OIC yasema Jerusalem ni ya Palestina | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

JERUSALEM

OIC yasema Jerusalem ni ya Palestina

Viongozi wakuu wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) wamesema wanaitambua Jerusalem kama mji wa Palestina na kwamba hawatakubali kuona hilo likibadilika, wakiitaka Marekani kufuta msimamo wake.

Wakikutana jijini Istanbul hivi leo (13 Disemba), viongozi wameitaka Marekani kufuta mara moja uamuzi wake wa kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel, huku wakitishia kuchukuwa hatua kali dhidi ya Marekani na Israel endapo wataendelea na mipango yao ya kuufanya mji huo mtukufu kwa dini zote tatu - Ukritso, Uislamu na Uyahudi - kuwa makao makuu ya Israel. 

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina amewaambia viongozi wajumbe wa mkutano huo kwamba uamuzi wa Marekani kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel ulikuwa uhalifu, akiifananisha na kitendo cha Donald Trump kuugawa mji huo kama vile ni sehemu ya Marekani. Na kwayo, amesema Abbas, serikali ya Marekani haiaminiki tena kwenye mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati.

"Haitakubalika tena kwa Marekani kuwa na jukumu lolote kwenye mchakato wa kisiasa kwa sababu imejiegemeza upande mmoja wa Israel. Huo ndio msimamo wetu na tunataraji nanyi mutatuunga mkono."

Akiufungua mkutano huo, mwenyeji Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki, alisema anabeba jukumu la kuitangaza rasmi Jerusalem kuwa mji mkuu wa dola la Palestina huku akitaka uungwaji mkono wa viongozi wengine wa Kiislamu duniani.

"Nazialika nchi zote ambazo zinalinda sheria ya kimataifa na haki, kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa dola la Palestina lililokaliwa kimabavu. Hatuwezi kuchelewesha hatua hii zaidi. Kama nchi za Kiislamu, hatutavunjika moyo kamwe kwenye madai yetu ya Palestina yenye mamlaka kamili na iliyo huru ambayo Jerusalem ni mji wake mkuu."

"Lazima Jerusalem isalie ya Waislamu"

Tayyip Erdogan

Mwenyeji wa mkutano, Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki, anataka Jerusalem itambuliwe rasmi kama mji mkuu wa Palestina.

Erdogan aliwaambia viongozi na mawaziri hao zaidi ya 50 wa mataifa ya Kiislamu kwamba uamuzi wa wiki iliyopita wa Trump ulikuwa zawadi kwa vitendo vya Israel, ukiwemo ukaliaji kimabavu, ujenzi wa makaazi ya walowezi, utwaaji wa ardhi na mauaji na ghasia zilizochupa mpaka.

Naye Rais Hassan Rouhani wa Iran alisema kuwa nchi yake iko tayari wakati wowote kusaidiana na mataifa mengine kuhakikisha uhuru wa Palestina unapatikana na kuurejesha nyuma ule aliouita ukorofi wa Israel na Marekani.

"Marekani haijawahi kuwa mpatanishi mkweli na kamwe haitakuwa. Kitendo hiki cha sasa kimelifanya hilo lionekane wazi kwa watu wote waliotarajia Marekani ingelikuwa na nia ya kutatua suala la Palestina. Kwamba Marekani inachotaka ni kupata maslahi makubwa zaidi kwa Mazayuni na haiheshimu matakwa halali ya Wapalestina."

Jerusalem, mji unaozingatiwa na Mayahudi, Wakristo na Waislamu kuwa mtukufu kwao, ni mahala ulipo msikiti wa tatu kwa utukufu kwa Waislamu na umekuwa kiini cha mzozo wa Israel na Palestina kwa miongo kadhaa sasa.

Israel iliitwaa sehemu ya mashariki ya mji huo kutoka kwa Waarabu mwaka 1967 na kisha kuifanya kuwa sehemu yake, kitendo ambacho kamwe hakijawahi kutambuliwa na mataifa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com