Mshikemshike wa Bundesliga sasa ni kugombea daraja | Michezo | DW | 06.05.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Mshikemshike wa Bundesliga sasa ni kugombea daraja

Ligi ya Ujerumani, Bundesliga, yaingia wiki ya 33, huku kinyanyang'anyiro hasa kikiwa ni kuwania kutoshuka daraja na sio mshindi, kwani ameshajuilkana kuwa ni Borussia Dortmund

Mohamadou Idrissou wa Borussia Mönchengladbach

Mohamadou Idrissou wa Borussia Mönchengladbach

Sasa mashabiki hawaangalii tena kuhusu Dortmund ama Leverkusen, badala yake katika sehemu ya mwisho ya msimamo wa ligi.

Katika sehemu hiyo kuna kila kitu kinachohitajika katika kutia hamasa viwanjani. Mpambano ambao ni ni wa vuta-nikuvute leo (Jumamosi 7 Aprili 2011) ni baina ya Eintracht kutoka Frankfurt, ambayo chini ya kocha wao Christoph Daum, bado bundi ameendelea kutua katika paa lao na haijashinda tangu sehemu ya pili ya ligi kuanza mwanzoni mwa mwaka huu.

Eintracht inaumana na FC Köln, ambayo mwishoni mwa juma lililopita ilipata ushindi mnono dhidi ya watani wao wa jadi Leverkusen na kuisafishia njia Borussia Dortmund kunyakua ubingwa, ikiwa bado michezo miwili.

Tofauti ya timu hizi mbili katika msimamo wa ligi ni pointi tatu. Köln ikiwa na point tatu zaidi ya Frankfurt ambayo inafundishwa na kocha wa zamani wa Köln, na mchezo huu unakila hali ya kutoa matokeo ambayo yatakuwa majaliwa ya Frankfurt, kushuka ama kupata tamaa ya kubakia katika daraja la kwanza msimu ujao.

Wachezaji wa Borussia Möenchengladbach wanafahamu kila hali ya mchezo ambao ni nafasi ya mwisho. Kwa muda mrefu wamekuwa wakiburura mkia katika msimamo wa ligi ya Bundesliga, lakini hadi sasa hakuna mtu ambaye anaikatia tamaa kabisa Möenchengladbach. Mabingwa wateule Dortmund na Hannover walishangazwa na timu hii baada ya kupokea vipigo na hatimaye timu hii kuondoka katika nafasi hiyo ya nuksi.

Na sasa timu inayoingia uwanjani jioni dhidi ya Möenchengladbach ni Freiburg, anasema mshambuliaji Mike Hanke.

"Mchezo wa leo unaumuhimu mkubwa kwetu. Ni kama fainali. Lakini tumeona katika wiki zilizopita, kwamba tunaweza kuhimili vishindo. Wapinzani wetu wote wawili walikuwa ni timu ngumu, tumezishinda.Nafikiri tukicheza kwa kujiamini zaidi , tunaweza pia kuishinda Freiburg."

Katika nafasi hiyo pia wapo VfL Wolfsburg ikiwa katika nafasi ya 15 ikiwa na point moja tu zaidi kutoka katika eneo la hatari. Ikiwa na mchezo wa nyumbani hii leo Mabweha hao wanawakaribisha mashetani wekundu, Kaiserslautern, ambao tayari wamepata salama tangu wiki iliyopita na sasa hawana shaka tena ya kushuka daraja.

Hali ngumu inawakabili lakini Werder Bremen wakiwa katika nafasi ya 13 na points 38, wanawakaribisha mabingwa wateule Borussia Dortmund, ambao huenda wasiweke ushindani mkubwa hii leo na hali hiyo ikawasaidia Bremen.

Bahati waliyonayo Bremen huenda isiwakute Stuttgart, ambayo ikiwa na points 39 inaumana na Hannover, ambao wanawania nafasi ya tatu ya champions league pamoja na Bayern Munich. Hannover iko nafasi ya nne kutoka juu.

Ikiwa imeshinda michezo miwili mfululizo, Bayern inaweza kwa nguvu zake kuzuwia msimu ambao kwao ni maafa makubwa kwa kupata nafasi hiyo ya tatu ambayo itawasaidia kuingia katika kinyang'anyiro cha Champions League msimu ujao. Bayern wanapambana na timu iliyokwisha nyoosha mikoni juu na kuaga bundesliga St.Pauli.

Mlinzi Holger Badstuber wa Bayern hana wasi wasi tena wa kuitaka Hannover ifungwe na Stuttgart ili wao waweze kusonga mbele.

"Hatuwezi tena kutegemea kuteleza kwa Hannover dhidi ya Stuttgart, licha ya kuwa watapata upinzani mkubwa. Tunapaswa kuchukua points tatu ili tuweze kuwa na uhakika wa kupata nafasi ya tatu. Baada ya hapo kila kitu kitakuwa ni sawa tu."

Michezo mingine hii leo ni kati ya Schalke 04 ambayo imeyaaga mashindano ya Champions League kwa kukandikwa mabao 6-1 na Manchester United wiki hii, Schalke inacheza na Mainz 05. SV Hamburg inapambana na Bayer Leverkusen . FC Nürnberg inakwaana jioni hii na Hoffenheim.

Mwandishi: Sekione Kitojo/DPAE/RTRE/AFPE/Fritz,Olivia DW(Sport)
Mhariri: Hamidou Oummilkheir

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com