Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Javier Solana yuko Georgia | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Javier Solana yuko Georgia

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Javier Solana amesema leo hii anatarajia Urusi itaheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Georgia kufuatia kuwasili kwake katika nchi hiyo ilioathirika na vita.

default

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Javier Solana.

Solana amewasili Georgia kabla ya kuwekwa kwa waangalizi wa amani wa Umoja wa Ulaya.

Ziara hiyo ya Solana inatiwa kiwingu na onyo la Urusi kwamba waangalizi hao wa amani wa Umoja wa Ulaya hawatoruhusiwa mara moja kuingia katika ukanda wake wa usalama ndani ya Georgia.

Solana amekaririwa akisema kabla ya kuanza kuwekwa rasmi kwa waangalizi wa Umoja wa Ulaya kusimamia amani huko Georgia baada ya vita vyake vya mwezi wa Augusti na Urusi kwamba ana matumaini pande zote husika zitatimiza kama walivyofanya wao masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Serikali ya Urusi imesema hapo awali kwamba waangalizi hao wa amani wa Umoja wa Ulaya hawatoruhisiwa kuingia mara moja maeneo ya kuzuwiya mapigano yanayodhibitiwa na Urusi karibu na jimbo lililojitenga la Ossetia Kusini wakati watakapoanza kuwekwa hapo kesho Jumatano.

Shirika la habari la Interfax la Urusi limemkariri msemaji wa vikosi vya Urusi huko Ossetia Kusini Vitaly Manushko akisema kwamba waangalizi hao wa Ulaya watapiga doria hadi kwenye ukingo wa mwisho wa kanda ya usalama chini ya makubaliano yaliofikiwa kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi leo hii.

Ameongeza kusema waangalizi hao watakuwa hawana silaha na hawatoanzisha vituo vya ukaguzi.

Baada ya kuwasili katika mji mkuu wa Georgia Tbilisi Solana alikuwa akitarajiwa kukutana na Rais Mikheil Sakashvili na kuwahutubia waangalizi wa Umoja wa Ulaya wanaoshiriki katika shughuli hizo za kulinda amani.

Solana pia anatarajiwa kwenda kwenye mji wa Georgia wa Gori karibu na jimbo la waasi la Ossetia Kusini kutembelea ofisi ya shughuli za waangalizi wa amani wa umoja huo pamoja na kukutana na wakimbizi.

Kile kinachojulikana kama Kikosi cha Waangalizi cha Umoja wa Ulaya chenye takriban watu 200 kinakusudia kuleta utulivu katika eneo hilo na kuhakikisha kwamba Georgia na Urusi zinatimiza mpango wa amani uliofikiwa chini ya udhamini wa Umoja wa Ulaya.

Wizara ya mambo ya nje wa Ujerumani pia anauangalia kwa matumaini mpango huo.

Imesema hatua ya kwanza muhimu ni kwa mpango huo kuona waangalizi wanawekwa katika kile kinachojulikana kama kanda zisizoruhusiwa mapigano kati ya Ossetia Kusini au Abkhazia na eneo lililobakia la Georgia na hatimae wangelipenda kuona waangalizi hao wa Umoja wa Ulaya wanakuwa huru kwenda nchini kote Georgia na kufanya kazi zao ipasavyo.

Wengi wa waangalizi hao wana historia ya kufanya kazi katika polisi au jeshi wakiwemo kikosi kikubwa cha wanajeshi wa Ufaransa wakati wengine ni wataalamu wa masuala ya haki za binadaamu na mahkama.

Leo Abkhazia inashehrekea miaka 15 ya ushindi wake dhidi ya vikosi vya Georgia katika vita vya kutaka kujitenga kwa jimbo hilo.

Urusi imeyatambuwa majimbo hayo yaliojitenga ya Ossetia Kusini na Abkahzia kuwa ni mataifa huru.

 • Tarehe 30.09.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FRnL
 • Tarehe 30.09.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FRnL
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com