Tanzania yaihakikishia Marekani uchaguzi utakuwa huru | Matukio ya Afrika | DW | 09.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Tanzania yaihakikishia Marekani uchaguzi utakuwa huru

Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Profesa Palmgamba Kabudi amemhakikishia balozi wa Marekani nchini humo, kuwa uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki, na kwamba wataheshimu matokeo.

Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Profesa Palamagamba Kabudi alikutana na balozi wa Marekani nchini humo Donald Wright kwa mazungumzo mjini Dar es Salaam, ambapo wawili hao waligusia uchaguzi ujao, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28.

Mwanadiplomasia huyo aliyewasili nchini katika miezi ya hivi karibuni amesema Tanzania kama lilivyo taifa lake Marekani yote yanaelekea kwenye uchaguzi mkuu hivyo kile anachoweza kukisema kuhusu wapigakura wa taifa hili, kinafanana kabisa na kile cha nyumbani kwake.

Soma pia: NEC yakataa mapingamizi ya Lissu dhidi ya Magufuli, Lipumba

Balozi Wright amesema wakati huu ambapo wagombea wanaendelea kuzunguka majukwaani kunadi sera zao, jambo linalopaswa kuzingatiwa na Watanzania ni kutojiweka mbali ya kampeni hizo ili hatimaye  wachague viongozi bora watakawaletee maendeleo wanayotarajia.

Tansania | Wahlen | Wahlstimmen werden abgegeben

Wananchi wametakiwa kutumia vyema haki yao kwa kuchagua viongozi wanaofaa."Ushauri wangu kwa Watanzania utakuwa sawa tu kama ule kwa Wamarekani, ambao ni kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi kwa kupigakura. Kufuatilia wagombea na kubainishi ni nani hasa unadhani atakuwa anafaa kuongoza Watanzania na kuhakikisha sauti yako inasikika kupitia sanduku la kura", alisema balozi Wright.

Soma zaidi:Walioenguliwa Tanzania hawajui hatima yao kuhusu uchaguzi 

Ushauri wa balozi huyo wa Marekani unakuja wakati ambapo wagombea sasa wanaendelea kuchanja mbuga katika maeneo mbalimbali wakijaribu kupenyeza ushawishi wao kwa wapiga kura wanaofikia milioni 29, lakini pia kukiwa na malalamiko ya wagombea kadhaa wa upinzani walioenguliwa kwenye nafasi wanazowania.

Kuhusu nafasi ya uchaguzi huu ambao ni wa sita kufanyika tangu Tanzania irejee kwenye mfumo wa vyama vingi mnamo 1992, Tanzania imesema inatarajia utafanyika kwa uwazi na ukweli na itaheshimu maoni ya wapiga kura.

Tazama vidio 01:02

Tume ya uchaguzi Tanzania yawarejesha wagombea 15 walioenguliwaWaziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema majadiliano yake na Balozi huyo wa Marekani, mbali ya kugusia maeneo mengine ya mashirikiano lakini suala la kufanikisha uchaguzi huu utakaofanyika Oktoba 28 limekuwa kiini cha mazungumzo hayo.

Wakati Tanzania ikielezea mwelekeo wake kwa jumuiya ya kimataifa kuhusu uchaguzi huu, bado haijafahamika kama waangalizi wa nje watapewa nafasi ya kuufuatilia.

Soma zaidi:HRW: Uhuru mashakani kuelekea uchaguzi Tanzania


Katika chaguzi kadhaa zilizopita, waangalizi kutoka Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, pamoja na wale wa Umoja wa Afrika, nchi za SADC na Jumuiya ya Madola walipiga kambi nchini na kutoa tathmini zao kuhusu mwenendo wa chaguzi hizo. Baadhi ya ripoti za jumuiya hizo zilikosowa mwenendo wa chaguzi, huku nyengine zikisifia.