Mkutano wa kiuchumi wa nchi za Kiislamu wafunguliwa. | Masuala ya Jamii | DW | 02.03.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Mkutano wa kiuchumi wa nchi za Kiislamu wafunguliwa.

Mkutano wa mwaka wa kiuchumi wa nchi za Kiislamu duniani umefunguliwa rasmi leo mjini Jakarta, Indonesia, na Rais wa Indonesia, Susilo Bambang Yudhoyono, pamoja na Waziri Mkuu wa Malaysia, Abdullah Ahmad Badawi.

default

Moja wapo ya Benki za Kiislamu nchini Malaysia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Waziri Mkuu wa Malaysia, Abdullah Ahmad Badawi, ameshutumu kile alichokiita 'uroho usiokuwa na mipaka'', uliosababisha kuwepo mgogoro wa fedha duniani, na kutoa wito wa kuweko mfumo mpya wa fedha kuchukua nafasi ya mfumo wa masoko ya hisa.


Amesema tumerithi mfumo ambao watu wanafanya biashara kutokana na kile ambacho hawamiliki, na matokeo yake kushurutisha mfumuko wa bei katika soko la dunia kunasababisha hasara kubwa katika uchumi.


Kwa upande wake, Rais wa Indonesia, Susilo Bambang Yudhoyono, ameonya dhidi ya mwelekeo wowote kuelekea sera ya kila nchi kulinda viwanda vyake na katika kipindi hiki cha kukabiliana na kuporomoka uchumi na kutoa wito wa yakamilishwe mazunghumzo ya hivi karibuni ya Shirika la biashara Duniani -WTO- yaliyokusudiwa kuleta muwafaka juu ya biashara ya dunia nzima na kuondosha vizingiti.


Wakati huohuo, akizungumza jana katika Mkutano wa Maandalizi wa mkutano huo, Makamu wa Rais wa Indonesia, Jusuf Kalla, amesema uendeshaji wa benki za Kiislamu umeepukana na mgogoro wa kiuchumi ulioikumba dunia kiasi bila ya kuathiriwa, akilinganisha na pigo lililokumba mfumo wa fedha wa nchi za magharibi.


Amesema mgogoro wa fedha wa hivi karibuni umetufundisha kuwa mfumo wa uchumi ambao umejikita katika makubaliano ya kibiashara yasiyo ya kweli utakuwa rahisi kufilisika.


Makamu wa Rais wa Indonesia aliendelea kusema kuwa uendeshaji wa shughuli za benki za kiislamu na mfumo wa fedha vimeonesha uwezo wake kwa kukwepa kwa kiasi na kutoathiriwa na mgogoro wa fedha duniani.


Ameongeza kusema kuwa nchi za kiislamu ambazo zinafuata mfumo wa kiuchumi wa kiislamu hazijaathiriwa sana na tatizo hilo kubwa lililokumba dunia.


Bwana Jusuf Kalla amesema uendeshaji wa shughuli za benki kiislamu umestawi kufikia dola trilioni 1.0, ambapo ulanguzi unakatazwa na pia kiwango kikubwa cha madeni.


Sheria za sekta hiyo, ambayo inashirikisha maadili ya sheria za kiislamu, zinakataza shughuli nyingi za hatari ambazo zinachochea mgogoro wa kuanguka uchumi duniani.


Sheria za kiislamu zinakataza malipo na utozaji riba, hali ambayo inaonekana ni chanzo cha mchezo wa kamari.


Mkutano huo wa tano wa mwaka wa wa kiuchumi wa nchi za kiislamu, ambao umekuwa ukifanyika toka mwaka 2004, unaowakutanisha pamoja viongozi mbalimbali na wafanyabiashara kutoka nchi za kiislamu, unalenga kubadili mtazamo wa dunia kwa ulimwengu wa kiislamu kutoka katika eneo lenye migogoro kuwa kanda yenye kuleta faida kubwa, kiuchumi.


Aidha mkutano huo unalenga kuendeleza fursa ya biashara na vitega uchumi katika ulimwengu wa kiislamu.


Mkutano huo umehudhuriwa na karibi viongozi 80 wa nchi, mawaziri wa serikali pamoja na viongozi wa mashirika mbalimbali kutoka nchi zipatazo 30 duniani, na utalenga zaidi kuzungumzia masuala ya Chakula, nishati, mazingira na usalama wa fedha pamoja na biashara ndogondogo.


 • Tarehe 02.03.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza/AFP
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H3rE
 • Tarehe 02.03.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza/AFP
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H3rE
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com