Putin na Hollande wakubali kushirikiana kuikabili IS | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Putin na Hollande wakubali kushirikiana kuikabili IS

Rais wa Ufaransa Francois Hollande na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wamekubaliana kushirikiana dhidi ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu IS lakini tofauti zinasalia kuhusu hatma ya Rais wa Syria Bashar Al Assad

Hayo yanajiri huku Ujerumani ikiuetetea uamuzi wake wa kujiunga katika vita dhidi ya IS. Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema nchi yake na Ufaransa zitabadilishana taarifa kuwasaidia kutambua ngome za wanamgambo wa IS nchini Syria.

Putin amesema nchi hizo mbili zitabadilishana taarifa za kijasusi kutambua ni maeneo gani yanadhibitiwa na IS na ni yapi yanadhibitiwa na waasi ambao sio magaidi wanaopinga kuwepo madarakani kwa Rais Assad ambao hawapaswi kulengwa katika mashambulizi ya kijeshi.

Makubaliano hayo kati ya Ufaransa na Urusi ndiyo madhubuti zaidi kufikiwa na Hollande ambaye amekuwa akifanya juhudi kabambe kutafuta uungwaji mkono katika vita dhidi ya wanamgambo wa IS waliodai kufanya mashambulizi makubwa ya kigaidi mjini Paris tarehe 13 mwezi huu na kuwauwa watu 130.

Assad bado ni chanzo cha tofauti

Hollande amesisitiza kuwa kiongozi wa Syria hana nafasi katika mustakabali wa siku za usoni wa Syria, suala ambalo Putin ambaye ni mshirika mkubwa wa Assad amekataa kukubaliana nalo.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande na wa Urusi Vladimir Putin

Rais wa Ufaransa Francois Hollande na wa Urusi Vladimir Putin

Urusi pia imekataa kukubali moja kwa moja kujiunga na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani unaofanya mashambulizi ya angani dhidi ya IS nchini Syria na Iraq.

Putin amesema Urusi itazingatia kujiunga na muungano huo wa kijeshi iwapo watakubaliana na nchi husika kuhusu mfumo wa pamoja wa kuendesha mashambulizi hayo dhidi ya IS.

Urusi imekuwa ikifanya kampeni sambamba ya mashambulizi ya angani dhidi ya IS tangu tarehe 30 mwezi Septemba kufuatia ombi la kufanya hivyo kutoka kwa Rais Assad.

Kabla ya kuelekea Moscow, Hollande pia alipata uungwaji mkono kutoka kwa Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ambaye aliliomba bunge la Uingereza hapo jana kuidhinisha nchi hiyo kujiunga na kampeini dhidi ya IS.

Cameron ameiruhusu Ufaransa kutumia kambi yake ya kijeshi iliyoko Cyprus kufanya shughuli za jeshi lake la angani dhidi ya IS.

Nchini Ujerumani Waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen amesema Ujerumani itatoa ndege zake za kufanya upelelezi, manowari, ndege za kujaza mafuta na ndege za kuilinda meli ya Ufaransa ya kubeba ndege za kijeshi-Charlie de Gauelle.

Von der Leyen amesema Ufaransa ilishambuliwa vibaya na IS na wanafahamu kuwa mashambulizi kama hayo yanaweza kuifika Ujerumani au nchi nyingine wakati wowote.

Ujerumani kuisaidia Ufaransa dhidi ya IS

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier na von der Leyen wameutetea uamuzi wa serikali ya Ujerumani kujiunga na kampeini ya kijeshi dhidi ya IS.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier na wa ulinzi Ursula von der Leyen

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier na wa ulinzi Ursula von der Leyen

Von der Leyen na Steinmeier wamewaambia wanahabari kuwa mbali na misaada hiyo ya kijeshi katika vita dhidi ya IS, juhudi za kuleta suluhisho la kisiasa katika mzozo wa Syria, zinahitajika katika siku za usoni.

Mawaziri hao wawili wamesema kampeni ya kijeshi Syria inaambatana kikamilifu na sheria za kimataifa na kusisitiza umuhimu wa kuungana na Ufaransa katika azma yake ya kuwashinda wanamgambo wa IS.

Msaada huo wa Ujerumani sharti uidhinishwe na baraza la mawaziri na kuungwa mkono na bunge. Ofisi ya Rais wa Ufaransa imesema Hollande ameishukuru mno Ujerumani kwa kumuunga mkono katika azma yake ya kukabiliana na IS.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/dpa

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com