Schalke yatwaa uongozi wa Bundesliga | Michezo | DW | 29.03.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Schalke yatwaa uongozi wa Bundesliga

Manchester United yajiandaa kwa changamoto kesho na B .Munich.

Felix Magath -kocha wa Schalke aiambia Munich (Ho) simama.

Felix Magath -kocha wa Schalke aiambia Munich (Ho) simama.

Schalke, imechukua usukani kuongoza Bundesliga hapo jana baada ya kuizaba Bayer Leverkusen, mabao 2-0 shukurani kwa jogoo lao kevin Kuranyi.

Bayern Munich, ikiwa na miadi kesho na Manchester United katika champions league,inachechemea sio tu kwa kuzabwa mabao 2:1 na Stuttgart uwanjani mwao hapo Jumamosi,bali hata jogoo lao Arijen Robben kutoka Holland,limeumia na hakuna uhakika iwapo litakuwa fit kwa zahama ya kesho na Manu.

Nigeria, imepigwa kumbo nje ya Kombe la Afrika la wachezaji wasiolipwa -kombe la CHAN na kocha wa zamani wa Uingereza, Sven-Goran Eriksson, ndie atakaeiongoza Ivory Coast katika kombe lijalo la dunia nchini afrika kusini.

Bundesliga na Premier League:

Ni Schalke, inayoongoza sasa Bundesliga-Ligi ya Ujerumani,baada ya kuipokonya Bayern Munich usukani jana kufuatia ushuindi wa mabao 2:0 dhidi ya Bayer Leverkusen .Alikuwa mshambulizi wao Kevin Kuranyi, alielifumania mara 2 lango la Bayer Leverkusen.Mabao yake hayo yamemuweka kileleni mwa orodha ya watiaji magoli mengi katika Bundesliga pamoja na Edin Dzeko wa klabu bingwa Wolfsburg. kila mmoja ametia mabao 17.Kwa mabao hayo 2,kocha wa timu ya taifa ya ujerumani Joachim Loew ,ameamua kumuita tena Kuranyi,kujiunga na timu ya taifa na kumsamehe madhamhi yake aliofanya zamani.kwani, wasghambulizi aliowachagua hadi sasa kocha Loew akina Miroslav Klose na Lukas podolski wametia mabao 4 tu kinyume na 17 ya Kuranyi.Kuranyi alisema,

"Bila shaka, hizo ni habari nzuri.Tunajikuta sasa katika awamu ya mwisho na tunapanga kuendelea kutamba zaidi katika mechi ijayo tukicheza kwa nguvu zaidi na kufaulu.Nitatoa mchango wangu na najitahidi kuona timu yangu inafanikiwa."Alisema Kevin Kuranyi, anajiunga tena na Timu ya Taifa kwa Kombe lijalo la dunia.

Wakati Schalke iko kileleni ,Bayern Munich, inauguza maumivu ya stadi wake kutoka Holland ,Arjen Robben alieumia jumamosi pale Stuttgart ilipoiferdhehi Munich uwanjani mwake ilipoizaba mabao 2-1.

sasa hakuna uhakika iwapo Robben atakuwa fit kwa zahama ya kesho ya Champions League kati ya bayern munich na Manchester United.Ni mwishoni mwa wiki iliopita tu pale kocha wa Munich, Van gaal, alipojitapa kwamba msimu huu anataka vikombe vyote 3-viwili vya nyumbani na cham pions league.Ikiwa hatachunga kesho atapata pigo jengine siku tu tangu lile la mwanzo katika uwanja huo huo. Baada ya kuzabwa mabao 2:1 na Stuttgart ,kocha wa Munich alisema,

"Hatukufaulu kwavile daima, ni shida kupata ufumbuzi ukicheza na timu inayojua kujilinda."

Mkiani mwa Ligi,FC Cologne, ilitamba kwa kishindo huko Hannover.Stadi wake iliomuazima kutoka Manchester United, Zoran Tosic,alitia mabao 2 maridadi katika ushindi wa mabao 4:1 wa FC Cologne. Baadae kocha wa Hannover,akinungunika alisema:

"Haiwezekani kabisa kuiachia Cologne, mwanya namna vile na kuiachia nafasi ya kujikomboa kutoka safu ya kuteremshwa daraja ya pili.Tumeifungulia Cologne mlango hasa wa kutia mabayo yale 2 ya kwanza."

Ama katika Premier League, Ligi ya Uingereza,Manchester United inakuja kesho Munich bila wasi wasi wa kuumia yeyote katika kikosi chake.Isitoshe, mabao 4:0 dhidi ya Bolton wanderes hapo jumamosi ni salamu za kutosha M anu ilioipelekea Munich.Wayne Rooney na mlinzi Rio Ferdinand ni fit kabisa. ilikua lakini Chelsea ilioparamia kileleni mwa Premier League mwishoni mwa wiki baada ya kuizaba Aston villa mabao 7-1.

Tugeukie dimba barani Afrika :

Aliekuwa kocha wa Uingereza,mswede Sven-Goran Eriksson, alichaguliwa jana kuwa kocha mpya wa Corte d'iviore au Ivory Coast.na Mariam Abdullah:

Eriksson, ataiongoza Ivory Coast katika Kombe lijalo la dunia hapo Juni,nchini Afrika kusini.Mswede huyo mwenye umri wa miaka 62, aliiongoza Uingereza hadi robo-finali ya Kombe la dunia 2002 na 2006 .Anachunua nafasi ya mbosnia, Vahid Halihodzic, alietimuliwa pale Tembo walipopigwa kumbo na Algeria nje ya Kombe la Afrika la Mataifa nchini Angola, Januari,mwaka huu. Ivory Coast, inayoongozwa na nahodha Didier Drogba, imeangukia kundi la kufa-kupona pamoja na Brazil,Ureno na Korea ya kaskazini.Miaka 4 iliopita, Ivory Coast, iliaga kombe la dunia ilipojikuta kundi gumu kama hilo lililojumuisha Argentina na Holland na kumaliza 3 mbele ya Serbia na Montenegro.

Huko Afrika kusini kwenyewe, Uwanja utakaofungua dimba mjini Johannesberg hapo juni 11 baina ya Bfana Bafana na Mexico na utakaochezewa finali Julai 11, ulijaribiwa hapo Ijumaa kwa mechi kadhaa. Soccer City Stadium, iliandaa mpambano baina ya timu ya Baraza la mji wa Johannesberg na timu ya wakongwe mashuhuri wa dimba mbele ya mashabiki afu kadhaa.Uwanja huu ,umejengwa upya na sasa unachukua mashabiki 94.700.

KOMBE LA AFRIKA (CHAN)

Mwishoni mwa wiki, ilikua duru ya pili ya duru ya kwanza ya kinyan'ganyiro cha Kombe la Afrika la Mataifa la wachezaji wa ndani ya Afrika-Kombe la CHAN.Nigeria, iliaga kombe hili na mapema kwani, ilimudu sare tu 0:0 na jirani yake Niger.Na kwavile, katika duru ya kwanza, Nigeria ilikomewa mabao 2:0 mjini Niamey, Nigeria sasa iko nje.Mabingwa wa Kombe hili jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ilicjhezeshwa kindumbwe-ndumbwe na simba wa nyika-Kameroun kwa kuchapwa mabao 3:0.Kameroun, ikashinda kwa mabao 4:1 kufuatia duru zote 2 na imeingia finali ya Kombe hili 2011 nchini Sudan.

Bafana bafana au Afrika kusini, nayo iliitandika Botswana 2:1 na kusonga mbele .Jirani zao Angola, wenyeji mapema mwaka huu wa Kombe la kawaida la Afrika,ilitimua nje Madagascar kwa 2:0.Zimbabwe , walionea Swaziland kwa kuichapa mabao 3:0 na hivyo, itacheza finali kwa ushindi jumla wa mabao 5-1.

Huko Kampala, Ugandan Cranes, walitamba nyumbani kwa mabao 4:0 na kuitoa Rwanda kwa jumla ya mabao 5:1.Mvua ya magoli pia ilinyesha Dar-es-salaam, kwani, watanzania walilipiga hodi mara 6 katika lango la wasomali na kukaribishwa ndani .Tanzania imeikomea somalia mabao 6:0 na sasa inajandaa kwa changamoto ijayo na Rwanda.

Mwandishi:Ramadhan Ali/afp,dpa,rtr

Mhariri:Abdul-Rahman