1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel apinga uvumi wa kugombea urais Ujerumani

12 Februari 2026

Ofisi ya aliyekuwa Kansela Angela Merkel imekanusha taarifa kwamba huenda akawa miongoni mwa wanaowania kuwa rais ajaye wa Ujerumani. Vyama vya siasa vinatafakari nani anaweza kumrithi Rais Steinmeier mwaka ujao.

https://p.dw.com/p/58c68
Angela Merkel
Merkel kwa kiasi kikubwa amejiondoa katika siasa za kila siku na ameepuka kuwa kama ‘kansela kivuli’.Picha: John MacDougall/picture-alliance/AP

Aliyekuwa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amekanusha uwezekano wowote wa kuwania urais wa shirikisho la Ujerumani, ofisi yake ilisema Alhamisi, ikitupilia mbali uvumi kwamba angeweza kuteuliwa kwa wadhifa huo.

Kauli hiyo imekuja wakati vyama vya siasa vimeanza kupima majina ya wagombea watakaoweza kumrithi rais wa sasa, Frank-Walter Steinmeier, katika uchaguzi wa mwaka ujao.

Ofisi ya Merkel ilisema nini?

"Huo ni upuuzi,” msemaji wa ofisi ya kansela huyo wa zamani alisema akijibu swali kutoka gazeti la Der Tagesspiegel.

Katika majibu tofauti kwa shirika la habari la Ujerumani Deutsche Presse-Agentur (dpa), msemaji huyo alijibu "hapana” alipoulizwa moja kwa moja kama Merkel yuko tayari kugombea.

Ingawa kumekuwa na wito wa mara kwa mara wa mwanamke kuwa mkuu wa nchi ya Ujerumani, hadi sasa hakuna kansela wa zamani aliyewahi kuwa rais baada ya kuondoka madarakani.

Tangu aondoke ofisini, Merkel amekuwa akijishughulisha zaidi na maisha binafsi, kushiriki mara chache katika hafla za umma, pamoja na miradi mikubwa ikiwemo kuandika tawasifu yake, "Freiheit” (Uhuru). Kwa kiasi kikubwa amejitenga na siasa za kila siku na hatoi maoni mara kwa mara kuhusu maamuzi ya serikali au migogoro ya vyama.

Ujerumani Berlin 2025 | Frank-Walter Steinmeier | Rais wa Shirikisho
Muhula wa rais wa sasa Frank-Walter Steinmeier unamalizika Machi mwakani.Picha: Felix Zahn/photothek.de/picture alliance

Kwa nini uvumi huo ulizuka?

Gazeti la Bild liliripoti kwamba kulikuwa na tetesi ndani ya chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union (CDU), ambacho Merkel aliwahi kukiongoza, kuwa chama cha Alliance 90/The Greens (chama cha watetezi wa mazingira) kingeweza kumpendekeza kwa wadhifa huo wa heshima.

Ripoti hiyo ilisema wazo hilo lilikuwa likijadiliwa kama sehemu ya mikakati mipana kuhusu nani atakuwa mkuu ajaye wa nchi. Ofisi ya Merkel ilitoa tamko baada ya taarifa hizo kusambaa zaidi kwenye vyombo vya habari.

Chama cha Kijani kilikanusha kuwa na mpango wowote wa kumpendekeza Merkel. Kiongozi mwenza wa wabunge wa chama hicho, Britta Hasselmann, aliliambia gazeti la Rheinische Post: "Hakuna ukweli wowote katika hilo.”

Aliongeza kuwa hadi sasa hakuna jambo lililojadiliwa au kuamuliwa ndani ya chama kuhusu uchaguzi wa rais wa shirikisho.

Merkel azua wasiwasi baada ya kuoneka akitetemeka

Rais wa Ujerumani huchaguliwaje?

Rais wa shirikisho huchaguliwa na Mkutano wa Shirikisho, unaojumuisha wabunge wote wa Bunge la Shirikisho (Bundestag) pamoja na idadi sawa ya wajumbe walioteuliwa na mabunge ya majimbo. Kazi pekee ya mkutano huo ni kumchagua rais.

Kwa kawaida wagombea hupendekezwa na chama kimoja au zaidi, na kwa ujumla hawafanyi kampeni. Mwanachama yeyote wa Mkutano wa Shirikisho pia anaweza kupendekeza jina la mgombea.

Wadhifa wa rais nchini Ujerumani kwa kiasi kikubwa ni wa heshima, lakini una mamlaka ya kimaadili na huikilisha nchi kimataifa.

Rais Steinmeier ataondoka madarakani muhula wake wa pili utakapomalizika Machi 18, 2027, na kwa mujibu wa katiba ya Ujerumani haruhusiwi kugombea tena.

Ndani ya muungano wa vyama vya kihafidhina, unaojumuisha pia chama cha Christian Social Union cha Bavaria (CSU), jina la Waziri wa Elimu, Karin Prien, pia limetajwa kama mmoja wa wanaoweza kuwania nafasi hiyo.