Mkutano wa viongozi wa Irak kufanyika katika siku mbili zijazo | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.08.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa viongozi wa Irak kufanyika katika siku mbili zijazo

Waziri mkuu wa Irak Nuri al Malik ameitisha mkutano wa wakuu wa makundi mbali mbali ya kisiasa na kijamii nchini humo katika jitihada za kuikoa serikali yake ambayo inakabiliwa na migawanyiko ya kisiasa.

Waziri mkuu wa Irak Nuri al Malik

Waziri mkuu wa Irak Nuri al Malik

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika katika siku mbili zijazo.

Waziri mkuu Nuri al Malik ambae serikali yake ya umoja wa kitaifa inakabiliwa na mgawanyiko tangu kundi kubwa la Kisunni lilipo jitoa kutoka serikalini amesema atajaribu kulishawishi kundi hilo kurejea serikalini la sivyo atalazimika kutafuta washirika wengine watakao chukuwa mahala pa kundi hilo.

Irak inakabiliwa na mzozo wa kisiasa wa ndani ambao umemlazimu waziri mkuu Nuri al Malik kuitisha mkutano wa viongozi ili kutafuta suluhisho la mgongano wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Katika muda wa wiki kadhaa zilizopita takriban mawaziri wote wa madhehebu ya Kisunni wamejiuzulu kutoka kwenye baraza la mawaziri na wengine wanasusia vikao na kuuacha ukumbi wa baraza la mawaziri kuwa na viti vitupu 17 kila baraza la mawaziri linapokutana.

Mawaziri wengi wanamlaumu waziri mkuu Nuri al Malik kwa kupuuza madai yao.

Mkutano huo wa dharura utawajumuisha pamoja rais Jalal Talabani ambae ni Mkurdi, waziri mkuu Nuri al Malik kutoka madhehebu ya Shia makamu wa rais Tareq al Hashemi wa madhehebu ya Sunni kiongozi wa jimbo la Kurdistan Masoud Barzani na msaidizi wa kiongozi wa Kishia Abdul Aziz al Hakim.

Viongozi hao watajadili njia zitakazowezesha kumaliza magawanyiko wa kisiasa ulio izorotesha serikali ya Irak kwa miezi kadhaa sasa.

Waziri mkuu Nuri al Malik hawezi kuendeleza mpango wa maridhiano bila ya ushirikiano wa makundi mbali mbali ya nchini Irak.

Migawanyiko ilikithiri pale kundi kubwa la Sunni lilipojiondoa kutoka serikalini tarehe 1 mwezi huu wa Agosti, wiki iliyopita vilevile mawaziri wengine watano watiifu kwa waziri mkuu wa zamani Iyad Allawi walianza kususia vikao vya baraza la mawaziri.

Ikiwa ni pamoja na wajumbe wa madhehebu ya Shia wafuasi wa Moqtada al Sadr waliojitoa kutoka kwenye serikali miezi kadhaa iliyopita.

Lakini licha ya mkutano huu wa viongozi kuitishwa na waziri mkuu Nuri al Malik haimaanishi kwamba makubaliano yatafikiwa.

Wakati huo huo wimbi jipya la mashambulio limeibuka, leo hii takriban askari polisi watano wameuwawa katika eneo lenye ulinzi mkali la Green Zone mjini Baghdad eneo hilo ndiko anakoishi waziri mkuu wa Irak Nuri al Malik na mabalozi wa nchi za kigeni.

Kwingineko wakaazi wa mji wa Diwaniya ulio kusini mwa Irak wameeleza wasiwasi wao kuhusu kuzuka mapigano baina ya makundi yanayopingana ya Kishia hasa baada ya kuuwawa mwishoni mwa wiki gavana wa jimbo hilo la Diwaniya Khalil Jalil Hamza na mkuu wa polisi jenerali Khaled Hassan. Viongozi hao waliuwawa kwenye mlipuko wa bomu lililo tegwa kando ya barabara.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com