1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kusitisha kuidhinisha mauzo ya silaha kwa Uturuki

Sekione Kitojo
13 Oktoba 2019

Ujerumani haitaidhinisha tena mauzo ya silaha  ambazo zinaweza kutumika katika mashambulizi ya kijeshi ya Uturuki kaskazini mwa Syria, waziri wa mambo ya kigeni Heiko Maas ameliambia gazeti la Bild am Sonntag.

https://p.dw.com/p/3RCKI
Syrien Militäroffensive der Türkei im Norden
Picha: picture-alliance/Photoshot

"Kutokana  na mashambulizi  ya  kijeshi  ya  Uturuki kaskazini mashariki  mwa Syria , serikali  ya shirikisho haitatoa  tena vibali vipya  kwa  ajili  ya  vifaa  vya  kijeshi  ambavyo vinaweza  kutumika na  Uturuki nchini  Syria," Maas  amesema.

Maas  aliongeza kwamba  serikali  ya  Ujerumani  tayari imeweka vizuwizi katika  mauzo ya  nje ya  silaha  zake  kwa  Uturuki katika mwaka  2016 kutokana  na  mashambulizi  ya  nchi  hiyo katika  jimbo la  Afrin.

Türkische Militäroffensive in Nordsyrien | Luftangriff in Ras al-Ain
Moshi ukifuka kutokana na mashambulizi ya Uturuki ndani ya ardhi ya SyriaPicha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Washirika  wa  mataifa  ya  magharibi wamekosoa operesheni  ya Uturuki ndani  ya  Syria, ambayo  ilianza siku  ya  Jumatano , ikisema inatishia  mzozo  mkubwa  wa  kibinadamu pamoja  na  kufufua  kundi la itikadi  kali la  Kiislamu  linalojiita  Dola  la  Kiislamu  katika  eneo hilo.

Siku  ya  Jumamosi , wizara ya  mambo  ya  nje  na  ulinzi mjini  Paris zilisema  kuwa  Ufaransa  inasitisha  mauzo  yake  ya  silaha  kwa Uturuki  kutokana  na  mashambulizi  ya  Uturuki kaskazini  mwa Syria.

Serikali  mjini  Paris imeamua  kusitisha  mipango  yote ya  mauzo ya  silaha  kwa  Uturuki  ambayo  inaweza  kutumiwa  katika mashambulizi, wizara  hizo zilisema  katika  taarifa  ya  pamoja.

Militäroffensive der Türkei in Nordsyrien
Majeshi ya Uturuki yakitayarisha vifaa kabla ya kuingia kaskazini mwa SyriaPicha: Getty Images/B. Kara

Siku  ya  Ijumaa , Uholanzi ilisema  imesitisha  kwa  muda mauzo yake  ya  silaha  kwa  Uturuki, na  Sweden  ikasema itatafuta kuungwa  mkono kwa  ajili  ya  kuwekewa  vikwazo  vya  Silaha Uturuki  na  mataifa  yote  ya  Umoja  wa  Ulaya katika  mkutano  wa mawaziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Umoja  huo wiki  ijayo.

Mauzo ya silaha kwa Uturuki

Wanasiasa mashuhuri wa mrengo  wa  kushoto  nchini  Ujerumani wamekuwa  wakitoa  mwisho wa  kupigwa  marufuku  kabisa mauzo ya  silaha nchini  Uturuki.

Deutschland Proteste in Köln gegen der türkischen Militäroffensive in Nordsyrien
Mmoja kati ya waandamanaji mjini Kolon Ujerumani akipunga bendera katika kupinga operesheni ya Uturuki dhidi ya Wakurdi nchini SyriaPicha: Reuters/T. Schmuelgen

Siku  ya  Jumamosi , maelfu ya  watu  walishiriki  maandamano katika  miji nchini  Ujerumani kupinga  mashambulizi  ya  kijeshi  ya Uturuki. Mjini  Kolon , zaidi ya watu 10,000, wengi  wao  wakiwa Wakurdi , wanakadiriwa  kujiunga  na  maandamano  hayo.

Kiasi  ya  waandamanaji 4,000 waliingia  mitaani  mjini  Frankfurt, wakati  waandamanaji 3,000 katika  kila  mmoja  ya  miji  ya Hamburg  na  Hannover walishiriki maandamano.

Maandamano  zaidi  yaliripotiwa  mjini  Bremen, Berlin na Saarbrueken.

Maandamano  pia  yaliripotiwa  katika  miji  ya  Ufaransa. Maandamano  makubwa  kabisa  yalikuwa  katika  mji  mkuu  Paris, ambako  watayarishaji  wameliambia  shirika  la  habari  la  Ufaransa AFP kuwa  watu 20,000 walijitokeza.

Frankreich Proteste in Paris gegen der türkischen Militäroffensive in Nordsyrien
Maandamano ya kupinga operesheni ya jeshi la Uturuki dhidi ya Wakurdi wa SyriaPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Mori

Baada  ya  tangazo  la  Maas , Katrin Goering-Erkardt  wa  chama cha   walinzi  wa  mazingira The Green, alisema ; "Marufuku  ya serikali  ya  Ujerumani ya  mauzo  ya  silaha ni  hatua  ya  kwanza iliyochelewa  mno. Hata hivyo, haipaswi  tu  kutekelezwa kwa  ajili ya  mauzo  ya  baadaye lakini  pia kwa  mauazo  ambayo  tayari yamekwisha  idhinishwa."

Ujerumani imejizuwia  kusitisha  kabisa  mauazo  ya  silaha  kwa Uturuki katika  mashambulizi  ya  hapo zamani  ya Uturuki  nchini Syria.