Sudan Kusini: Wanadiplomasia 40 wafutwa kazi | Matukio ya Afrika | DW | 17.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Sudan Kusini

Sudan Kusini: Wanadiplomasia 40 wafutwa kazi

Serikali ya Sudan Kusini imesema imewatimua wawakilishi wake wa kibalozi 40 katika nchi za nje. Wanadiplomasia hao hawakuonekana kazini kwa miaka mingi na kwa hivyo kuanzia sasa wameondoshwa kwenye mfumo rasmi wa malipo.

Wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imeeleza kwamba ilijaribu kuwasiliana na maafisa hao bila ya mafanikio, ikiwa pamoja na wale waliokuwa wanaiwakilisha nchi yao Merakani na Uingereza. Hakuna afisa hata mmoja aliyejibu au aliyerejea nchini Sudan Kusini. Kwa bahati mbaya wizara hiyo haikuwa na njia nyingine ila kuwatimua mabalozi hao baada ya juhudi kubwa kushindikana ya kuwataka warejee nyumbani na kufanya kazi nchini. Hatua ya kuwafukuza kazi watu hao wengi imetokana na wao kutorejerea nyumbani baada ya mihula yao kumalizika.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Kusini Mawien Makol ameliambia shirika la habari la AFP kuwa mabalozi hao hawajulikani waliko na majina yao yameshapishwa hadharani. Wote waliorodheshwa hawatalipwa tena mishahara yao na kwamba wameachishwa kazi rasmi mara moja na wameamriwa kurejesha pasi zao za kusafiria pamoja na zile za familia zao.

Wametakiwa kukabidhi hati hizo kwenye balozi za Sudan Kusini zilizopo karibu nao. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ameeleza kuwa baadhi ya maafisa hao walikuwa wanaiwakilisha nchi yao Kenya na Uganda. Tamko lilitolewa limeeleza kuwa hatua ya kuwafukuza watumishi hao inatokana na sheria inayohusu masuala ya kibalozi ya mwaka 2011. Kwa mujibu wa sheria hiyo, yeyote ambaye haendi kazini kwa muda wa zaidi ya siku 45 bila ya kutoa maelezo atahesabika kuwa ameacha kazi.

Uganda Südsudan - Friedensgespräch zwischen Präsident Kiir, Oppositionsführer Machar und der ugandische Präsident Museveni (Getty Images/AFP/S. Sadurni)

Kiongozi wa Upinzani wa Sudan Kusini Riek Machar na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kwenye mazungumzo ya amani nchini Uganda. Katikati: Rais wa UgandaYoweri Museveni

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Makol amekanusha madai kwamba serikali ya Sudan Kusini imechukua hatua hiyo ili kuokoa fedha kutokana na kubanwa na uhaba wa fedha. Hata hivyo hivi karibuni  serikali ya Sudan Kusini ilizifunga balozi zake kadhaa za nje na baadhi ya mabalozi na watumishi wengine wamekuwa wanalalamika juu ya kulipwa mishahara yao kwa kuchelewa. Lakini Makol ameeleza kuwa zoezi hilo ni jambo la kawaida na halihusiani na matatizo ya kiuchumi.

Sudan Kusini ambayo bado ni nchi changa kabisa duniani, ilitumbukia katika mgogoro mnamo mwaka 2013 yaani miaka miwili tu mara baada ya kujipatia uhuru wake. Mgogoro huo wa kivita ulisababisha vifo vya watu 380,000 na kuwafanya wengine zaidi ya milioni 4 takariban thuluthi moja ya watu wa nchi hiyo  wayakimbie makaazi yao. Mapigano yalisimishwa kabisa baada ya mkataba wa amani kutiwa saini mwezi Septemba mwaka uliopita lakini utekelezaji wake umekwama. Pamoja na hayo hatua ya kuunda serikali ya umoja tarehe 12 ya mwezi  huu imeahirishwa kwa muda wa nusu mwaka.

Chanzo:/AFPE