1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaahidi kuisaidia Tanzania kukabili selimundu

George Njogopa26 Septemba 2019

Marekani imetenga dola milioni 120 kusaidia katika utafiti kupambana na ugonjwa wa selimundu katika nchi ambazo tatizo hilo ni kubwa ikiwemo Tanzania.

https://p.dw.com/p/3QHK6
Sichelzellenanämie
Picha: picture alliance / dpa

Marekani imeahidi kuipiga jeki Tanzania kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa selimundu yaani sickle cell na tayari imetenga kitita cha dola milioni 120 kwa ajili ya utafiti wa kupambana na ugonjwa huo.

Fedha hizo zinatarajia kuzinufaisha nchi ambazo tatizo hilo linatajwa kuwa kubwa ikiwamo Tanzania inayoshika nafasi ya tatu barani Afrika kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na tatizo hilo.

Naibu Waziri wa Afya wa Marekani Admiral Brett Giroir ambaye amekuwa na mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi, kando ya kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea mjini New York Marekani amesema taifa lake limedhamiria kusaidia kukabiliana na ugonjwa huo.

Pia, ameutaja mkutano wake na Waziri Kabudi kama mwanzo mpya wa ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili akisema kuwa nchi yake ina nyenzo zote ikiwemo teknolojia ya kupambana na maradhi hayo ili kuboresha maisha ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo.

Amesema katika siku za hivi karibuni Tanzania imekuwa ikipiga hatua katika kuimarisha masuala yanayohusu afya za wananchi wake na kwa maana hiyo ni mkakati wa Marekani kuona kuwa ugonjwa wa seli mundo unapata tiba.

"Marekani imedhamiria kwa thati kukabiliana na tatizo la selimundu na Rais Trump pia amelizungumzia hili mwaka jana na mwaka huu kwamba kituo cha taifa cha utafiti wa afya kitatumia Dola za Marekani milioni 120 mwaka ujao kwa ajili ya utafiti wa kupambana na ugonjwa huu wa selimundu." Naibu Waziri wa Afya wa Marekani Admiral Brett Giroir amesema.

Tanzania na Marekani zitashirikiana katika kufundisha na kujengeana uwezo wa namna ya kupambana na maradhi ya selimundu.
Tanzania na Marekani zitashirikiana katika kufundisha na kujengeana uwezo wa namna ya kupambana na maradhi ya selimundu.Picha: picture alliance / ap

Marekani inaamini kuwa kwa kufanya hivyo itasaidia kuokoa maisha ya watoto wengi wanaokumbwa na tatizo hilo linaloongezeka nchini.

Akizungumzia mpango huo wa Marekani, Waziri Kabudi amesema utafiti na hatimae tiba ya maradhi hayo ya selimundu kwa kiasi kikubwa itainufaisha Tanzania kutokana na kushika nafasi ya tatu katika Bara la Afrika na ya nne duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa seli Mundu.

Amesema Tanzania na Marekani zitashirikiana katika kufundisha na kujengeana uwezo wa namna ya kupambana na maradhi ya ugonjwa huo.

Tanzania ni nchi ya tano duniani kwa kuwa na watu wenye ugonjwa wa selimundu, ikitanguliwa na nchi za India, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Utafiti unaonyesha kuwa kila mwaka nchini Tanzania takribani watoto 11,000 huzaliwa na ugonjwa huo.

Moja ya sababu ya ongezeko hilo ni uelewa mdogo juu ya ugonjwa huo unaohusiana na seli za damu kuwa katika umbo nusu. Huu ni ugonjwa unaorithishana vizazi kwa vizazi ambao chanzo chake ni wazazi wote wawili kuwa na vinasaba vya ugonjwa huo.