1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Mazingira-Bonn

12 Agosti 2009

Kama wajumbe 2,000 kutoka takriban nchi 190 wanakutana mjini Bonn Ujerumani kuendelea na majadiliano yanayohusika na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuweza kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

https://p.dw.com/p/J8aI

Mikutano inayofanyika mjini Bonn ni maendeleo ya majadiliano yanayotayarisha mswada wa mkataba utakaowasilishwa katika mkutano wa kilele mjini Copenhagen nchini Denmark mnamo mwezi wa Desemba. Katika mkutano wa Copenhagen, viongozi wanatazamiwa kutia saini mkataba mpya utakaochukua nafasi ya Mkataba wa Kyoto unaomalizika mwaka 2012.

Lengo la mkataba huo mpya ni kupunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira ambazo kwa sehemu fulani hulaumiwa kusababisha ongezeko la joto duniani. Mkataba huo pia utazingatia njia ya kuzisaidia nchi zinazoathirika zaidi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Jumla ya nchi 192 zinapaswa kutia saini mswada wa mkataba mpya ili uweze kuwasilishwa mjini Copenhagen.

Nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda isipokuwa Marekani ambayo haikutia saini Mkataba wa Kyoto, zinatazamia kupunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira kwa asilimia 15 hadi asilimia 21 ifikapo mwaka 2020 na hivyo, kufikia vile viwango vya mwaka 1990. Lakini vipimo hivyo havifikii viwango vilivyopendekezwa na jopo la wanasayansi wa Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa wataalamu hao, utoaji wa gesi hizo unahitaji kupunguzwa kwa kiwango cha asilimia 25 hadi 40 ili kuweza kuzuia ongezeko la joto linalosababisha ukame,mafuriko na kuongezeka kwa usawa wa bahari.

Mkuu wa kitengo cha mabadiliko ya hali ya hewa katika Umoja wa Mataifa Yvo De Boer amesema, hizo ni hesabu zilizokadiriwa ili kuonyesha haja ya kuwepo mkakati wa muda mrefu wa kuhifadhi mazingira. Amesema, mkakati huo utagharimu fedha nyingi sana, lakini mfumo wa kusaidiana kubeba mzigo huo ndio kilicho muhimu. Hata hivyo, nchi zinazoinukia kiuchumi kama vile China na India, zinashikilia kuwa kabla ya nchi hizo kukubali kuchukua hatua zaidi za kupunguza viwango vya gesi zinazochafua hewa, nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda kwanza ziahidi kuwa zitatoa msaada wa fedha.

Sweden iliyoshika wadhifa wa urais unaozunguka katika Umoja wa Ulaya, imefurahishwa na ukweli kuwa katika mkutano wa mwezi uliopita nchini Italia,wachafuzi wakuu wa mazingira zikiwemo nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda G-8 pamoja na China na India walikubaliana na pendekezo la wanasayansi kuwa ogezeko la joto duniani lisivuke nyuzi joto 2 za Celsius. Majadiliano ya mjini Bonn yanayotayarisha mswada wa mkataba mpya wa mazingira yanatazamiwa kumalizika Agosti 14.

Mwandishi: P.Martin/RTRE/DPA

Mhariri: M.Abdul-Rahman