Mwaka mmoja tangu shambulio kubwa la kigaidi la Bombay | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.11.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mwaka mmoja tangu shambulio kubwa la kigaidi la Bombay

Uchochezi wa vyombo vya habari uchwara nchini India

Wanajeshi wa India wapiga doria nje ya hoteli ya Oberoi Trident mjini Bombay(Mumbai) baada ya kufanyika shambulio la kigaidi katika mji huo mwaka mmoja uliopita

Wanajeshi wa India wapiga doria nje ya hoteli ya Oberoi Trident mjini Bombay(Mumbai) baada ya kufanyika shambulio la kigaidi katika mji huo mwaka mmoja uliopita

Mwaka mmoja uliopita, magaidi kumi wa kundi linaloitwa Lashkar-e-Taiba waliuvamia mji wa India wenye shughuli za kifedha, Bombay, na wakasababisha umwagaji mkubwa wa damu. Shambulio la kundi hilo lenye siasa kali za Kiislamu, lenye mizizi yake nchini Pakistan, na ambalo lina maingiliano na mtandao wa al-Qaida lilidumu siku tatu. Washambuliaji hao walifanya hujuma ya ustadi kabisa wa kijeshi dhidi ya mji huo, ambao ni alama ya India ya kisasa. Si chini ya watu 166 walikufa kutokana na risasi zilizofyetuliwa na magaidi hao. Wachunguzi wa mambo wanakisia kwamba idadi ya watu waliokufa ilikuwa kubwa zaidi kuliko ile iliotajwa. Kati ya washambuliaji ni mmoja tu wao aliyebaki hai, naye ni raia wa Ki-Pakistani anayetokea mkoa wa Punjab...

Shambulio hilo la Bombay lilivifanya vyombo vya habari vya huko India visijuwe cha kusema: vipi mtu aseme au aandike juu ya shambulio kubwa kabisa la kigaidi katika nchi yake mwenyewe, shambulio lilodumu siku tatu na kuchukuwa madarzeni ya roho za watu? Vipi mtu aseme juu ya shambulio ambalo umaarufu wake umeingia katika tarehe kwa kupewa jina la shambulio la 26 Novemba?

Katika miaka ya tisini, shughuli za redio ziliregezwa kamba na kupelekea huko India kuanzishwa zaidi ya televisheni za kibinafsi 500. Nyingi za televisheni hizo zinatangaza habari, tena zinafanya hivyo kwa saa 24 kwa siku. Ushindani kati ya vituo hivyo vya televisheni ni mkubwa na mkali. Stesheni hizo za televisheni zinategemea sana matangazo kwa mapato yao, lakini vijana wa kuendesha televisheni hizo wanakosekana.

Zikikabiliwa na shambulio hilo katika mji mkubwa wa shughuli za kifedha,vituo vingi vya habari vilishindwa kuwapatia wananchi habari za undani na za ukweli. Nyingi ya stesheni hizo zilionesha kwa masaa picha za moja kwa moja za mkasa huo, kiini zilikuwa picha za watu waliokufa na za maiti kadhaa. Pia mipango ya kimbinu ya polisi na majeshi ya usalama ilizungumziwa. Lakini nadra matokeo hayo yalifanyiwa utafiti wa mpangilio wenye maana. Wahariri wa habari walikumbana na amri za kutoka juu, ambazo ziliwataka wafikirie kwanza kabisa kuvutia idadi kubwa ya watazamaji wa vipindi vyao, hivyo vituo hivyo kujipatia mapato zaidi. Amri katika siku hizo ilikuwa: wachia kamera ionyeshe kila kitu mfululizo.

Yale masuala ya maadili ya uandishi wa habari yaliwekwa kando. Mwishowe watu walijuwa nani wa kulaumiwa: naye ni hasimu mkubwa, Pakistan. Mwanzoni vyombo vya habari vilizungumzia tu kwamba shambulio hilo lilipangwa katika ardhi ya Pakistan. Lakini kwa haraka, tetesi zikazagaa kwamba serekali ya Pakistan na pia idara ya kijasusi ya Pakistan zinaweza kuwa zilihusika na mkasa huo. Hata wakati wa hatua ya mwanzo ya shambulio hilo, kuna baadhi ya waandishi wa habari wa India waliotuhumu kwamba Pakistan ilikuwa nyuma ya hujuma hiyo. Duru zisizokuwa na uhakika na tetesi zilinukuliwa ili kuzitilia mkazo tuhuma hizo.

Hivyo, taarifa za habari ziliiweka serekali katika mbinyo. Mnamo masaa, hasira za wananchi zilikuwa kubwa hata kupelekea madola ya kinyukliya, India na Pakistan, kusimama ukingoni mwa mapambano ya kivita.

Kwa upande mwengine, magazeti ya Pakistan ambayo kutoka mwaka 2004 yamekuwa ya kiliberali, pia yalipandwa na mori. Nchi yao ilikuwa kizimbani. Yalisema ni uwongo kusema Pakistan imeshiriki kwa vyovyote katika shambulio hilo, na kwa haraka yakataja kwamba wa kulaumiwa ni Idara ya Ujasusi ya India, ambayo, kama ilivyo kawaida, inataka sababu ya kuendesha vita dhidi ya Pakistan. Kama ilivyokuwa huko India, nako huko Pakistan ushindi ulikuwa wa wale wanaochapisha habari za kutia chumvi na kungeza mori. Uchambuzi wa kina haujakuweko kuhusu kundi la kigaidi la Lashkar-e-Taiba na idara ya kijasusi ya jeshi la Pakistan. Matokeo ya lazima hayajaelezewa hadharani. Waandishi wa habari wachache walioripoti kwa undani juu ya mada hiyo, walipata shida ya kusikilizwa.

Mwaka mmoja baadae, sura ya vyombo vy ahabari katika India na Pakistan ni ya udanganyifu, haijafaulu kuyafanya majadiliano kuhusu shambulio hilo kuwa yenye kuangalia msingi wa tokeo hilio. Kutokana na kupotoshwa majadiliano juu ya mkasa huo, mara kadhaa serekali imetishia kuvipiga mkasa vyombo vya habari, kama mfano wa shambulio la Bombay, pindi vitaripoti mambo ambayo yataharisha usalama wa taifa. Lakini haijafikia kiwango cha kuuwekea vizuwizi uhuru wa magazeti. Huenda tu kwa vile serekali inahitaji msaada wa vyombo vya habari katika vita vyake vya propaganda dhidi ya Pakistan.

Kilichobaki ni kwamba vyombo vya habari, kutokana na hali hiyo, hujipa jukumu la kuishauri serekali na kukubaliana nayo nini cha kiripoti. Hivyo, kuzifanya pande zote mbili zitosheke. Kwa upande mwengine, katika mpaka na Pakistan, chuki za kizalendo dhidi ya jirani India zinaendelezwa, kama vile serekali inavotaka.

Kwamba ule mwenendo wa amani baina ya nchi mbili hizo, ambao ulisita kutokana na shambulio la kigaidi la Bombay, haujaibuka tena ni kutokana na fikra za wananchi wa nchi zote mbili. Utamaduni wa vyombo vya habari ambao kila upande unaulaumu upande wa pili umetia mizizi. Majadiliano katika televisheni na redio kila wakati yanawaonesha maafisa wa zamani wa jeshi na mabingwa wa uslama wakizungumzia hatari ilioko mpakani. Mbinyo wa kutaka yariopotiwe mambo yanayowatia watu hamasa na jazba unapata makali. Yote ni kuwavutia watu waangalie televisheni, hivyo matangazo ya biashara. Hamna mtu yeyote anayeza kuona kwamba lengo la muda wa wastani ni kuwa na vipimo bora vya uandishi wa habari katika viwanda vya vyombo vya habari vya nchi zote mbili, na pia kutoa mafunzo yalio bora kwa wahariri chipukizi.

Mwandishi: Grahame Lucas/Miraji Othman/ZP

Mhariri: Mohammed Abdulrahman

 • Tarehe 25.11.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KgJt
 • Tarehe 25.11.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KgJt
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com