Obama atetea uamuzi wa kumshambulia Gaddafi ili kuepusha mauaji halaiki | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.03.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama atetea uamuzi wa kumshambulia Gaddafi ili kuepusha mauaji halaiki

Obama asema utawala wake umechukua hatua za kijeshi ili kuepusha maangamizi ya raia nchini Libya

default

Rais Barack Obama.

Rais Obama ameutetea uamuzi wa utawala wake wa kumshambulia Kanali Gaddafi. Amesema hatua hiyo ilikuwa ya lazima ili kuzuia mauaji halaiki.

Wakati huo huo wajumbe kutoka nchi zaidi ya 40 leo wanakutana mjini London kujadili njia za kuutatua mgogoro wa Libya

Rais Obama amewaambia wananchi wake kwamba Marekani imezuia mauaji halaki nchini Libya. Rais Obama alieleza hayo katika hotuba aliyoitoa kwenye Chuo Kikuu cha kijeshi mjini Washington na kutangazwa moja kwa moja na televisheni. Amesema laiti jumuiya ya kimataifa inengelisuasua kwa siku hatamoja zaidi tu , pangelitokea mauaji halaiki katika mji wa Benghazi.

Amesema endapo Marekani ingeendelea kusubiri mauaji halaiki yangelitokea katika mji huo na kuliathiri eneo lote, na yangelizisakama nafsi za watu duniani kote.Amesema kuacha mauaji yatokee kusingelingana na maslahi ya Marekani.

Rais Obama ameeleza kwua kama Rais wa Marekani, hakutaka kusubiri kuona picha za maangamizi na makaburi ya jumuiya bila ya kuchukua hatua.

Hata hivyo Rais huyo ameonya vikali dhidi ya kujaribu kumwondoa Gaddafi kwa kutumia nguvu. Amesema kufanya hivyo kutakuwa kurudia mauaji yaliyotokea nchini Iraq.Obama ameeleza kuwa mnamo muda wa mwezi mmoja tu, Marekani imeshirikiana na washirika wake wa kimataifa katika kujenga mfungamano mkubwa na kuweza kupewa jukumu na jumuiya ya kimataifa la kuwalinda raia nchini Libya.

Lakini amesisitiza kwamba lingekuwa kosa kulitelekeza jukumu hilo kwa lengo la kuleta mabadiliko ya utawala nchini Libya.Ameeleza kuwa kuzipanuza operesheni za kijeshi ili kumwangusha Gaddafi kungelikuwa kosa

Wakati huo huo wajumbe kutoka nchi zaidi ya 40 wanakutakana mjini London leo kujadili njia za kuutatua mgogoro wa Libya.Mkutano huo utahudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki -Moon, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kuihami ya NATO Anders Fogh Rasmussen na wajumbe wa Umoja wa nchi za Kiarabu.

Muda mfupi kabla mkutano huo kuanza, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa waliwasilisha mada inayotoa mwito wa mwanzo mpya nchini Libya.Sarkozy na Cameron wametoa mwito kwa wafuasi wa Gaddafi kuwataka watengane na kiongozi huyo.

Hata hivyo mkutano wa mjini London unafanyika bila ya Urusi ambayo haikualikwa.Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Sergei Lavrov hatahudhuria mkutano huo kwa sababu nchi yake siyo sehemu ya mfungamano wa kimataifa unaochukua hatua za kijeshi dhidi ya Kanali Gaddafi.

Hapo awali waziri Lavrov aliyakosoa mataifa yanayoishambulia Libya kwa kuvuka mipaka ya yale yaliyopitishwa katika azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mwandishi/ Rüdiger Paulert/ZAR/
Tafsiri/Mtullya abdu/

Mhariri/Abdul-Rahman, Mohammed.

 • Tarehe 29.03.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/10jXr
 • Tarehe 29.03.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/10jXr

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com