Mzozo wa kisiasa Bahrain | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.03.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mzozo wa kisiasa Bahrain

Mzozo wa kisiasa katika kisiwa cha Bahrain unaendelea kushika kasi, baada ya majeshi ya Saudi Arabia na Umoja wa falme ya nchi za kiarabu kupeleka majeshi yao kisiwani humo, kusaidia kuwadhibiti waandamanaji wa kishia.

default

Maelfu ya waandamanaji kisiwani Bahrain

Mzozo wa kisiasa katika kisiwa cha Bahrain unaendelea kushika kasi, baada ya majeshi ya Saudi Arabia na Umoja wa falme ya nchi za kiarabu kupeleka majeshi yao kisiwani humo, kusaidia kuwadhibiti waandamanaji wa madhehebu ya kishia,

Halima Nyanza na taarufa zaidi.

Zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Saudi Arabia wanaarifiwa kuweko Bahrain,huku Umoja wa falme wa nchi za kiarabu ukisema utapeleka askari polisi wapatao 500 ikiwa ni ombi kutoka kwa utawala wa Bahrain, baada ya wiki kadhaa za maandamano kuipinga serikali ya nchi hiyo pamoja na familia ya kifalme inayodhibiti kisiwa hicho.

Zaidi ya asilimia 60 ya wa-Bahrain ni kutoka jamii ya madhehebu ya Shia, ambao wamekuwa wakilalamika kunyanyaswa na familia ya kifalme ya madhehebu ya Sunni na kuitaka iondoke madarakani. Ambapo pia wanataka mageuzi katika demokrasia kutoka kwa Wasunni ambao ndio watawala wa nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 200 sasa.

Aidha ujio huo wa majeshi ya kigeni umekuja baada ya kutokea kwa mapigano makali katika maeneo tofauti ya Bahrain usiku wa kuamkia leo kati ya Wasunni na Washia.

Ghasia hizo ambazo zimekuwa zikitokea takriban kila siku kisiwani humo kwa wiki kadhaa sasa zimesababisha Chuo Kikuu cha Bahrain na shule nyingi kufungwa ili kuepuka machafuko hayo.

Hata hivyo, hatua hiyo ya kupelekwa kwa majeshi ya kigeni, Bahrain imeshutumiwa vikali na Iran na kusema kuwa ni jambo lisilokubalika.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Iran Ramin Mehmanparast amesema uwepo wa majeshi ya kigeni na kuingilia mambo ya ndani ya Bahrain ni jambo lisilokubalika na hali hiyo itaendelea kufanya mambo kuwa magumu zaidi.

Amesema watu wa Bahrain wanamatakwa yao, ambayo amesema kuwa ni halali na kwamba wamekuwa wakiyawasilisha kwa amani.

Ameongezea kusema kuwa machafuko yoyote yanakayotokea ikiwa ni kujibu madai hayo halali ya raia yanapaswa kuzuiwa.

Katika hatua nyingine, Marekani imesema majeshi ya kigeni kuingia katika kisiwa hicho sio uvamizi na kukataa kutoa wito wa kutaka yaondoke nchini humo.

Aidha katika mazungumzo yake na utawala wa Bahrain, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates alisema nchi yake haina uhakika kama Iran iko nyuma ya ghasia hizo.

Kumekuwa na tetesi kwamba Iran imekuwa ikiwaunga mkono wanaharakati hao wa Kishia nchini Bahrain, madai ambayo Iran imeyakanusha.

Utawala wa Wasunni nchini Bahrain umekuwa na wasiwasi kuwa madai ya kutaka utawala wa kifalme uondoke madarakani yatainufaisha Iran.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp, Reuters)

Mhariri: Abdul-Rahman,Moahammed

 • Tarehe 15.03.2011
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/10ZIS
 • Tarehe 15.03.2011
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/10ZIS

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com