1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa kuamua juu ya uchunguzi Ukraine

Grace Kabogo
12 Mei 2022

Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kuamua kama lianzishe uchunguzi kuhusu madai ya ukiukaji uliofanywa na vikosi vya Urusi kwenye eneo la mji wa Kiev ambalo Ukraine imesema ni uhalifu wa kivita.

https://p.dw.com/p/4BDLy
Moldawien Besuch des UN-Generalsekretärs Antonio Guterres
Picha: Bogdan Tudor/AFP

Azimio lililowasilishwa na Ukraine na kuungwa mkono na zaidi ya nchi 50 litaiamuru tume iliyoundwa hivi karibuni ya kuchunguza matukio kwenye mikoa karibu na Kiev ambayo ilishikiliwa kwa muda na vikosi vya Urusi.

Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Emine Dzhaparova amesema uhalifu uliofanywa na Urusi dhidi ya raia kwenye maeneo hayo ni pamoja na utesaji, unyanyasaji wa kingono na kijinsia. Amesema miji mingi imeharibiwa kabisa na watu hawawezi tena kuishi.

"Maeneo ya mikoa ya Kiev, Chernihiv, Sumy, Kharkiv, ambayo yanadhibitiwa na Urusi tangu mwishoni mwa mwezi Februari na Machi, yameshuhudia ukiukaji wa kutisha wa haki za binaadamu kwenye bara la Ulaya katika miongo kadhaa," alifafanua Dzhaparova.

Msemaji wa ujumbe wa Urusi katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva, hakuzungumzia mara moja kuhusu uwezakano wa uchunguzi wa uhalifu wa kivita.

Urusi imekanusha kuwalenga raia na imeuita uvamizi wake Ukraine tangu Februari 24, kama "operesheni maalum ya kijeshi" kuipokonya silaha Ukraine katika kile ambacho Urusi imekiita chuki dhidi ya Urusi inayochochewa na nchi za Magharibi.

Katibu Mkuu wa NATO aipongeza Finland kwa kutaka kujiunga na jumuiya hiyo

Belgien | NATO Generalsekretär Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens StoltenbergPicha: John Thys/AFP/Getty Images

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg amepongeza uamuzi wa viongozi wa Finland kuunga mkono nchi hiyo kujiunga na jumuia hiyo, akisema mchakato wa kuwa mwanachama utakuwa rahisi na usio na vipingamizi.

Hata hivyo, Urusi imeonya kuwa nia ya Finland kujiunga na NATO ni kitisho kwa usalama wa nchi hiyo na italazimika kuchukua hatua za kijeshi kujibu uamuzi huo. Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov, amewaambia waandishi habari kwamba kutanuka kwa NATO na kuelekea kwenye mipaka yake, haitoifanya dunia na bara hilo kuwa na utulivu na usalama.

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz ameahidi uungaji mkono kamili wa serikali ya Ujerumani katika juhudi za Finland kujiunga na NATO.

Ama kwa upande mwingine, Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imesema leo kuwa itafanya kazi na serikali za umoja huo kuisaidia Ukraine kuuza mamilioni ya tani ya nafaka ambazo zimekwama nchini humo kutokana na jeshi la wanamaji la Urusi kuzuia bandari za Ukraine. Ukraine ilikuwa nchi ya nne kwa kuuza nafaka duniani mwaka 2020 hadi 2021.

Huku hayo yakijiri, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7 wanakutana mjini Hamburg, Ujerumani kujadiliana kuhusu vita vya Ukraine, nishati na usalama wa chakula. Mwenyeji wa mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, hivi karibuni alirejea kutoka Kiev.