshi wake waliojeruhiwa kwenye vita hivyo hadi sasa imefikia 200. Kwenye taarifa yake, Kamandi Kuu ya jeshi imesema wengi wao wamepata majeraha madogomadogo na wanajeshi 180 tayari wamerejea kwenye majukumu yao. Wanajeshi 13 wameuawa.