1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya Iran yatikisa nchi za Ghuba

9 Machi 2026

Mji mkuu wa Qatar Doha, umeshuhudia miripuko kadhaa ya makombora kutoka Iran ambayo imeendelea na kampeini yake ya kulipiza kushambuliwa na Marekani na Israel.

https://p.dw.com/p/5A4LA
Makombora yakionekana kulipuka kwenye mji mkuu wa Qatar Doha
Makombora yakionekana kulipuka kwenye mji mkuu wa Qatar DohaPicha: Mahmud Hams/AFP

Miripuko kadhaa imesikika hivi leo katika maeneo mbali mbali ya mji mkuu wa Qatar Doha wakati pia ving'ora vikilia katika mji wa Manama, taarifa hiyo ni kwa mujibu wa waandishi habari wa shirika la AFP.

Iran imeendelea na kampeini yake ya mashambulizi ya anga dhidi ya mataifa majirani zake katika Ukanda wa Ghuba.

Jeshi la Israel ambalo pamoja na Marekani wamekuwa wakiishambulia Iran, limesema limeanzisha operesheni nyingine kubwa zaidi ya kuishambulia miji ya Tehran, Isfahan na Kusini mwa Iran.Mashambulizi makubwa ya Israel yatikisa Tehran

Ripoti pia zinaarifu kwamba wizara ya ulinzi ya Uturuki imesema kombora la masafa marefu lililofyetuliwa kutoka Iran lilizuiwa na mfumo wa ulinzi wa NATO, likiwa ni tukio la pili ndani ya siku tano,la kuilenga Uturuki. Kombora hilo lililenga eneo la Gaziantep kwa mujibu wa Uturuki.

Marekani  imewashauri raia wake wasiokuwa na majukumu ya lazima waondoke Kusini mwa Uturuki na kwenye ubalozi wake mdogo karibu na mji wa Adana ambako kuna kambi kubwa ya NATO.