Tishio la Usalama Marekani
30 Oktoba 2010Marekani imedhibitisha kuwa miripuko iligunduliwa katika vifurushi viwili , vilivyokuwa vinaelekea nchini humo. Rais Barack Obama amesema katika mkutano na waandishi habari uliofanyika katika ikulu kwamba vifurushi hivyo vilikuwa vinatarajiwa kupelekwa katika maeneo mawili ya kuabudu ya Wayahudi mjini Chicago. Pia amesema kuwa vifurushi hivyo vilitoka Yemen na viligunduliwa Dubai na Uingereza.
Wizara ya usalama wa ndani nchini Marekani ,imesema inaimarisha hatua za kiusalama kutokana na tishio hilo.
Kwengineko ndege za kivita za Marekani zimeisindikiza ndege ya abiria ya kampuni ya Emirates kutoka Umoja wa falme za kiarabu hadi mjini New York ambako ilitua salama. Shirika la kijeshi la Marekani na Canada, NORAD limesema lilikuwa na shaka kwasababu ndege hiyo iliyokuwa na abiria 201 ilisafiri katika anga ya Canada na baadaye kuingia katika anga ya Marekani. Ndege mbili za kivita za Marekani ziliisindikiza ndege hiyo hadi katika uwanja wa ndege wa John F Kennedy nchini Marekani. Shirika la upelelezi la FBI limesema kuwa ndege hiyo ilikuwa na mizigo kutoka Yemen.
Mwandishi: Maryam Abdalla/Rtre/Afpe Mhariri:Sekione Kitojo