1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaitaka NATO kuipatia silaha zaidi

Grace Kabogo
7 Aprili 2022

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba ameitolea wito Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuipatia nchi yake silaha sasa kabla ya kuchelewa zaidi.

https://p.dw.com/p/49cME
Ukraine-Krieg Dorf Borodyanka | Zerstörungen
Picha: Kostiantyn Honcharov/DW

Kuleba ameonya kuwa mapambano katika eneo la Donbas yanakumbushia operesheni kubwa za kijeshi za maelfu ya vifaru, ndege na magari ya kivita wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kauli hiyo ameitoa Alhamisi huku akiwataka washirika wake wa NATO kuisaidia zaidi Ukraine kwa silaha ndani ya siku chache zijazo.

"Aidha mtusaidie sasa, na ninazungumza kuhusu siku na sio wiki. Au msaada wenu utakuwa umechelewa sana, watu wengi zaidi watakufa, raia wengi watapoteza makaazi yao, vijiji vingi vitaharibiwa. Kwa sababu msaada huu ulichelewa kutolewa," alisisitiza Kuleba.

Takriban raia 160,000 wamekwama kwenye mji wa Mariupol bila ya umeme, huku wakiwa na chakula na maji kidogo. Meya wa mji wa Mariupol amesema hadi sasa idadi ya watu waliouawa katika mji huo imefikia 5,000. Kwa mujibu wa meya huyo, wakaazi 40,000 wamepelekwa Urusi kwa lazima, na sasa wamepokelewa kama wakimbizi.

Ukraine Menschen fliehen aus Mariupol
Wakaazi wa Mariupol wakiondoka kwenye mji huo uliozingirwaPicha: Maksim Blinov/SNA/IMAGO

Kundi la mataifa saba yaliyoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7 Alhamisi limetoa wito wa Urusi kusimamishwa uachama katika Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa kutokana na vitendo vyake viovu na ukatili nchini Ukraine. Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi hizo za Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani wamesema wana uhakika sasa ni wakati wa Urusi kusimamishwa uanachama.

Baadae Alhamisi Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linatarajia kupiga kura iwapo iisimamishe Urusi uanachama katika Baraza la Haki za Binaadamu kutokana na madai kwamba wanajeshi wa Urusi waliwaua raia wakati wakiondoka kwenye mji wa Bucha, ulio karibu na Kiev.

Zelensky ataka Urusi ifukuzwe Umoja wa Mataifa

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky pia ametoa wito wa Urusi kufukuzwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ili isiweze kuzuia maamuzi kuhusu uchokozi wake na vita vyake yenyewe.

Mkuu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa, Martin Griffiths amesema wapelelezi watachunguza mauaji ya raia yaliyogundulika baada ya wanajeshi wa Urusi kuondoka kwenye mji wa Bucha. Akiwa ziarani mjini Bucha, nje kidogo ya mji mkuu, Kiev, Griffiths amesema kwamba ulimwengu tayari umeshtushwa na mauaji hayo na kwamba hatua inayofuata ni kufanya uchunguzi.

Türkei Gespräche zwischen Russland und der Ukraine in Istanbul
Wajumbe wa Urusi na Ukraine katika mazungumzo ya amani Istanbul, UturukiPicha: Sergei Karpukhin/TASS/dpa/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje ya Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema mauaji ya Bucha yanafunika mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine. Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema Ukraine imeipatia nchi yake rasimu ya makubaliano ya amani ambayo ina vipengele visivyokubalika, ambavyo vinakiuka pendekezo la awali.

Urusi: Ukraine haina nia kumaliza mapigano

Lavrov amesema Ukraine haina nia ya kumaliza mapigano. Cavusoglu amesisitiza Alhamisi kuwa mazungumzo yataendelea na kwamba Urusi na Ukraine zinaonekana ziko tayari kwa duru mpya ya mazungumzo yatakayofanyika Uturuki.

Ikulu ya Urusi imesema itafanya uamuzi kuangalia iwapo Rais Vladmir Putin atahudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa kundi la nchi zilizostawi na zinazoinukia kiuchumi za G20, utakaofanyika baadae mwaka huu nchini Indonesia, kutegemeana na mambo yatakavyobadilika.

Msemaji wa ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov alikuwa akijibu swali kuhusu wito wa baadhi ya viongozi wa nchi za G20 kumtenga Putin katika mkutano huo kutokana na uamuzi wake wa kupeleka maelfu ya wanajeshi Ukraine. Peskov pia amevikosoa vikwazo vipya vya Marekani ilivyoweka dhidi ya watoto wa Putin. Akizungumza Alhamisi, Peskov amesema hilo ni jambo gumu kulielewa na kulielezea.

(AFP, DPA, AP, Reuters)