Trump asema vita dhidi ya Iran kumalizika hivi karibuni
15 Aprili 2026
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa vita dhidi ya Iran viko karibu kuisha. Kauli hiyo inakuja wakati jeshi la Marekani likitangaza kutekeleza kikamilifu vizuizi vyake dhidi ya bandari za Iran karibu na Mlango Bahari wa Hormuz.
Hata hivyo, Iran imetangaza kuwa itatumia bandari mbadala, tofauti na zile za kusini mwa nchi, ili kupitisha mizigo na shughuli zake za baharini.
Kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha FoxNews, rais Trump amesema kuwa Iran inataka makubaliano ya haraka na Marekani.
"Nadhani vita iko karibu kumalizika, ndiyo. Kwa maana ninaiona kuwa iko karibu sana kuisha. Unajua nini? Kama ningeondoa majeshi yangu sasa hivi, ingewachukua miaka 20 kuijenga upya nchi hiyo. Na bado hatujamaliza.Tutaona kitakachotokea. Nadhani wanataka sana kufikia makubaliano", alisema Trump.
Wakati huo huo, Pakistan imesema inaendelea na juhudi za kusaidia mazungumzo kati ya Marekani na Iran ili kumaliza mgogoro huo. Kwa mujibu wa Trump, mazungumzo mapya yanaweza kufanyika ndani ya siku mbili zijazo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres naye ametoa mtazamo wa aina hiyo akisema kuna uwezekano mkubwa kwa pande hizo mbili kurejea mezani. Matamshi yake yanafuatia mkutano aloufanya na Naibu Waziri Mkuu wa Pakistan, Ishaq Dar.
Umuhimu wa ukaguzi wa mpango wa nyuklia wa Iran
Mzozo huo wa Mashariki ya Kati tayari umesababisha vifo vya watu zaidi ya elfu tatu nchini Iran, zaidi ya elfu mbili Lebanon, pamoja na wengine nchini Israel na mataifa ya Ghuba. Wanajeshi 13 wa Marekani pia wameuawa.
Nchini Iran, milipuko miwili imetokea katika mji wa Tehran, na kujeruhi watu watatu. Serikali imesema hali iko chini ya udhibiti. Ni kwa mara ya kwanza tukio la aina hiyo kujiri nchini Iran toka kuanza kwa mashambulizi ya Israel na Marekani.
Wakati huo huo, mkuu wa shirika la kimataifa la nishati ya nyuklia, IAEA, amesisitiza umuhimu wa ukaguzi kamili wa mpango wa nyuklia wa Iran kama sehemu ya makubaliano yoyote ya kumaliza vita.
Katika hatua nyingine, Saudi Arabia imetangaza kuweka dola bilioni tatu katika benki kuu ya Pakistan kusaidia uchumi wake unaoyumba kutokana na mvutano wa kikanda.
Vile vile, Australia na Brunei zimekubaliana kuepuka vikwazo vya biashara ya nishati na chakula vinavyotokana na vita hivyo.
Hatimaye, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, anatarajiwa kufanya ziara katika nchi kadhaa za Mashariki ya Kati ili kuendeleza juhudi za amani kabla ya kumalizika wiki ijayo kwa usitishwaji wa muda wa mapigano.