Mkutano wa Vienna, kuhusu ukimwi. | Masuala ya Jamii | DW | 21.07.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Mkutano wa Vienna, kuhusu ukimwi.

Mkutano wa Kimataifa kuhusu ukimwi unaendelea leo, baada ya jana usiku maelfu ya wanaharakati wa masuala ya ukimwi kuandamana mjini Vienna kunakofanyikia mkutano huo, wakidai haki zaidi kwa watu walioathiriwa.

default

Mkutano wa kimataifa wa ukimwi, Vienna Austria.

Maandamano hayo makubwa ambayo yaliandaliwa na kuhudhuriwa na wajumbe wa mkutano huo wa kimataifa kuhusu ukimwi, yaliongozwa na mkurugenzi wa jumuia ya kimataifa ya ukimwi IAS, ambao ndio waratibu wa mkutano huo wa Vienna, sambamba na mkuu wa shirika la umoja wa mataifa kuhusu ukimwi UNAIDS Michel Sidibe pamoja na mkuu wa mfuko wa kupambana na ukimwi, kifua kikuu na malaria Michel Kayzatchkine.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, mkuu wa mfuko wa dunia wa kupambana na ukimwi, kifua kikuu na malaria Michel Kazatchkine amesema hata kama kuna rasilimali na teknolojia, mafanikio hayatakuwepo katika kutibu wagonjwa kama haki za binadamu hazitoheshimiwa.

Maandamano hayo makubwa ya jana yalihudhuriwa pia na muimbaji na mwanaharakati wa masuala ya ukimwi wi, mwanamuziki Annie Lennox ambaye aliimba nyimbo chache, lakini pia alizikosoa serikali za Ulaya mashariki ambako maambukizo ya ukimwi yanaongezeka kwa kasi, kwa kuziuliza ziko wapi?, kutokana na kwamba janga hilo limewafikia na wao wanapuuzia.

Maandamano hayo pia yalihudhuriwa na dada wa Rais wa Marekani Barack Obama, Auma Obama, ambaye analifanyia kazi shirika la Care la Marekani linaloshughulika na mapambano ya ukimwi nchini Kenya.

Kauli mbiu katika mkutano hio wa Vienna inasema ''haki hapa, sasa hivi''.

Katika hatua nyingine Shirika la Afya duniani WHO limesema madawa yanayosaidia kupunguza makali ya virusi vya HIV, yamewafikia watoto 355, 000 mpaka mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2009, ikilinganishwa na 276,000 katika mwaka wa 2008.

Lakini hata hivyo shirika hilo limesema maisha ya watoto hao yangeokolewa zaidi iwapo matibabu ya madawa hayo yangeanza mapema.

WHO imetoa takwimu hizo katika mkutano huo wa 18 wa kimataifa kuhusu ukimwi mjini Vienna, ambako zaidi ya wanasayansi, watunga sera na wafanyakazi wengine wa masuala ya ukimwi 20,000 wanahudhuria.

Mkutano huo utamalizika siku ya Ijumaa wiki hii.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa katika makadirio yake ya mwaka 2008, Zaidi ya watu milioni 33 duniani kote wameambukizwa virusi vya HIV, vinavyosababisha ukimwi.

Katika mwaka huo watu milioni 2.7 waliambukizwa na laki nne kati ya hao walikuwa watoto wa chini ya umri wa miaka 15.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp,ap)

Mhariri:

 • Tarehe 21.07.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OQf3
 • Tarehe 21.07.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OQf3
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com