Sheria ya Uchaguzi wa Zimbabwe yababaisha | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.03.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Sheria ya Uchaguzi wa Zimbabwe yababaisha

Kundi la Wanasheria wa Zimbabwe linalogombea haki za binadamu-ZLHR-limeshtushwa na kile kilichoitwa "hitilafu" katika sheria ya uchaguzi.

*** Stäcker, Chaos, Folter, Haft und Hoffnung - Simbabwe vor den Wahlen *** Zimbabwe's President Robert Mugabe addresses Zanu PF party supporters at a campaign rally at Mubaira Growth Point, 120km outside Harare, Zimbabwe, 14 March 2008. In power since 1980, President Mugabe has for the first time got to contend with two other presidential hopefuls in the 29 March elections. EPA/STR +++(c) dpa - Report+++

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe akihotubia mkutano wa hadhara wa ZANU-PF

Kwa mujibu wa kundi hilo, maelezo ya utaratibu utakaoamua mshindi wa uchaguzi wa rais unababaisha.Kuambatana na kipengele kikuu cha Sheria ya Uchaguzi,iwapo hakuna mgombea atakaepata zaidi ya asilimia 50 ya kura,basi washindi wawili wa kwanza watapaswa kupambana katika kipindi cha siku 21 katika rauni ya pili ya uchaguzi.

Lakini kifungu kingine kwenye sheria hiyo kinachotoa maelezo zaidi ya kipengele kikuu kinasema,mgombea atakaepata kura nyingi zaidi ndio atatangazwa mshindi.

Hayo ni mambo mawili yanayobabaisha,kwa hivyo kundi la ZLHR limemuomba Jaji George Chiweshe alieteuliwa na serikali kama mwenyikiti wa Kamisheni ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC) kuifafanua sheria hiyo kabla ya uchaguzi wa Machi 29.Afisa wa miradi ya ZLHR,Rangu Nyamurindira amemuambia Chiweshe,"hitilafu za masharti yanayohusika na duru ya pili ya uchaguzi,huenda zikasababisha mchanganyo,kwa hivyo zinahitaji kufafanuliwa na Kamisheni ya Uchaguzi.Nyamurindira amesema,kawaida ni kipengele kikuu cha sheria kilicho na uzito katika utaratibu huo kama ilivyowahi kuamuliwa mara kadhaa palipozuka migogoro ya aina hiyo.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaonya,iwapo Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe atakabiliwa na duru ya pili ya uchaguzi huenda akatumia kifungu kinachoruhusu uwingi wa kura pekee,bila ya kujali maoni ya kisheria. Mchambuzi mmoja akaongezea kuwa Mugabe,mara kwa mara amedhihirisha kuwa sheria inapokuwa dhidi yake, basi hufanya kile kitakachompatia ushindi.

Nyamurindira amesema,kundi lake linazingatia pia kuiomba Mahakama Kuu kupata ufafanuzi kutoka kwa jaji,kuhusu kipengele kitakachotumiwa,iwapo Mugabe atashindwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Mchanganyo huu,ni moja kati ya changamoto tofauti zinazowakabili maafisa wanaoshughulikia vile vile uchaguzi wa bunge lenye viti 210.

Kwa upande mwingine,Mbunge Trudy Stevenson wa tawi dogo la chama cha upinzani cha MDC anaitaka serikali itoe kopi ya majina ya wapiga kura walioorodheshwa kwenye kompyuta.Orodha ya aina hiyo inaweza kuchunguzwa na wataalamu wa kompyuta kutambua iwapo kumefanywa marekebisho kwa maksudi ili kumpendelea Mugabe na chama chake cha ZANU-PF.

Wakati huo huo,mawakili wa Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha Morgan Tsvangirai cha MDC,Tendai Biti aliepeleka Mahakama Makuu maombi ya kupatiwa orodha ya majina ya wapiga kura,wanasema,wamearifiwa na serikali kuwa wataweza kuipata orodha hiyo baada ya uchaguzi.Uwezekano wa kuwepo rauni ya pili,umepewa umuhimu mkubwa katika uchaguzi wa Machi 29.

Safari hii Rais Mugabe mwenye miaka 84,mbali na Morgan Tsvangirai atapambana pia na waziri wake wa fedha wa zamani,Simba Makoni.Mgombea wa nne ni Langton Towungana asiejulikana na wengi.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com