Umoja wa Ulaya, China kufanya mkutano wa kilele | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Mkutano wa kilele kati ya China na Umoja wa Ulaya

Umoja wa Ulaya, China kufanya mkutano wa kilele

Ulaya yafanya mazungumzo na China, ikitafuta kujiweka kati ya Marekani na China, kulinda maslahi yake ya kibiashara, huku pia ikisimamia maadili ya demokrasia na ya haki za binadamu

Mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na China unafanyika leo kwa njia ya video, ukifupishwa na kuwa wa siku moja kutoka tatu ilizopangiwa awali. Katika mkutano hao viongozi wa Ulaya wanakabiliwa na mtihani wa kuweka wizani kati ya maslahi ya biashara kusimamia maadili ya haki za binadamu. 

Soma zaidi: Mkutano wa kilele wa EU-China: Nini hasa kilichotokea?

Kabla ya mripuko wa virusi vya corona, mkutano huu wa kilele ulitarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 13 hadi 15 Septemba mjini Leipzig mashariki mwa Ujerumani, ambako, kwa mara ya kwanza rais Xi Jinping wa China angezungumza ana kwa ana na viongozi wote wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya, na ungeonyesha nguvu za kansela wa Ujerumani Angela Merkel, katika wadhifa wake kama rais wa Umoja wa Ulaya wakati huu.

Mkutano uliofupishwa, uaminifu uliochujuka

Lakini sasa mkutano huo unafanyika kwa njia ya video, tena kwa siku moja tu. Kansela Merkel ataungana na rais wa baraza la Ulaya Charles Michel na rais wa Halmashauri ya Ulaya Ursula von der Leyen, na upande mwingine utakuwa na rais Xi Jinping akiwaongoza maafisa wa China.

Deutschland Merkel PK Navalny

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye pia ni rais wa zamu wa Umoja wa Ulaya

Ilipouahirisha mkutano huo mwezi Juni, Ujerumani ilisema sababu ilikuwa ni mripuko wa virusi vya corona, lakini kuahirishwa huko kulikidhi malengo ya kisiasa, kwa sababu hadhi ya China imeporomoka siku za hivi karibuni, kama anavyoeleza Lucrezia Poggeti, mtaalamu wa mahusiano kati ya Ula ya na China kutoka kikundi cha wataalamu cha Merics cha mjini Berlin, katika mahojiano na DW.

''Sifa ya China imepata pigo mnamo miezi michache iliyopita kuhusiana na mienendo yake kisiwani Hong Kong, na jinsi ilivyolishughulikia janga la corona kwa njia ambazo wengi wanaamini hazikuwa na uwazi.'' amesema Poggeti na kuongeza kuwa  China pia inashutumiwa kuendesha kampeni ya aibu katika namna ilivyochukulia bidhaa za kujilinda dhidi ya corona ilizoziuza Ulaya, ikitaka zionekane kana kwamba ilikuwa ikitoa msaada.

Mtazamo uliobadilika

China Präsident Xi Jinping

Rais wa China, Xi Jinping

Ulaya inaingia katika mkutano huo ikiwa na mtazamo uliobadilika juu ya China. Umoja wa Ulaya hauitazami tu China kama mshirika katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi na mshirika wa kiuchumi, bali pia kama mshindani anayetaka kuleta mwelekeo mpya kimaadili. Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema siku za nyuma Ulaya ilibweteka kuhusu China, lakini sasa imefunguka macho.

Soma zaidi: Merkel ahimiza umoja katika kupambana na korona 

Mkutano huu pia unafanyika wakati China ikikabiliwa na mbinyo mkali kutoka Marekani, siku chache tu baada ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo katika mataifa kadhaa ya Ulaya ya kati na kusini, iliyotazamwa kama ya juhudi za kuitenga China.

Katika mazungumzo yake ya umoja wa Ulaya, bila shaka China itakuwa ikijaribu kuzuia kujengeka kwa mshikamano wa Ulaya na Marekani dhidi yake, ikiwa na kumbukumbu mpya juu ya makubaliano aliyoyapata Pompeo wakati wa ziara yake, ya kuizuia kampuni ya China ya Huawei katika mipango ya ujenzi wa mtandao wa kizazi kipya wa G5.

 

6 DW-eigen