Safari za ndege Dubai zarejea baada ya shambulio la droni
16 Machi 2026
Tukio la kuwaka moto kwa tanki la mafuta, ambalo halikusababisha majeruhi, ni shambulizi la tatu kulenga uwanja wa ndege wa Dubai tangu Iran ilipoanzisha mashambulizi ya kisasi dhidi ya mataifa ya Ghuba tarehe 28 Februari. Iran inasema mashambulizi hayo yanalenga uwepo wa Marekani katika kanda hiyo.
Aidha, shambulizi jingine la droni limeripotiwa kulenga miundombinu ya mafuta katika pwani ya mashariki ya Umoja wa Falme za Kiarabu. Kwa mujibu wa mamlaka za nchi hiyo, shambulizi hilo lilitokea katika eneo la uzalishaji wa mafuta la Fujairah na kusababisha moto mkubwa, huku juhudi za kuudhibiti zikiendelea.
Eneo hilo liko katika pwani ya UAE kwenye Ghuba ya Oman, nje ya Mlango Bahari wa Hormuz, ambao kimsingi umefungwa na Iran. Saudi Arabia pia imesema imezuia wimbi la droni za Iran zipatazo 35 zilizorushwa kuelekea mkoa wake wa mashariki wenye visima vikubwa vya mafuta.
Israel nayo imeripoti kuwa Iran imefyatua makombora kuelekea nchini humo. Kwa mujibu wa jeshi la Israel, Iran inatumia pia mabomu ya kutawanya vilipuzi vidogo vidogo katika maeneo mbalimbali, ambayo yanaweza kukwepa baadhi ya mifumo ya ulinzi wa anga.
Mashambulizi Tehran na Beirut
Wakati huo huo, Iran yenyewe imelengwa kwa mashambulizi ya anga, ambapo jengo moja la shule katika mji wa Khomeyn, katikati mwa nchi hiyo, limeharibiwa. Shirika la habari la Iran, Mehr, limemnukuu gavana wa mkoa wa Markazi akisema kuwa hakukuwa na vifo, ingawa nyumba kadhaa zilizo karibu ziliripotiwa kuharibiwa. Picha zilizosambazwa na vyombo vya habari vya Iran zilionyesha jengo kuu la shule ya sekondari likiwa limeharibiwa vibaya. Hata hivyo, haikubainika mara moja ni jeshi gani lililohusika na shambulizi hilo.
Milipuko mikubwa pia imesikika mjini Beirut alfajiri ya leo, wakati Israel ilipoufanyia mashambulizi mji huo mkuu wa Lebanon ikisema inalenga miundombinu inayohusishwa na kundi la wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran.
Jeshi la Israel limetoa amri ya kuondolewa kwa wakazi katika maeneo kadhaa ya Beirut na kusini mwa Lebanon. Katika taarifa yake, jeshi hilo limesema limeanza kile lilichokiita "operesheni ndogo za ardhini” dhidi ya Hezbollah katika kusini mwa Lebanon.
Hadi sasa, zaidi ya watu 800,000 wameripotiwa kupoteza makazi yao kutokana na kampeni ya kijeshi ya Israel nchini humo, huku takribani watu 850 wakiuawa, wakiwemo watoto 107 na wanawake 66.
Katika hatua nyingine, jeshi la Israel limesema limeharibu ndege iliyodaiwa kuwa ikitumiwa na aliyekuwa kiongozi mkuu wa Iran, marehemu Ali Khamenei, katika uwanja wa ndege wa Mehrabad mjini Tehran usiku wa kuamkia leo. Kwa mujibu wa jeshi hilo, ndege hiyo ilikuwa ikitumiwa na maafisa waandamizi wa Iran na viongozi wa kijeshi kwa safari za ndani na nje ya nchi pamoja na kuratibu shughuli na mataifa washirika.