1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa kisiasa wachukua mwelekeo mpya nchini Thailand.

Eric Kalume Ponda26 Novemba 2008

Mzozo wa kisiasa unaokumba serikali ya Thailand umechukua mwelekea mpya huku waandamanaji wa kundi la Peoples Alliance for Democracy waliouzingira Uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Bangkok.

https://p.dw.com/p/G2YX
Naafisa wa Usalama nchini Thailand wanaokabiliana na waandamanaji wa People`s Alliance for Democracy PAD, waliouzingira uwanja wa ndege wa Bangkok.Picha: AP


Waandamanaji hao wanasisitiza kuwa hawataondoka kutoka uwanja huo licha ya kutakiwa kufanya hivyo na kamanda mkuu wa jeshi la nchi hiyo.


Kamanda huyo wa jeshi Jemedari Anupong Paochinda anawataka waandamanaji hao kuondoka katika uwanja huo wa ndege, na seruikali kuitisha uchaguzi mpya ili kutanzua mzozo huo wa kisiasa.

Kiongozi wa kundi hilo la People´s Alliance for Democracy PAD, Pibhop Dhongchai ambaye wafuasi wake wanataka kuipindua serikali ya waziri mkuu Somchai Wongsawat, amesema kuwa wafuasi wake hawatabanduka hadi pale watakapofanya mazunguzo na upande wa serikali.


Uwanja huo wa ndege wa Suvarnabhumi umefungwa baada ya waandamanaji hao kuuvamia hapo jana na kutatiza safari za ndege ,hali iliyopelekea kukwama kwa maelfu ya watalii na na kuathiri sekta ya utalii nchini humo.


Ndege iliyombeba waziri mkuu huyo mkuu ambaye amekuwa akihudhuria mkutano wa viongozi kutoka eneo la Asia na Pacific kuhusu ushirikiano wa kibiashara nchini Peru, ililazimika kutua katika uwanja wa ndege wa kijeshi ulioko mjini Chiang Mai, kaskazini mwa nchi hiyo, kukwepa waandamanaji wanaouzingiza uwanja wa kimataifa.


Waandamanaji hao waliuzingiza uwanja huo wa ndege, katika juhudi za kumzuia waziri huyo mkuu kurejea nchini humo.


Kuna habari kwamba mtu mmoja aliuawa wakati wa ghasia zilizozuka baina ya maafisa wa usalama na waandamanaji hao punde tu waziri huyo mkuu alipowasili kutoka ziarani nchini Peru.


Waziri huyo mkuu bado hajazungumzia lolote kuhusiana na pendekezo la mkuu huyo wa jeshi la kumtaka aivunje serikali na kuitisha uchaguzi, ishara kwamba hayuko tayari kujiuzulu au kulivunja bunge. Msemaji wa waziri huyo mkuu Nattawut Sai-Gua alinukuliwa akisema kuwa huenda waziri huyo mkuu akashikilia msimamo wake na kubakia madarakani.


Hata hivyo Jemedari Anupong Paochinda amepuuzilia mbali uwezekano wa mapinduzi ya kijeshi, akisema kuwa hatua kama hiyo itakuwa na athari kubwa zaidi, na cha msingi ni kutoa nafasi ya mashauriano baina ya serikali na wafuasi wa kundi hilo la PAD.


Kundi hilo la PAD lilianzisha harakati za kuipinga serikali ya waziri mkuu Somchai Wongsawat kwa ufisadi, na kuendeleza udhalimu wa waziri mkuu wa zamani Thaksin Shinawatra anayeishi uhamishoni kufuatia mapinduzi ya kijeshi mnamo Septemba 19 2006.


Hata hivyo wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa mapinduzi hayo hayakufanikiwa kuwaodnoa washirika wa waziri huyo mkuu ambao walirejea madarakani wakati wa uchaguzi mkuu ulioitishwa mwaka Disemba 23 mwaka wa 2007.


Kiongozi huyo wa zamani yaaminika anausemi mkubwa katika serikali ya nwaziri mkuu Somchai, licha ya kuishi uhamishoni. Mwezi uliopita mahakama nchini humo ilimuhukumu kiongozi huyo wa zamani kifungo cha miaka miwili gerezani kwa kutumia vibaya mamlaka yake.