Juhudi za kuusuluhisha mzozo wa Iran na Marekani zinaendelea
14 Aprili 2026
Vyanzo viwili kutoka Washington vimethibitisha kuwa majadiliano bado yanaendelea kuhusu awamu mpya ya mazungumzo. Mwanadiplomasia kutoka moja ya mataifa yanayoshiriki kusuluhisha mzozo huo amesema Tehran na Washington zimekubali kushiriki katika mazungumzo hayo yanayoweza kufanyika Alhamisi.
Vita vya Marekani, Israel na Iran vimeyumbisha masoko na uchumi wa dunia kutokana na kuzuiwa kwa usafirishaji wa bidhaa hasa mafuta katika eneo la mlango bahari wa Hormuz. Awali Iran ilizuia meli kupita kwenye Mlango Bahari huo. Nayo Marekani imeanza jana Jumatatu oparesheni ya kuweka vizuizi vya kijeshi kwenye bandari za Iran.
China imeilaani hatua hiyo ikisisitiza kuwa ni hatari na itakwamisha juhudi za kupata suluhisho la mzozo huo. Aidha msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa China. GUO JIAKUN amezitaka pande husika za mzozo huo kufanya juhudi zaidi ili kuumaliza.
Kauli hiyo ya China imetolewa muda mfupi baada ya Rais XiJinping kukutana na Mwanamfalme wa Abu Dhabi Sheikh Khaled bin Mohamed bin Zayed Al Nahyan mjini Beijing ambapo ametaka uhuru wa mipaka wa mataifa ya Mashariki ya Kati na Ghuba uheshimiwe.
Ufaransa, Uingereza zaandaa mkutano kujadili Mlango Bahari wa Hormuz
Katika hatua nyingine, Ufaransa na Uingereza zinatarajia kuandaa pamoja mkutano unaolenga kuulinda Mlango Bahari wa Hormuz. Kulingana na taarifa kutoka ofisi za wakuu wa mataifa hayo mkutano huo utakaofanyika Ijumaa kwa njia ya video, utayashirikisha mataifa 40. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer wataongoza mkutano huo.
Katika mzozo mwingine unaohusiana na kile kinachoendelea kati ya Iran na Marekani, Israel imesema iko tayari kwa mazungumzo na Lebanon wakati mazungumzo ya kwanza ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili yakitazamiwa kufanyika Washington Marekani.
Hata hivyo Israel imedai kundi la Hezbollah linasalia kuwa tatizo kutokana na kile ilichotaja kuwa kundi hilo linazuia makubaliano ya kumaliza mapigano. Marekani inazishinikiza pande hizo mbili kumaliza mgogoro wao kwa kuhofia kuwa unaweza kukwamisha mazungumzo ya kumaliza vita vya Iran.
Mapema Jumanne, kundi la Hezbollah lilitoa taarifa kuwa halitatazingatia makubaliano yoyote yatakayotokana na mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Israel na Lebanon.