Mzozo wa madeni Ulaya: jee Italy itaifuata Ugiriki? | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.07.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mzozo wa madeni Ulaya: jee Italy itaifuata Ugiriki?

Katika kupambana na kusambaa mzozo wa madeni, nchi ziliomo katika eneo linalotumia sarafu ya Euro zinataka kufuata njia ambayo hadi sasa ilikataliwa.

default

Waziri wa fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, mtu muhimu katika suala la kuyatanzua madeni ya baadhi ya nchi za sarafu ya Euro

Kufilisika kwa Ugiriki ni jambo ambalo sio tena linalokataliwa. Mawaziri wa fedha wa nchi za Euro wanataka kuchunguza namna ya kuyarekebisha madeni ya nchi hiyo na pia  juu ya namna wakopeshaji wa kibinafsi watakavoweza kuinusuru nchi hiyo isifilisike. Kauli mbiu ni: kufanya kila njia ili kuyadhibiti madeni ya Ugiriki. Wakati huo huo, Italy nayo inazidi kuwa katika mbinyo wa walanguzi na tetesi. Hatari ni kwamba kwa muda mfupi bei za dhamana za mikopo za serikali ya nchi hiyo zimepanda na kufikia kiwango cha juu.

Katikati ya wakati ambapo tetesi zimezagaa, mzozo wa sarafu ya Euro unaweza kuikumba Italy, na hivyo kusamabaa. Hivyo ndivyo anavoona waziri wa fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, ambaye kama ilivyokuwa hapo kabla anaiona Ugiriki kuwa ndio tatizo la kimsingi.

"Ufunguo wa suluhisho ni uwezo wa Ugiriki wa kubeba madeni lazima uboreshwe zaidi, yaani uwezo wake wa kuweza kulipa riba na madeni yenyewe, bila ya kuhatarisha uwezo wa kiuchumi wa nchi hiyo. Bila ya shaka, Ugiriki yenyewe, kuliko mambo yote, itabidi ifanye kazi kwa nguvu ili iboreshe uwezo wake wa kubeba madeni. Na sisi sote tunajuwa kwamba watu wengi wameitaka Ugiriki ifuate njia hiyo; lakini hiyo ndio njia pekee ya kupitia ili kukiuka tatizo liliokuweko miaka mingi la bajeti isiokuwa thabiti. Ni hapo ndipo masoko ya fedha yatarejesha imani kwa nchi hiyo."

Kwa hivi sasa masoko hayo hayauangalii kwa jicho zuri uchumi wa Ugiriki. Na ni wazi kabisa kwamba nchi hiyo imeelemewa. Waziri Wolfgang Schäuble alisema lazima mnamo mwezi Agosti uamuzi ufikiwe juu ya msaada wa pili kwa Ugiriki. Wakopeshaji wa kibinafsi watachangia, lakini kwa namna gani ni jambo ambalo hadi sasa halijaamuliwa. Harakati za serekali za nchi ziliomo katika eneo la Euro pamoja na kamisheni ya Umoja wa Ulaya ziko mbioni kutafuta suluhisho. Kamishina wa Umoja wa Ulaya juu ya masoko ya ndani, Michel Barnier, bado anaziona wakala zinazopima uwezo wa kifedha wa kila nchi kuwa ndizo zenye dhamana ya hali ya sasa.

Wahakiki wanasema ikiwa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya inataka kuzidhibiti wakala hizo, basi inakuwa kama vile kamisheni hiyo inataka kuwafanya washenga wa habari mbaya kuwa na dhamana ya hali hii ya sasa.

 Angalau kamishina wa sarafu wa Umoja wa Ulaya, Olli Rehn, alikiri kwamba matatizo mengi yalioko katika eneo la sarafu ya Euro ni ya kujitakia. Tatizo la msingi ni kwamba hadi sasa nchi zanachama wa Umoja huo wa Sarafu ya Euro katika kukopa na uwezo wa kushindana zimekuwa zikidhibitiana kwa kiwango kichache sana. Serekali ya pamoja inayoshughulikia masuala ya uchumi ingeyafanya mambo yawe vingine. Maelezo zaidi juu ya jambo hilo yatajadiliwa baina ya Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Baraza ka mawaziri la nchi wanachama na bunge la Jumuiya ya Ulaya.

EU-Kommissar Olli Rehn Europäische Kommission Wirtschaft und Finanzen

Kamishina wa Umoja wa Ulaya juu ya uchumi na fedha, Olli Rehn

Bwana Rehn alisema ni muhimu kwamba nchi zote wanachama zinafikia malengo ya siasa zao za fedha. Alisema wao katika kamisheni wanaweza tu kuzitolea mwito nchi zanachama, lakini pale ule mpango wa kuwa na serekali itakayoshughulikia masuala ya kiuchumi utakapokubaliwa, basi risala za kamisheni zinaweza kuzilazimisha serekali za nchi.

Na alama kwamba mambo ni ya moto hivi sasa, kuna tetesi kwamba kutafanywa mkutano maalum wa kilele wa nchi za Euro ijumaa ijayo. Hata hivyo, neno mkutano juu ya mzozo ni mwiko kutajwa huko Brussels.

Mwandishi: Hasselbach,Christoph/ZR/Othman Miraji.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

 • Tarehe 13.07.2011
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/11u7T
 • Tarehe 13.07.2011
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/11u7T

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com