1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yapata taarifa binafsi za IS

10 Machi 2016

Polisi wa jinai Ujerumani wamesema wamefanikiwa kuyapata mafaili yenye taarifa binafsi za wapiganaji wa kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu - IS na wanaamini kuwa taarifa hizo ni za kweli

https://p.dw.com/p/1IAZI
Picha: picture-alliance/dpa

Tangazo hilo limetolewa leo baada ya kituo cha televisheni cha Uingereza, Sky News kuripoti kuwa kimepata mafaili 22,000 ya kundi la Dola la Kiislamu-IS katika mpaka wa Uturuki na Syria. Mafaili hayo yana majina ya ukweli ya wapiganaji wa IS, maeneo wanakotokea, namba zao za simu na hata majina ya watu wanaowafadhili na kutoa mafunzo kwa wanamgambo hao.

Gazeti la Ujerumani la Sueddeutsche Zeitung, limeripoti pia limepata mafaili kadhaa kama hayo katika mpaka wa Uturuki na Syria, ambapo limesema mafaili ya IS na picha za video zilipatikana kwa wingi kutoka kwa wapiganaji wa Kikurdi wanaopingana na IS na pia wapiganaji wa IS wenyewe.

Msemaji wa shirika la jinai la Ujerumani, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amesema shirika lake kwa sasa linayatathmnini mafaili hayo. Hata hivyo, amekataa kusema ni wapi shirika hilo limeyapata mafaili hayo, kuna nyaraka ngapi na imeyapata mafaili hayo tangu lini.

Nyaraka hizo zitasaidia kuwafatilia washirika wa IS

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere ameliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA kwamba nyaraka hizo zitawapa maafisa nafasi nzuri ya kuwafatilia na kuwashtaki watu wanaoshirikiana na IS.

Kwa mujibu wa kituo cha Sky News, nyaraka hizo ziko katika aina ya fomu zilizojazwa na wapiganaji walioandikishwa wakati wanajiunga na IS. Fomu hizo zina maswali 23 na zinawahusisha watu kutoka kiasi ya mataifa 51.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de MaizierePicha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Wakati huo huo, imeripotiwa kuwa kamanda wa kundi la Dola la Kiislamu, Abu Omar Al-Shishani amejeruhiwa katika shambulizi la anga la hivi karibuni lililofanywa na Marekani nchini Syria.

Shirika linalofatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake Uingereza, limesema duru zimeeleza kwamba shambulizi la anga la Machi 4 lililokuwa linaulenga msafara wa Shishani, liliwaua walinzi wake na yeye mwenyewe alijeruhiwa vibaya. Wizara ya ulinzi ya Marekani ilisema kamanda huyo aliuawa katika shambulizi hilo.

Ama kwa upande mwingine Marekani na washirika wake wamefanya mashambulizi 20 ya anga dhidi ya IS nchini Iraq na Syria hapo jana. Taarifa iliyotolwa leo na jeshi la muungano imeeleza kuwa mashambulizi 15 yamefanyika Iraq katika miji ya Ramadi na Sinjar na matano yameshambulia karibu miji mitatu ya Syria.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP,RTR
Mhariri:Josephat Charo