1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atangaza kuanza vizuizi kwa bandari za Iran

14 Aprili 2026

Hali bado ni ya wasiwasi kwenye kanda ya Mashariki ya Kati hasa baada ya tangazo la Marekani kuwa limeanza operesheni ya kijeshi ya kiziwekea vizuizi bandari zote za Iran.

https://p.dw.com/p/5C7Ff
Marekani Washington D.C. 2026 | Rais Donald Trump wa Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: Mandel Ngan/AFP

Rais Donald Trump wa Marekani alisema operesheni hiyo inayojumuisha kuzikamata meli zinazosafirisha shehena ya mafuta ya Iran ilianza rasmi jana jioni na kuonya kupitia mtandao wake wa kijamii kwamba boti au meli yoyote ya kijeshi ya Iran itakayojaribu kuzisogelea meli za Marekani itashambuliwa.

Hata hivyo, hadi sasa maafisa wa jeshi la Marekani hawajatoa maelezo yoyote ya kina kuhusu namna operesheni hiyo itakavyotekelezwa.

Hilo linashuhudiwa wakati Iran imeapa kujibu mapigo kwakuhakikisha hakuna tone hata moja la mafuta linakalosafirishwa kupitia Mlango Bahari wa Hormuz kutoka bandari ya nchi za nchi nyingine za Ghuba.

Afisa mmoja wa Marekani amesema mbali ya Manuari moja ya kijeshi, Washington hivi sasa inazo pia meli kubwa 11 za kivita pamoja na nyingine 3 ndogo katika eneo zima la Mashariki ya Kati.

Lakini kulingana na afisa mwingine wa kijeshi wa nchi hiyo hakuna meli ya kivita ya Marekani iliyo karibu na ghuba ya Uajemi, eneo ambalo linajumuisha sehemu kubwa ya mwambao wa bahari wa Iran.

Marekani tayari imeziarifu kampuni za usafirishaji baharini kwamba imeweka vizuizi kwa meli kuingia na kutoka kwenye bandari za Iran lakini haiko wazi iwapo maelekezo hayo ndiyo yatasaidia utekelezaji wa kampeni yake ya kijeshi.

Tehran yahoji kuhusu msingi wa mzingiro wa Marekani 

Iran imesema kupitia wizara ya mambo ya kigeni kuwa marufuku na vizuizi vilivyotangazwa na Marekani vitakuwa na athari mbaya kwa uchumi wa dunia.

Meli za mafuta karibu na Mlango Bahari wa Hormuz
Meli za mafuta karibu na Mlango Bahari wa Hormuz.Picha: Altaf Qadri/AP Photo/picture alliance

Msemaji wa wizara hyo Esmaeil Baqaei amehoji kupitia ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X ikiwa ni "jambo la busara kwa mtu kuikata pua yake ili kuukarabati uso".

Mzozo huo na Iran tayari umekwishayumbisha ustawi wa uchumi wa dunia.  Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, na wenzake wa Benki ya Dunia na Wakala wa Kimataifa wa Nishati, IEA wamesema jana Jumatatu kwamba uharibifu uliotokea kwenye miundombinu ya mafuta kutokana vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran utaendelea kuzifanya bei za mafuta na mbolea duniani kuwa juu "kwa kipindi kirefu".

Mkurugenzi wa IEA  Fatih Birol amesema mparaganyiko wa usambazaji mafuta kutokana na mzozo huo ni "changamoto kubwa zaidi kwa usalama wa nishati" katika historia ya ulimwengu.

Pipa la mafuta ghafi lilipindukia kwa mara nyingine dola 100 jana Jumatatu na kuna wasiwasi bei huenda itaendelea kupanda.

Miito ya pande mbili kutumia diplomasia badala ya vita yatawala 

Marekani  New York 2025 | Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Bianca Otero/ZUMA/IMAGO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alizirai Marekani na Iran kurejea kwenye meza ya mazungumzo na kuipa tena diplomasia nafasi badala ya makabiliano.

Hadi sasa bado hakuna taarifa zozote kuhusu awamu nyingine ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili baada ya yale ya mwishoni mwa juma mjini Islamabad kumalizika bila makubaliano.

Rais Trumpwa Marekani alisema jana kuwa yuko tayari kuendelea na mazungumzo na kudokeza kwamba mawasiliano yanafanyika baina ya pande hizo mbili.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov alizungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Iran Abbas Araghchi na kuirai Tehran kutumia njia zote kuhakikisha vita havitazuka tena baada ya muda wa sasa wa usitishaji mapigano kumalizika.