″Tatizo si la kisheria bali ni la kijamii″ | Magazetini | DW | 18.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

"Tatizo si la kisheria bali ni la kijamii"

Leo hii hasa ni masuala mawili yaliyozingatiwa na wahariri wa magazeti ya humu nchini: Kwanza mauaji yaliyotokea Jumatatu katika chuo kikuu cha Blacksburg nchini Marekani ambapo watu 33 waliuawa katika shambulio la risasi. Suala la pili ni kupelekwa vikosi vya Umoja wa Mataifa katika eneo la Darfur, Sudan.

Tukianza na matukio nchini Marekani, wahariri wengi wa magazeti wameandika haki ya kubeba silaha haifai kutumiwa siku hizi. Hilo ni gazeti la “Neues Deutschland”:

“Hakuna asiyejua kwamba hata sheria kali hazizuii damu kumwagika. Na hakuna nchi ambako mauaji yamekuwa yakizitikisa shule na vyuo vikuu kama Marekani . Huko wataalamu wanasema kuna uwiano kutokana na ile hali kwamba ni rahisi na halali mtu kujinunulia silaha.Yaonyesha hawajajifunza na yaliyotokea miaka ya nyuma.”

Mhariri wa “Märkische Oderzeitung” pia anataja wasiwasi juu ya sheria huru ya siasa, lakini anasema suluhisho halipatikani kupitia udhibiti mkali. Anaendelea kuandika:

“Ni wazi kwamba, majadiliano juu ya uhuru wa silaha nchini Marekani yatakuwa makali. Lakini sheria hazitabalidishwa. Halafu kutasikika mwito wa kutaka ipigwe marufuku michezo ya video zenye kuonyesha mauaji. Hiyo pia haitasaidia. Yule ambaye anataka kununua silaha, anaweza kufanya hivyo, hata nchini Ujerumani ambapo sheria ni kali zaidi. Vilevile marufuku dhidi ya michezo ya video hayana maana katika enzi ya mtandao wa Internet ambamo kila kitu kinapatikana bila ya pingamizi. Badala yake sisi binadamu tunapaswa kukaa kwa karibu zaidi, kuangaliana na kutunzana.”

Ni maoni yagazeti la “Märkische Oderzeitung.” - “Tatizo si la kisheria bali ni la kijamii” ndivyo tunasoma vilevile katika gazeti la “Allgemeine Zeitung” la mjini Mainz:

“Tatizo la msingi halitatatuliwa, yaani ukali wa jamii ya Kimarekani ambamo ni muhimu sana kushinda katika maisha. Wale wanaoshindwa lakini, na hata wale wanaoamini wameshindwa, wanaweza kukata tamaa haraka. Si kwamba kila mmojawao ataanzisha mauaji kama haya, lakini wengi.”

Kwa mada ya pili: Mwanzoni mwa wiki hii, serikali ya Sudan imekubali jeshi la Umoja wa Mataifa lipelekwe Darfur kuhakikisha amani katika eneo hilo la kivita. Gazeti la “Süddeutsche Zeitung” lakini linaonya kutokuwa na matumaini mno:

“Ingekuwa ni njozi kuamini kuwa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wataweza kuleta amani Darfur. Huenda jeshi hilo litaweza kupunguza dhiki na kuzuia mauaji makubwa. Lakini mzozo huu hauwezi kutatuliwa na jeshi. La muhimu ni kwamba serikali ya Sudan na makundi ya waasi waanzishe tena mazungumzo. Pengine habari hiyo mpya juu ya jeshi la Umoja wa Mataifa itasababisha misimamo ilainishwe.”

Ni gazeti la “Süddeutsche Zeitung”. Na hatimaye tunamnukuu mhariri wa “Frankfurter Rundschau” juu ya suala hilo la Darfur:

“Tusiamini serikali ya Sudan imekubali vikosi vya Umoja wa Mataifa kwa sababu ina maslahi yoyote ya kumaliza mzozo wa Darfur. Ukweli wa mambo ni kuwa serikali hii inadhalilisha mzozo huu haradhani, na wakati huo huo kuuchochea kisiri. Sasa Sudan imeshindwa nguvu kwa shinikizo la kisiasa. Shinikizo lazima lizidishwe ili Sudan ilazimishwe kuchukua hatua za kumaliza mzozo huu.”

 • Tarehe 18.04.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHTC
 • Tarehe 18.04.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHTC