NATO kukutana na Urusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.04.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

NATO kukutana na Urusi

Mabalozi wa Jumuiya ya kujihami ya NATO na Urusi watakutana kwa mara ya kwanza kwa karibu miaka miwili iliyopita. NATO ilisitisha ushirikiano wake na Urusi kutokana na mzozo wa Crimea.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltnberg, amesema NATO pamoja na Baraza la Urusi, watakutana katika makao makuu ya jumuiya hiyo mjini Brussels katika wiki mbili zijazo. Mkutano huo wa kujenga utafanyika kwa mara ya kwanza tangu NATO ilipoamua kusitisha uhusiano wake wa ngazi ya juu na Urusi, baada ya nchi hiyo kulichukua eneo la Crimea iliyoko nchini Ukraine na kuanza kuwaunga mkono waasi wa mashariki mwa Ukraine.

Wawakilishi wa jumuiya hiyo na Urusi waliacha wazi ushirikiano wa kijeshi na kisiasa, lakini kwa mara ya mwisho mkutano wa mashauriano ulifanyika Juni, 2014. Stoltenberg, amesema pande hizo mbili zitajadiliana kuhusu mizozo ndani na kuzunguka Ukraine, hasa katika kutekeleza makubaliano ya Minsk. Pia watazungumzia usalama nchini Afghanistan na kuhusu shughuli za kijeshi, zikiangazia zaidi kuhusu uwazi na uwezekano wa kupunguza hali ya hatari.

Hata hivyo, Stoltnberg amesema hakutakuwa na kurejea katika uhusiano kama kawaida hadi hapo Urusi itakapoheshimu tena sheria za kimataifa, akitolea mfano wa Rasi ya Crimea.

Mvutano mkubwa kati ya NATO na Urusi

NATO ilisitisha uhusiano na Urusi baada ya nchi hiyo kuteka eneo la Crimea

NATO ilisitisha uhusiano na Urusi baada ya nchi hiyo kuteka eneo la Crimea

Mzozo wa Ukraine ulisababisha mvutano mkubwa na hatari zaidi kati ya NATO na Urusi, tangu kumalizika kwa Vita Baridi. Urusi imeielezea NATO kama kitisho chake namba moja cha usalama na itaendelea kufanya uchunguzi kuhusu operesheni za anga na kijeshi za jumuiya hiyo.

Katika kujibu hoja hiyo, NATO inayoongozwa na Marekani, iliwahakikishia wanachama wake wa Ulaya Mashariki kwa kupeleka majeshi zaidi na operesheni kubwa za kijeshi.

Uamuzi wa kufanyika mkutano huo wa ngazi ya juu, umefikiwa wakati ambapo Urusi imejifanya kuwa mchangiaji muhimu katika mizozo kadhaa, ikiwemo Syria, Ukraine na Nagorno-Karabakh. Wakati huo huo, Urusi hivi karibuni ilitafuta ushirikiano mkubwa na mataifa ya Magharibi, hasa kuhusu ugaidi, katika juhudi za kuondoa hatua ya kutengwa kwake.

Msukumo wa Urusi kuongeza ushirikiano wake wa kidiplomasia na kijeshi katika kile inachodhani kuwa jadi yake ya ushawishi, umesababisha msuguano kati ya nchi wanachama wa NATO katika Ulaya Mashariki na Uturuki.

Hata hivyo, hatua ya Uturuki kuidungua ndege ya kivita ya Urusi katika mpaka wa Syria mwaka uliopita, ilielezea hatari ya kijeshi iliyofanywa na pande zote mbili na kusababisha hali ya kutoelewana. Hali kama hiyo imejitokeza tena wiki hii katika eneo la Nagorno-Karabakh, ambako Urusi na Uturuki zina wanajeshi wake katika pande tofauti zinazozoana katika mzozo huo.

Wakati huo huo, baada ya mzozo wa miaka miwili nchini Ukraine, mataifa ya Magharibi yana nia ya kuutekeleza mkataba wa Minsk, ambao umesababisha kupungua kwa ghasia, lakini haujatatua masuala makubwa ya kisiasa. Nchini Syria, ambako Urusi inaiunga mkono serikali ya Rais Bashar al-Assad, mataifa ya Magharibi yanaweza kuangalia jinsi ya kushirikiana na Urusi katika mapambano dhidi ya kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu-IS.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ DW

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com