1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Steinmeier aungwa mkono na chama kikuu cha upinzani

Saleh Mwanamilongo
5 Januari 2022

Chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani cha CDU kimetangaza kumuunga mkono Rais Frank-Walter Steinmeier, kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.

https://p.dw.com/p/45BsQ
Deutschland | Bundespräsident Steinmeier Weihnachtsgrüße
Picha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

Vigogo wachache wa chama cha mrego wa kulia cha aliyekuwa Kansela Angela Merkel,Christian Democratic Union,CDU, walikuwa wakipendekeza kuteua mwanamke kugombea nafasi ya rais wa Ujerumani kwenye uchaguzi wa mwezi ujao. Ujerumani bado haijawa na rais mwanamke. Lakini matumaini ya mpinzani kuchaguliwa yametoweka kufuatia chama cha Kijani, moja ya vyama vitatu vinavyounda serikali ya mseto ya Kansela Olaf Scholz kuidhinisha muhula wa pili kwa Steinmeier.

Rais wa sasa, ambaye ni mwanachama mkongwe wa chama cha mrengo wa kushoto cha Kansela Scholz, SPD na alie na umri wa miaka 66 anaheshimiwa sana katika siasa za Ujerumani.

''Sauti inayowaleta watu pamoja''

Steinmeier alikuwa waziri wa mamabo ya nje wa Kansela Merkel
Steinmeier alikuwa waziri wa mamabo ya nje wa Kansela MerkelPicha: Hannibal Hanschke/Reuters/dpa/picture alliance/

Chama cha upinzani cha CDU na chama chake dada cha Bavaria, Christian Social Union,CSU,viliamua kumuunga mkono Steinmeier.  Armin Laschet kiongozi anayeondoka wa chama cha CDU amesema kwamba Ujerumani inahitaji mtu wa kuaminika na sauti inayowaleta watu pamoja na isiyowatenga wakati wa mvutano na mgawanyiko unaochochewa na janga la covid-19. Laschet alimsifu Steinmeir kwa kile alichoelezea kuwa ni uweledi wake mkubwa wa sera za kigeni.

Laschet amesema baada ya kupima hoja mbalimbali, waliamua katika awamu hii ambayo Ujerumani sasa inasimama kutoa msaada wao kwa rais ambaye yuko tayari kuendelea kutekeleza wajibu wake kwa nchi. Amesema anadhani lakini wakati utafika ambapo mwanamke atakuwa rais.

Kikao kitakachomchagua rais kinaundwa na wabunge wa Bundestag na idadi sawa ya wawakilishi wa majimbo yote 16 ya Ujerumani. Vyama katika serikali ya muungano ya Kansela Scholz vitakuwa na wingi wa kura, ingawa sio mkubwa. Uungwaji mkono wa vyama vya mrego wa kulia umeondoa hatari yoyote ya Steinmeier kukabiliwa na changamoto kubwa kwenye uhaguzi huo.

Mamlaka ya kimaadili

Mwezi Mei, Steinmeier alitangaza kuwa atawania muhula wa pili, miezi kadhaa kabla ya uchaguzi wa bunge ulioupa ushindi muungano wa hivi sasa wa Kansela Scholz. Kabla ya kuwa rais, Steinmeier alihudumu mara mbili kama waziri wa mambo ya nje wa Merkel. Hapo awali alikuwa kiongozi wa ofisi ya Kansela Gerhard Schroeder.

Rais wa Ujerumani ana mamlaka madogo wa kiutendaji, lakini anachukuliwa kama mtu mwenye mamlaka muhimu ya kimaadili.