Mkuu wa usalama wizara ya mambo ya nje Marekani ajiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkuu wa usalama wizara ya mambo ya nje Marekani ajiuzulu

Mkuu wa usalama katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani amejiuzulu kutokana na shutuma juu ya usimamizi mbaya wa ofisi yake kwa kampuni binafsi za usalama nchini Iraq baada ya walinzi wa kampuni ya Blackwater kuwauwa kwa kuwapiga risasi raia kadhaa.

Walinzi wa kampuni ya Blackwater nchini Iraq mzozo wao nchini humo wapelekea kujiuzulu kwa mkuu wa usalama katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Walinzi wa kampuni ya Blackwater nchini Iraq mzozo wao nchini humo wapelekea kujiuzulu kwa mkuu wa usalama katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema Richard Griffin hakutowa sababu ya kujiuzulu wadhifa huo wa msaidizi waziri katika Ofisi ya Usalama wa Kidiplomasia lakini amesema tu kwamba alikuwa akitaka kusonga mbele kukabiliana na changamoto mpya.

Msemaji huyo wa kike Julie Reside amesema Griffin amewasilisha barua yake ya kujiuzulu hapo jana na kuongeza kusema kwamba waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice amekubali kujiuzulu kwake.

Rice aliulizwa juu ya kujiuzulu kwa Griffin wakati akikutana na Naibu Waziri Mkuu wa Iraq Barham Salih lakini amesema tu kwamba anamshukuru sana mkuu huyo wa usalama kwa huduma yake ya kupigiwa mfano.

Kujiuzulu kwake kunakuja siku moja baada ya kutolewa kwa repoti ya ndani kwenye wizara ya mambo ya nje yenye kutaka kuwepo kwa udhibiti mkali zaidi kwa kampuni binafsi za usalama nchini Iraq kufuatia matukio kadhaa ya maafa nchini Iraq.

Katika tukio baya kabisa walinzi wa kampuni ya Blackwater waliokuwa wakiulinda msafara wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani waliufyatulia risasi umati wa watu mjini Baghdad hapo terehe 16 mwezi wa Septemba na kuuwa takriban raia 17.

Katika kile kinachoonekana kama onyo repoti ya jopo la wizara ya mambo ya nje imesisitiza kwamba kampuni binafsi zinapaswa tu kufyetuwa risasi kwa kuzingatia usalama wa watu wasiokuwa na hatia walioko karibu nao.

Mauaji hayo yanaonyesha wazi kutokuwepo kwa uwajibikaji kwa kampuni za Kimarekani zinazoifanyia kazi wizara ya mambo ya nje tafauti na vile ilivyo kwa wizara ya ulinzi ya Marekani ambapo wafanyakazi wake wa kibinafsi wanalindwa na sheria za kijeshi za Marekani.

Repoti ya jopo hilo inasema wizara ya mambo ya nje inapaswa kuwasiliana kwa haraka na wizara ya Sheria na Bunge la Marekani kuweka msingi wa kisheria wa kuziwajibisha kampuni kwa kuzingatia sheria ya Marekani.

Lakini repoti hiyo imemalizia kwa kusema kwamba wizara ya mambo ya nje ya Marekani haiwezi kuendeleza shughuli zake bila ya kampuni hizo binafsi kwa vile maafisa wake binafsi wa usalama hawazidi 1,500 duniani kote na jeshi la Marekani limetingwa mno kumudu kutowa ulinzi wa kidiplomasia.

Rice leo anatazamiwa kuhojiwa na kamati ya uangalizi ya serikali katika baraza la wawakilishi juu ya utendaji wa kampuni hizo za usalama.

Kwa miezi kadhaa mwenyekiti wa kamati hiyo Henrry Waxmann amekuwa akidai kupatiwa maelfu ya nyaraka kutoka ofisi ya Rice kuhusiana na namna wizara yake inavyofanya kazi na kampuni hizo za usalama kama vile ya Blackwater na DynCorp International.

Gazeti la New York Times limesema hapo Jumanne ukaguzi wa mahesabu wa Mkaguzi Mkuu Maalum wa serikali kwa Ukarabati wa Iraq umelenga dola bilioni 1.2 kwenye kondarasi ilizopewa kampuni ya DynCorp na wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

 • Tarehe 25.10.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7gJ
 • Tarehe 25.10.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7gJ

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com