Obama amteua balozi mpya wa Marekani Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.02.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama amteua balozi mpya wa Marekani Syria

Chama cha Republican chapinga uteuzi wa Robert Ford

Rais wa Marekani Barack Obama

Rais wa Marekani Barack Obama

Rais wa Marekani Barack Obama amemteua mwadiplomasia Robert Ford kuwa balozi wa kwanza wa Marekani nchini Syria baada ya kipindi cha miaka mitano kwa lengo la kuboresha uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kuzipa msukumo mpya jitihada zake za kusaka amani ya Mashariki ya Kati. Hata hivyo hatua ya rais Obama imepingwa vikali na wanasiasa wa chama cha Republican huko Marekani.

Iwapo ataidhinishwa na baraza la seneti la Marekani, bwana Robert Ford atakuwa balozi wa kwanza mjini Damascus tangu Marekani ilipomuondoa balozi wake baada ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafik Hariri, kuuwawa kwenye shambulio la bomu mnamo Februari mwaka 2005 linalodaiwa kufanywa na Syria. Balozi Ford atakuwa na kibarua cha kushauriana na serikali ya Syria kuhusu njia za kuimarisha mahusiano huku akishughulikia maswala nyeti ambayo yameendelea kuzusha wasiwasi.

Rais Obama amekabiliwa na mtihani mkubwa katika juhudi zake za kushirikiana Iran na kutafuta amani baina ya Israel na Wapalestina mwaka wa kwanza madarakani na sasa anaonekana akitafuta njia mpya ya kuondoa mkwamo uliopo.

Rais Obama amesema, "Mojawapo ya kitu cha kwanza ambacho ningekifanya kusongeza mbele juhudi za kidiplomasia Mashariki ya Kati ni kutoa ishara kwamba tunahitaji kuzungumza na Iran na Syria."

Lakini wadadisi wanasema uwezekano ni mdogo kwa serikali ya Syria, ikiongozwa na rais Bashar al Assad, ambayo yenyewe inang´ang´ana kubakia madarakani, kujitenga na Iran au kufanya makubaliano ya haraka na Israel. Samir Seifan, mtaalam wa uchumi na siasa mjini Damascus Syria anasema, "Marekani ndiyo mshirika mkubwa. Bila Marekani hakuna anayeweza kupata amani. Syria iko tayari kuendeleza mazungumzo ya amani na Israel, lakini Israel haitaki. Kwa hiyo hilo ndilo swala muhimu kati ya Syria na Marekani sasa.

Ukosoaji

Lakini uteuzi wa Robert Ford umezusha ukosoaji mkali kutoka kwa wanasiasa wa chama cha Republican nchini Marekani wakilalamikia sera ya rais Obama ya kushirikiana na maadui wa Marekani. Bi Illeana Ros-Lehtinen, mwanasiasa wa ngazi ya juu wa chama cha Republican katika kamati ya baraza la wawakilishi, inayohusika na uhusiano kati ya Marekani na nchi za kigeni, ameikosoa hatua ya rais Obama akiileza kuwa kitendo cha kutojali na ni kama zawadi kwa adui wa Marekani. Amesema uteuzi wa rais Obama unatoa ujumbe kwamba ni bora kuwa adui mkaidi badala ya kuwa mshirika mtiifu wa Marekani.

Bi Ros-Lehtinen amesema licha ya utawala wa Marekani kujaribu kuinyoshea mkono Syria, taifa hilo linaendelea kufadhili makundi ya kigaidi yenye msimamo mkali wa kidini kama vile Hezbollah na Hamas, kuhujumu uhuru wa Lebanon na kuendelea na mpango wake wa kutaka kutengeneza silaha hatari na makombora.

Utawala wa rais Obama ulitangaza mwanzoni mwa mwezi huu kwamba utapelaka balozi nchini Syria, na kuwasilisha jina la Robert Ford kwa serikali ya Damascus kukamilisha itifaki ya kidplomasia ili jina hilo liidhinishwe kabla kutangazwa rasmi. Wanasisasa wa Republican katika bunge la Marekani waliipinga hatua hiyo.

Tangazo la uteuzi wa balozi Robert Ford limetolewa siku moja kabla ziara ya naibu waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani, Willaim Burns, nchini Syria, inayotarajiwa kuendeleza mdahalo na utawala wa Damascus juu ya maswala yote ya uhusiano uliovurugika baina ya Marekani na Syria.

Ford ambaye sasa yuko katika ubalozi wa Marekani mjini Baghdad Irak, alikuwa balozi nchini Algeria kati ya mwaka 2006 na 2008 na balozi mdogo nchini Bahrain. Amefanya kazi pia huko Izmir na mjini Cairo, Misri.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE

Mhariri: Othman Miraji

 • Tarehe 17.02.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/M3Xy
 • Tarehe 17.02.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/M3Xy
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com