Ulaya yataka majibu madai ya udukuzi wa Marekani na Denmark | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.06.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ulaya yataka majibu madai ya udukuzi wa Marekani na Denmark

Mataifa kadhaa ya Ulaya yametaka kupatiwa majibu kufuatia ripoti kuwa Marekani iliwapeleleza viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hizo washirika kwa kutumia miundombinu ya mawasiliano ya Denmark kati ya mwaka 2012 hadi 2014.

Deutschland Frankreich PK Ministerrat | Merkel und Macron

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa wamesema kwa pamoja kuwa kuendesha ujasusi miongoni mwa mataifa washirika ni jambo lisilokubalika na kuwa wanataraji kupata ufafanuzi kutoka Washington na Copenhagen.

Matamshi hayo ya kutaka majibu yanafuatia ripoti ya uchunguzi iliyorushwa siku ya Jumapili na vyombo vya habari barani Ulaya ambayo imefichua kuwa taasisi ya usalama wa taifa ya Marekani NSA ilitumia mifumo ya mawasiliano ya Denmark kuwapeleleza wanasiasa wa ngazi ya juu nchini Ufaransa, Ujerumani, Norway na Sweden.

Inaarifiwa kuwa NSA ilifanikiwa kudukua mawasiliano ya ujumbe mfupi, mazungumzo ya simu na hata matumizi ya intaneti ikiwemo ya kansela Angela Merkel wa Ujerumani na viongozi wengine wakuu wa serikali.

Rais Macron ambaye jana alifanya mkutano kwa njia ya video na Kansela Merkel amesema hakuna nafasi kwa washirika wa Ulaya na Marekani kutiliana mashaka na ndiyo maana ni muhimu kwa Washington kufafanua kile kilichotokea.

"Hili halikubaliki miongoni mwa washirika na kwa hakika halikubaliki kabisa baina ya washirika wa Ulaya. Ninaongozwa na msingi wa kuaminiana ambao unatuunganisha watu wa Ulaya na Marekani, kwa namna hiyo tunafanya kila kitu kwa usalama wa pamoja na hakuna nafasi ya kutiliana wasiwasi baina yetu." amesema Macron.

Je, Denmark ilifahamu matendo hayo ya Marekani? 

USA Fort Meade | Zentrale der National Security Agency (NSA)

Taasisi ya NSA ndiyo inatajwa kuongoza shughuli hizo za upepelezi

Kwa upande wake kansela Merkel amesema anaunga mkono mtazamo huo wa rais Macron na kwamba ametiwa moyo na hakikisho lililotolewa na waziri wa ulinzi wa Denmark Trine Bramsen kuwa analaani matendo yote ya washirika kufanyiana ujasusi na upelelezi.

Bramsen ambaye aliteuliwa kuongoza wizara hiyo ya ulinzi mwaka 2019 badohajathibitisha au kukanusha ripoti hiyo inayoihusisha Denmark na upepelezi lakini amekaririwa akisema vitendo hivyo havikubaliki.

Mbali ya Ujerumani na Ufaransa mataifa jirani na Denmark pia yametaka ufafanuzi.

Waziri Mkuu wa Norway Erna Solberg amelaani tabia ya mataifa rafiki kufanyiana upepelezi na kuitaka serikali mjini Copenhagen kuweka wazi taarifa zote ilizonazo za madai yaliyofichuliwa.

Sweden pia imetaka kupatiwa majibu 

Symbolbild Spionage Affäre

Mara kadhaa Marekani imenyooshewa kidole kwa kuwapeleleza washirika wake

Sweden nayo imesema inafanya mawasiliano ya karibu na Denmark ikinuwaia kuuliza iwapo miundombinu ya nchi Denmark imekuwa ikitumika kuwafuatilia wanasiasa wa Sweden.

Hata hivyo hadi sasa haijawa wazi iwapo Denmark ilifahamu kuwa Marekani ilikuwa ikitumia miundombinu yake ya mawasiliano ya chini ya bahari kuyapeleleza mataifa jirani.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani na Taasisi ya NSA zote bado hazijatoa maelezo kuhusiana na madai hayo.

Hii haitokuwa mara ya kwanza kwa Marekani kutuhumiwa kuwapeleleza viongozi na wanasiasa wa Ulaya na maeneo mengine duniani.

Iwapo madai haya ya sasa yatathibitishwa itakuwa ni dhahiri kuwa kwa Washington kila mtu au taifa ni mlengwa wa operesheni zake za kijasusi na udukuzi.