1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kumchagua rais mwanamke kumrithi Steinmeier?

5 Machi 2026

Mjadala umeibuka nchini Ujerumani kuhusu nani anapaswa kumrithi rais Frank Walter Steinmeier mwaka ujao. Suali kubwa linalozusha mjadala ni ikiwa sasa ni wakati wa kuongozwa na rais mwanamke?

https://p.dw.com/p/59paO
Rais Frank-Walter Steinmeier akimtunuku Tuzo kansela wa zamani Angela Merkel mwaka wa 2023
Ujerumani itapata mkuu mpya wa nchi mwaka wa 2027 kuchukua nafasi ya Frank-Walter SteinmeierPicha: John MacDougall/AFP/Getty Images

Rais wa sasa nchini Ujerumani ni Frank Walter Steinmeier ambaye muhula wake wa pili madarakani unamalizika mwanzoni mwa mwaka ujao, 2027. Chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Social Democratic SPD na wanamazingira wanapigia upatu mara hii nafasi hiyo irithiwe na mwanamke.

Ilse Aigner akiwapungia mkono wapiga picha wakati akiwasili kwenye Tamasha la Bayreuth 2025
Waziri wa zamani wa Kilimo chini ya Angela Merkel, Ilse Aigner ameongoza bunge la Bavaria kwa miaka minane.Picha: Karl-Josef Hildenbrand/picture alliance/dpa

Hatua hiyo itakuwa ni ya kihistoria hasa ikizingatiwa Ujerumani imekuwa na marais 12 wote wanaume tangu kumalizika vita vya pili vya dunia. Jina la kansela wa zamani Angela Merkellilipotajwa kuwa miongoni mwa wanapaswa kurithi nafasi hiyo, mjadala mkubwa umezuka,suala hilo likigonga vichwa vya habari. Chama cha kijani kimependekeza jina la Kansela huyo wa zamani kugombea.

Merkel aliiongoza Ujerumani kwa miaka 16  mpaka mwaka 2021 na alikuwa kiongozi aliyepata umaarufu mkubwa katika kipindi chote cha utawala wake. Hata hivyo Merkel amepuuza mara moja atiati zinazosambaa kuhusu kumrithi Steinmeir akiziita tetesi hiyo kuwa hazina maana.

Wanaofuatilia masuala ya kisiasa wanasema kwamba pendekezo hilo huenda pia lisifanikiwe kwasababu ya uhasama wa muda mrefu kati ya Merkel na kansela wa sasa Friedrich Merz.

Rais wa Bunge la Ujerumani Julia Klöckner
Waziri wa zamani wa Kilimo na Rais wa sasa wa Bundestag Julia Klöckner anaonekana kama mtu mwenye mgawanyikoPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Hivi karibuni Merz alikiambia kituo cha Televisheni cha Phoenix kwamba pendekezo lake kuhusu nani arithi kiti cha rais Steinmeir atalitangaza mwezi Septemba.

Kiongozi huyo wa Ujerumani kutokana chama cha CDU amesema anataka kumchagua mtu atakayekuwa mwakilishi wa nchi kwa ujumla wake, lakini hakutaja ikiwa mtu anayemfikiria ni mwanamke au mwanamme.

Ikumbukwe kwamba chaguzi za mwisho mwaka huu za majimbo matano zitafanyika mwezi Septemba  na hapo ndipo itakapobainika mwelekeo hasa wa kisiasa kitaifa.

Karin Prien akiwa katika kikao na waandishi wa habari mjini Berlin
Karin Prien kwa sasa anahudumu kama Waziri wa Elimu, Masuala ya Familia, Wazee, Wanawake na Vijana wa Shirikisho.Picha: dts Nachrichtenagentur/IMAGO

Kimsingi rais wa Ujerumani hachaguliwi na wananchi moja kwa moja, baraza kuu la bunge ndilo linalowajibika kupiga kura ya siri  kumchagua rais anayekaa kwa muhula wa miaka mitano na kisha kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili wa mwisho.

Baraza hilo linajumuisha wabunge 630 wa mabaraza yote sambamba na wawakilishi wa majimbo yote 16 ya Ujerumani na wawakilishi hao wanaweza kuwa wanasiasa lakini pia hata raia wenye umaarufu kwenye jamii kama wanariadha au wasanii.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW