1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Mazungumzo mapya na Iran yanaandaliwa

15 Aprili 2026

Rais Donald Trump wa Marekani ameliambia gazeti la New York Post kuwa awamu ya pili ya mazungumzo na Iran inaweza kufanyika hivi karibu na kwa mara nyingine itakuwa nchini Pakistan.

https://p.dw.com/p/5CB0r
Washington D.C. 2026 | Rais Donald Trump wa Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: Anna Moneymaker/Getty Images/AFP

Trump ameashiria awamu hiyo mpya inaweza kufanyika ndani ya muda wa siku mbili zijazo kwenye mji mkuu wa Pakistan, Islamabad.

Matamshi ya Trump yanarandana na yale yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ambaye pia amezungumzia uwezekano mkubwa wa pande hizo mbili kurejea tena mezani.

Guterres ameyasema hayo baada ya kuzungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Pakistan, Ishaq Dar.

Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance naye ameuambia mkutano mmoja wa hadhara usiku wa kuamkia leo kuwa Trump amedhamiria "kuumaliza mzozo kati ya Marekani na Iran."

Licha ya matumaini ya kurejea mazungumzo, Washington imeapa kuendelea na shinikizo dhidi ya Iran.

Wizara ya Fedha ya nchi hiyo imesema haina mpango wa kulegeza tena vikwazo kwa biashara ya mafuta ya Iran baada ya hapo kabla kuruhusu mauzo ya mafuta ya nchi hiyo kufidia upungufu uliojitokeza baada ya kuzuka vita.

Pande hizo mbili zilikutana mjini Islamabad mwishoni mwa juma lililopita lakini mazungumzo yao yalimalizika bila makubaliano yoyote.

Washington na Terhan ´zatunishiana misuli´ Mlango Bahari wa Hormuz

Wakati wanadiplomasia wanaendelea na juhudi za nyuma ya pazia kujaribu kuandaa duru nyingine ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran katika wakati mataifa hayo mawili ´yanatunishiana misuli´ kwenye Mlango Bahari wa Hormuz.

Pakistan Islamabad 2026 | Viongozi wa Iran na Pakistan
Mazungumzo kati ya Marekani na Iran yaliyofanyika mjini Islamabad Aprili 11, 2026 yalimalizika bila makubaliano. Picha: Office of the Iranian Parliament Speaker/WANA/REUTERS

Marekani imesema imeanza kutekeleza kikamilifu vizuizi vyake dhidi ya bandari za Iran karibu na Mlango Bahari wa Hormuz huku Iran ikitishia kufanya mashambulizi iwapo maslahi yake yatahujumiwa. 

Marekani pia imesema itatumia mzingiro wake kwenye Mlango Bahari wa Hormuz kuongeza mbinyo kwa Iran wa kuinyima mapato ya mauzo yake ya mafuta.

China ambayo ni mnufaika mkubwa wa mafuta ya Iran imeitaja hatua hiyo ya Marekani kuwa "hatari na isiyofaa" hasa baada ya Trump kutishia kuzamisha meli yoyote inayotaka kuingia au kutoka kwenye bandari za Iran.

Katika kujibu hatua hiyo watawala mjini Tehran wamesema nao wamejipanga kuhakikisha hakuna tone hata moja la mafuta kutoka mataifa mengine ya Ghuba litakalosafirishwa kupitia Mlango Bahari wa Hormuz.

Umoja wa Ulaya wasema upatikanaji mafuta ya ndege utatatizika siku zijazo

Vita vya Iran vimesababisha mparaganyiko katika usambazaji mafuta duniani
Vita vya Iran vimesababisha mparaganyiko katika usambazaji mafuta duniani. Picha: Paul Ellis/AFP

Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imeelezea wasiwasi mkubwa wa kukumbwa na matatizo ya usambazaji wa mafuta ya ndege katika siku za usoni kutokana na vita vya Iran.

Wasiwasi huo umetolewa wakati wanadiplomasia wanaendelea na jitihada za kuitisha duru ya pili ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran kwa lengo la kuepusha kurejea tena kwa vita.

Msemaji wa Halmashauri Kuu ya umoja huo, Anna-Kaisa Itkonen, amesema bara la Ulaya linaweza kukabiliwa na ukosefu wa mafuta ya ndege katika kipindi kifupi kijacho kutokana na kutatizika kwa usambazaji wa nishati duniani tangu kuzuka kwa vita vya Iran.

Amearifu kwamba ingawa hivi sasa bado nishati hiyo inapatikana lakini mparaganyiko wa biashara ya mafuta ulioshuhudiwa katika wiki 6 zilizopita unatishia hatma ya upatikanaji wa mafuta ya ndege.

Tayari hivi sasa kampuni za ndege barani Ulaya zimepunguza sehemu ya safari na nyingine zimetahadharisha abiria kufikiria mara mbili kuhusu mipango yao ya safari.

Karibu asilimia 20 ya mafuta yote ya ndege duniani husafirishwa kupitia Mlango Bahari wa Hormuz ambao hivi sasa umefungwa na Iran tangu Marekani na Israel zilipoishambulia nchi hiyo mwishoni wa Februari.